NA GOODLUCK HONGO
NI miaka 24 imepita tangu Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Laurent Kabila kuuawa kwa kupigwa risasi Ikulu nchini humo.
Kabila aliuawa mnano Januari 8,2001 akiwa Ikulu jijini Kinshasa na walinzi wake ambao walikuwa na jukumu la kumlinda kabla ya kusaliti kiapo chao na kumuua.
Kabila alizaliwa Novemba 27,1939 na aliingia madarakani mnamo Mei 1997 kuiongoza DRC baada ya kuongoza muungano wa makundi ya wapiganaji yaliyojumuishwa na kuitwa Alliance des Forces Democratiques pour la Liberation du Congo-Zaire (AFDL)
Hata hivyo Kabila ndiye Rais aliyebadili jina la nchi hiyo iliyokuwa ikiitwa Zaire na kuiita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati ikiitwa Zaire Hayati Mobutu Sese Seko aliyekuwa Rais wa pili baada uhuru.
Kabila alianzisha uasi wa kumundoa Mobutu baada ya kuungwa mkono na Rwanda na Uganda wakati huo Uganda ikisumbuliwa na waasi wa Lord Resistance Army (LRA) huku Rwanda wakipambana na waasi wa Kihutu ambao walihusishwa na mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994 na kukimbilia nchini DRC baada ya Jeshi la RPF likiongozwa na Paul Kagame kuwafurusha.
Hata hivyo Rwanda na Uganda walimuunga mkono Kabila ili na wao waweze kuwathibiti waasi waliokuwa wakisumbua nchi zao kutoka ardhi ya DRC na hapo ndipo vita vilipoanza hadi Kabila kufanikiwa kuingia Ikulu Kinshasa.
Kabila alifanikiwa kwa haraka kuchukua madaraka kutokana uongozi wa mtangaulizi wake Mobutu Sese Seko ambaye alijulikana kama Rais wa Kinshasa na raia wengi wa DRC
Mobutu aliitwa Rais wa Kinshasa kutoka na yeye kulijenga jiji la Kinshasa na kuacha kupeleka maendeleo katika maeneo mengine ya DRC ambapo moja ya kitu kinachokumbukwa kilichofanywa na Hayati Mobutu ni kujenga minara mitatu mirefu katika jiji hilo lenye wakazi zaidi ya Milioni 10 ili inapofika jioni aweze kupumzia na kuliangalia jiji hilo akiwa juu lakini hakufanikiwa kukamilisha mradi huo baada ya kupinduliwa.
Minara hiyo mitatu na eneo lake ilimaliziwa na kuwa sehemu ya Makumbusho ya Taifa ambapo kazi hiyo ilifanywa na Serikali iliyoingia madarakani baada ya kuuawa kwa Rais Kabila
Kabila pia alipata urahisi wa kuingia Ikulu kutokana na Jeshi la DRC wakati huo ikiitwa Zaire kuwa dhaifu kutoka na mfumo wa utawala wa Mobutu uliopendelea upande mmoja wa nchi na kuacha upande mwingine hivyo Jeshi kushindwa kuwa na Komandi Kuu moja kwa nchi nzima.
Kutokana na mfumo wa utawala wa Mobutu hali hiyo imeendelea kuwaathiri raia wa nchi hiyo ambapo ikiwa Kiongozi anatokea Kinshasa na maeneo ya karibu basi huonekana kuwa ndio mkongomani halisi lakini akitokea maeneo nje ya eneo hilo huokenana kama sio mkongomani.
Rwanda na Uganda zilimdanganya Kabila?
Miezi kadhaa baada ya Kabila kuingia Ikulu,ulitokea uasi mkubwa wa kutaka kumpindua Rais Laurent Kabila ambaye aliamua kuomba usaidizi katika nchi za Angola ikiwemo na Zimbabwe zilizotuma majeshi yao kupambana na waasi hao ambapo mapigano makali yalishuhudiwa hadi waasi waliposhindwa na Kabila kuendelea kutawala.
Habari kutoka Kinshasa zinaeleza kuwa vita vilivyozuka ili kumuondoa Kabila vilitokana na Rais huyo kuwaeleza Rwanda na Uganda kuwa waondoe vikosi vyao nchini humo kwa kuwa ni muda mrefu umepita hivyo watakuwa tayari wameshawakamata waasi hao na kuwarudisha makwao kwa hatua zingine watakazochukua
Wakati vita vya kumuondoa Mobutu vikiendelea,Rwanda na Uganda ambavyo vilikuwa na vikosi vingi vya kijeshi vilidhibiti maeneo mengi ambayo yalitekwa kutoka kwa vikosi vya kijeshi vya Serikali ya Mobutu.
Baada ya harakati hizo za Rais Kabila kulazimisha Rwanda na Uganda kuondoa vikosi vyao ndipo Rwanda na Uganda zilidaiwa kugoma kuondoa vikosi vyao na hapo ndio ukawa mwanzo wa Rwanda na Uganda kuikalia DRC kwa kisingizio kile kile cha kulinda usalama wa nchi zao na kuunga mkono makundi ya waasi katika maeneo waliyoyateka wakati wa kumuondoa Hayati Mobutu.

Angola,Zimbabwe na nchi zingine zilisaidia kuzima uasi na jaribio la kumuondoa Rais Kabila Baada ya mapigano kumalizika hatimaye Januari 8,2001 wauaji wasiokuwa na huruma wala aibu ambao ni walinzi wa Rais walimpiga risasi Laurent Kabila na kumuua ambapo muuaji aliyetekeleza shambulio alianza kukimbia lakini alidaiwa kuuwa baadaye na walinzi wengine wenye nidhamu,utii,heshima na utu.
Licha ya kuuawa kwa mlinzi huyo ambaye alikuwa akikimbia katika eneo la Ikulu baada ya kutekeleza mauaji hayo,lakini badala ya muuaji huyo kukamatwa ili atoe maelezo ya waliomtuma na sababu za kumuua Rais wa nchi naye aliuliwa kwa kupigwa risasi hali iliyoacha fumbo hadi sasa kwa wahusika kujulikana zaidi.
Hayati Kabila alizikwa mbele ya Ikulu ya nchi hiyo siku kadhaa baada ya kuuawa ambapo mwili wake ulihifadhi katika kaburi la kioo na kufunikwa kwa Bendera ya Taifa ya DRC na kisha mwanawe Joseph Kabila kukabidhiwa madaraka ya kuiongoza DRC
Hata hivyo Kaburi hilo haijulikani kama bado lipo mbele ya Ikulu ya Rais nchini humo au limeshaondolewa kutokana na visasi,chuki, vilivyotawala nchini humo baina ya viongozi wa sasa na waliomaliza muda wao ambao waliokabidhiwa madaraka kwa njia ya amani na Rais Mstaafu Joseph Kabila ambaye alihukumiwa adhabu ya kifo huku watuhumiwa wa mauaji ya Rais Laurent Kabila wakiachiwa huru kwa nia ya kuukomesha utawala uliopita.

Ni wakati sasa kwa Viongozi wa sasa na wale waliomaliza muda wao kuondoa tofauti zao na kufanya maridhiano ya kitaifa ili kuijenga nchi hiyo na kuwaunganisha wakongomani kuwa wamoja na kutetea nchi yao badala ya kuendeleza visasi na chuki na kutoa mwanya kwa mataifa ya nje kuingia na kuvuna mali za nchi hiyo kwa kisingizo cha kuleta amani huku wakiendeleza migawanyiko kwa wananchi wa nchi hiyo bila wao kujielewa.




Discussion about this post