NA MFAUME PASTORY,NJOMBE
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amewahi kusema kuwa Maji ni kama damu ya Maisha ya dunia, kwani hutumika kuanzia katika suala la afya na lishe, hadi elimu na miundombinu.
Maji yanatajwa kuwa ni rasilimali ya kwanza duniani kutumika ikifuatiwa na mchanga ambapo maji yanatajwa kuwa ni muhimu katika kila nyanja ya mwanadamu kuishi na ustawi wake lakini pia yanachangia pakubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kushamiri kwa kila taifa.
Hata hivyo UN inasema kuwa watu wanaoishi mijini wanatarajiwa kuwa kwenye mgogoro wa kukosa maji na utaongezeka mara mbili kutoka watu milioni 930 mwaka 2016 hadi kufikia watu kati ya bilioni 1.7 na bilioni 2.4 mwaka 2050.”
Kauli ya UN kwa mataifa mbalimbali duniani imelenga kuhimiza kuchukuliwa kwa hatua madhubuti ili kuilinda dunia dhidi ya migogoro inayosababishwa na uhaba mkubwa wa maji ambao wakati mwingine husababishwa na Vita,Ukame wa muda mrefu,uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Katika miji na majiji mengi duniani bado upatikanaji wa maji safi na salama ni changamato kubwa ikiwemo upotevu wa rasilimali hiyo inayopotelea njiani kutokana na uchakavu wa mabomba ya kusafirishia.
Kutokana na hali hiyo,Serikali ya Tanzania ikiongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa watanzania waishio mijini na vijijini wanapata maji safi na salama kwa kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya maji.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuwa na taifa lenye uhakika na usalama wa maji kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kudumisha na kuendeleza ekolojia pamoja na kuwa na taifa lenye mfumo imara na shirikishi wa usimamizi wa ardhi oevu na rasilimali nyinginezo.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ikiwa na kauli mbiu “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” ambapo katika ahadi na Maelekezo yake (2025 – 2030) imefafanuwa kuwa Serikali ya CCM itaimarisha upatikanaji wa Maji kwa Wananchi wote.
“CCM inatambua umuhimu wa maji katika maisha ya kila siku ya wananchi, matumizi ya viwandani pamoja na kuimarisha hali ya usafi wa mazingira.
“ Aidha, CCM inatambua kazi kubwa ambayo Serikali imefanya katika miaka mitano iliyopita katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, hususan vijijini.
“Ili kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote, katika miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM itachukua hatua zifuatazo,ikiwemo kuimarisha ulinzi na uendelezaji wa vyanzo na rasilimali za maji;kuongeza idadi ya kaya vijijini na mijini zilizofikiwa na huduma ya maji safi na salama kwa asilimia isiyopupungua 90″inaeleleza Ilani hiyo
CCM kupitia Ilani yake imeeleza kuwa,Serikali yake itajenga miradi ya maji na mitambo ya kutibu maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu ili kuimarisha usalama wa maji;
“Kuanzisha na kutekeleza Gridi ya Taifa ya Maji itakayotumia vyanzo vikubwa vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, uchumi na mazingira, ikiwamo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, na Ziwa Nyasa.
“Katika miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM itajenga mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida.
“Mradi hpokpouu utakuwa na mabomba mawili, bomba moja la maji ya kunywa na bomba jingine kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na mifugo na kuimarisha mifumo ya uondoaji wa majitaka nchini ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 13 hadi angalau asilimia 40″inabainisha Ilani hiyo

Hata hivyo CCM kupitia Serikali yake itaongeza kasi ya uvunaji wa maji ya mvua kwa kujenga mabwawa ya ukubwa wa kati na mabwawa ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kilimo, mifugo na uvuvi ikiwemo kukamilisha ujenzi wa mabwawa ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Bwawa la Kidunda na Farkwa ili kuongeza usalama wa maji nchini
Kutokana na umuhimu huo,Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Njombe waliamua kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa katika eneo hilo na Serikali ili kujionea ujenzi wa miundombinu na vyanzo vipya vya maji wakiwa na lengo la kuangalia jinsi utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kuhusu upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
Viongozi hao wa CCM wametembelea Miradi ya Maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Njombe (NJUWASA) ili kutatua adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Ziara ya viongozi hao walioifanyika November 7, 2025 ikihusisha viongozi mbalimbali wakiongozwa na Katibu wa Itikadi,Mafunzo, Siasa na Uenezi wa chama hicho Solanus Mhagama na Diwani Mteule wa Kata ya Njombe Mjini Deo Mazao ambapo wametembelea vyanzo vitatu vya maji vya Ijunilo,Lugenge ambacho kimefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na chanzo cha maji cha Mto Hagafilo ambacho kimefikia asilimia 46 ya ujenzi wake.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Njombe (NJUWASA) Mhandisi Robert Lupoja anasema miradi hiyo inatekelezwa na mkandarasi Nandra Engineering ambayo inagharimu zaidi ya Sh.Trilioni moja kwa ajili ya Mkoa wote wa Njombe.
Mhandisi Lupoja anasema uzalishaji wa maji kwa sasa ni chini ya lita 1,000,000 kwa siku kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji ya wananchi lakini mradi wa Lugenge unatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Novemba na utaanza kutoa huduma ya maji.
Ameutaja mradi wa miji 28 unaogharimu kiasi cha Sh.Bilioni 41 wenye chanzo chake kutoka Mto Hagafili ambao unatarajiwa kukamilika kati kati ya mwaka 2026, utaongeza maji zaidi ya lita Milioni 11 kwa siku na utahudumia wananchi wote wa mji wa Njombe na kuondoa mgao wa maji safi na salama.
Aidha Mhandisi Lupoja anatoa wito kwa wananchi kuvumilia changamoto waliyonayo kwa sasa kuhusu maji kwa kuwa changamoto hiyo ni ya muda mfupi.

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi,Mafunzo, Siasa na Uenezi wa chama hicho Kata ya Njombe Mjini Solanus Mhagama anailezea ziara hiyo kuwa yenye manufaa makubwa kwa viongozi hao na serikali kwa sababu sasa wanakwenda kuwaeleza wananchi juu ya mafanikio makubwa na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa kuhusu upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Njombe baada ya kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mhagama anampongeza Mhandisi Lupoja kwa ushirikiano mkubwa aliyoutoa kwa viongozi hao akifahamu kuwa wanajukumu kubwa la kuelimisha umma juu ya miradi hiyo muhimu inayotekelezwa na Serikali yao ya awamu ya sita iliyo chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Diwani Mteule wa Kata ya Njombe Mjini Deo Mazao anakiri juu ya uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wake na ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kwenda kuwaeleza wananchi juu ya hatua kubwa zilizopigwa na serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Naye Mkazi wa Njombe Chuma Mbawala amebainisha kuwa upatinakaji wa maji safi na salama ni jambo la lazima kwa afya ya mwanadamu kwa kuwa rasilimali hiyo inatumika zaidi ya zingine.
“Tunaamini kukamilika kwa miradi hii itatusaidia sisi wananchi kwa kuwa eneo hili ni la milima hivyo hata uchimbaji wa visima ni mgumu tofauti na miji mingine ambapo watu wanaweza kuchimba visima bila kutumia mashine na wakapata maji kwa matumizi yao”ameongeza Mbawala





Discussion about this post