NA MWANDISHI WETU
BALOZI wa Palestina anayeiwakilisha nchi yake nchini Tanzania, Salim Siam amefanya ziara katika Ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) na kuweka wazi kwamba sasa wamefungua rasmi milango ya ushirikiano na Klabu hiyo kongwe nchini na waandishi wa habari kwa ujumla.
Akiwa katika ziara hiyo Balozi Siam amehimiza wanahabari kuonesha mshikamano na Palestina, ili kupaza sauti ya pamoja kukemea mateso wanayofanyiwa raia wa Palestina na majeshi ya Israel.
Akizungumza Desemba 18,2025 jijini Dar es Salaam mara baada ya kukutana na viongozi wa DAR-PC Balozi Siam amesema Wapalestina wanahitaji nguvu ya pamoja katika kukemea maovu hasa mauaji yanayoendelea katika eneo la Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ambayo yamegharimu maisha ya watu wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto.
Amesema tangu kuanza kwa mashambulizi katika eneo hilo Oktoba 2023, tayari Wapalestina 70,663 wameuwa kufikia Desemba 15 mwaka huu, wakiwemo wanahabari 256 na kuharibu kabisa majengo, Barabara, vyanzo vya maji, vyanzo vya nishati, majengo ya hospitali, shule na vyuo.
“Taarifa mpya kutoka kwa Waandishi Wasio na Mipaka inaonesha kuwa kwa mwaka huu wa 2025 pekee kumekuwa na ongezeko la mauaji ya wanahabari kote duniani ambapo kati yao, 67 wameuawa ndani ya mwaka mmoja, na nusu yao wakiuawa ndani ya ardhi ya Palestina.
“Tangu Oktoba 2023 karibu waandishi 220 wa Palestina wameuawa na vikosi vya Israel, ambapo 65 kati ya hao wameuawa wakiwa katika kutekeleza wajibu wao.
“Tunatoa wito kwa wanahabari kutokaa kimya katika mauaji haya ya aina hii, tunawaomba ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha ukandamizaji huu unawekwa wazi na kujulikana kote duniani ili kukomesha hali hii,” amesema Balozi Siam.
Aidha amesisitiza kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wa upatikanaji taarifa kuhusu yanayoendelea nchini mwake wakati wote, kwa kuwa anaamini kukandamizwa kwa haki kwa eneo moja ni ukandamizwaji wa haki kwa eneo jingine na kwamba wakandamizaji hao wanapokaliwa kimya hujenga mazoea na kufanya ukandamizaji huo kuwa hali ya kawaida katika maisha ya kila siku.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Wanahabari wa Dar es Salaam (DAR-PC), Andrew Msechu amesema wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu hali ilivyo Palestina na kwamba wanaendelea kuunga mkono msimamo wa Serikali katika kutambua na kuunga mkono upatikanaji wa Dola huru ya Palestina.
Amesema wanahabari wamekuwa wakijionea na kuumizwa na madhila yanayowasibu watu wa Palestina na namna uonevu dhidi ya raia wasio na hatia ulivyokithiri na mara kadhaa wamekuwa wakiangalia namna wanavyoweza kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uonevu huo.
“Madhila yanayowakabili Wapalestina yanahusisha pia wanahabari, ambao ni sehemu ya jamii pana ya Wapalestina wanaoonewa”ameongeza Msechu
Kwa mujibu wa International Federation of Journalists (IFJ), taarifa zinaonesha kuwa kwa mwaka huu wa 2025 pekee, wanahabari 51 wameuawa wakiwa katika juhudi za kupata na kutoa taarifa zinazohusu yanayoendelea nchini mwao.
Msechu ameeleza kuwa idadi hiyo inatisha na wao kama sehemu ya jamii ya wanahabari wanasikitishwa na kufadhaishwa sana na hayo yanayoendelea.
“Wanahabari wetu wamekuwa wakijitahidi kufanya kwa uwezo wao, japo si kwa uzito unaotakiwa kutokana na sababu kadhaa japo tumeendelea na kuungana wananchi wa Palestina na jumuiya ya kimataifa kupambana kuhakikisha kunakuwa na Palestina Huru na kwa kutumia kalamu zetu tutahakikisha tunashiriki katika kufanikisha hili,” amesema Msechu
Amebainisha kuwa tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kadhaa ni kuhusu kupata usahihi wa taarifa na imekuwa si rahisi kuifikia vyanzo sahihi kwa ajili ya kupata taarifa ambazo zinatakiwa kutoka ndani na hivyo kulazimika kudandia taarifa kutoka vyanzo vya kimataifa.


Discussion about this post