NA MFAUME PASTORY,NJOMBE
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Njombe umefanikiwa kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo ambayo sasa imetoa matokeo chanya na yenye uwezo wa kuishi kwa miaka mingi mara baada ya utekelezaji wake kukamilika.
Miradi hiyo imebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anton Mtaka aliyoifanya Desemba 3,2025 katika vijiji vya Igomba Kata ya Saja wilayani Wanging’ombe na Kata ya Lyamkena iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe
Ziara hiyo ilikuwa ni ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo amekagua mradi wa nyumba ya watumishi Igomba iliyojengwa na TASAF na michango ya jamii, Jengo la Zahanati Igomba lililojengwa na TASAF pamoja na michango ya jamii, Zahanati katika Halmashauri ya Mji wa Makambo iliyojengwa na TASAF pamoja mradi wa kiuchumi wa upandaji miche ya parachichi kwa kaya masikini ili kuwainua kiuchumi unaotekelezwa katika Kata ya Lyamkena Halmashauri ya Mji wa Makambako.
Hata hivyo kujengwa kwa miradi hiyo vijijini kunaonesha ni jinsi gani Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haitekelezi miradi ya maendeleo mijini pekee bali hata vijijini kazi zinaendelea.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo,Mtaka amesema kwa miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na matokeo chanya kwenye maisha ya wananchi wa kawaida hasa wa vijijini.
Amesema fedha zote ambazo zimetekeleza miradi hiyo zimekwenda moja kwa moja kwa wananchi ambapo wamefanufaika na uwepo wa miradi hiyo ya Serikali ikiwemo kuuza vifaa vya ujenzi, kuanzisha shughuli za kiuchumi kupitia nishati ya umeme,ikiwemo kupata fursa ya kuuza bidhaa kwa wahudumu na wateja wanaofika kupata huduma katika miradi hiyo.
“Hii ndio ‘’Samia Impacts’’ na ni muhimu kwa wananchi kuitunza na kuindeleleza miradi hii, na kuwapenda na kushirikiana na wahudumu watakaoletwa katika Zahanati hii lakini pia muwe na uwezo wa kutambua fursa ambazo zinaweza kutokana na miradi hiyo ambayo Rais Samia ameitekeleza”amesema Mtaka
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Zakaria Mwansasu amebainisha kuwa kiasi cha Sh. Bilioni 184 zilitumika kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Zahanati na Nyumba ya watumishi ambayo inawezesha kuishi watumishi wawili na familia zao.
Amesema wananchi wamechangia kiasi cha zaidi ya Sh.Milioni 15 na mpaka sasa watumishi wawili wamekwisha andaliwa kwenda kuhudumia katika Zahanati hiyo.
Mwansasu ameongeza kuwa kwa sasa wanamikakati ya upatikanaji wa dawa,na kuandaa kichomea taka ambapo hadi kukamilika kwa mradi huo utaweza kuhuhudumia kaya zaidi ya 369.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha hizi.”amesema Mwansasu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Keneth Haule amemhakikishia Mkuu wa Mkoa huo kuwa kutokana na manufaa ya miradi hiyo, kama Halmashauri inajielekeza katika kuandaa bajeti itakayoziwezesha kaya hizo kupata viuatilifu ili kuanza kutibu miti yao ya matunda ya parachichi.
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Njombe Elia Kasanga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi hiyo ambao sasa umeleta matokeo makubwa.

Akizungumzia Mradi wa upandaji wa miche ya tunda la parachichi ,Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji wa Makambako Neema Chaula amesema mpaka sasa wamehudumia kaya 64 zimepata miche kumi na wakapanda katika kaya zao ili iwainue kiuchumi.
Neema amesema mpaka kufikia mwaka 2026 walengwa wote wataanza kupata matunda kwani lengo ni kuboresha kipato chao na wataweza kujitegemeza kwa kuboresha maisha yao pamoja na lishe katika familia zao.
“Mpaka sasa tayari baadhi ya wanufaika wamekwisha anza kunufaika”ameongeza Chaula

Kwa upande wake mkazi wa Kata ya Lyamkena Halmashauri ya Mji wa Makambako Evelina Nyali amesema alikuwa akiishi kwenye nyumba ambayo haistahili binadamu kuishi lakini sasa amefanikiwa kujikwamua na umasikini kwa kuanza kuuza parachichi pamoja na kufuga ng’ombe
“Sasa najitegemea na malengo ya ndoto yangu ya kuwa na maisha bora inakwenda kutimia”amefafanuwa Nyali




Discussion about this post