NA MWANDISHI WETU,DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, katika Ikulu ya Chamwino,jijini Dodoma na kujadili maeneo muhimu ya ushirikiano.
Mbali na ushirikiano lakini pia Tanzania na Marekani zitaimarisha dhamira ya pamoja ya kujenga ushirikiano wa kisasa na wenye manufaa kwa pande zote mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika Desemba 8,2025 pia yamejikita katika hatua za majadiliano ya miradi mikubwa inayoongozwa na kampuni za Marekani nchini ambapo pande zote mbili zimekubaliana kuwa majadiliano ya miradi miwili ya kimkakati ukiwemo Mradi wa LNG na Mradi wa Tembo Nickel yamefikia hatua za mwisho kabla ya kutiwa saini rasmi.
Mbali na miradi hiyo lakini pia uwekezaji katika Mradi wa Mahenge Graphite, unaendelea kufanyiwa uchambuzi wa kiufundi.
Marekani na Tanzania pia wamegusia maeneo mapana ya ushirikiano ikiwemo utulivu wa kisiasa, usalama wa kikanda, mageuzi ya kiuchumi, ukuaji wa sekta binafsi, ushirikiano katika afya na programu za kubadilishana uzoefu kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.
Akizungumza katika mkutano huo,Rais Samia Suluhu Hassan ameukaribisha upya msimamo wa Marekani na kuhakikishia ujumbe huo kuwa Tanzania itaendelea kusimamia hatua zote zilizobaki ili kukamilisha taratibu na kufungua njia ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Kama Taifa lisilofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi, tayari na imejitoa kufanya kazi na washirika wote wanaoheshimu uhuru wetu na kushiriki katika dira yetu ya maendeleo.
“Miradi hii ni ya umuhimu mkubwa kwa Taifa, na tumejidhatiti kuikamilisha ili iweze kufungua ajira, uwekezaji, na ustawi endelevu kwa wananchi wetu.”
Rais Samia pia ameongeza kuwa zaidi ya kampuni 400 za Marekani kwa sasa zinafanya shughuli zao nchini Tanzania nah ii ni kiashiria cha uthabiti wa nchi”amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake Balozi Lentz ambaye amefuatana na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Uchumi kutoka ubalozi huo nchini,amesisitiza dhamira ya Washington ya kuhuisha mahusiano na kuongeza kina la ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya mataifa haya mawili.
“Marekani imejitolea kujenga ushirikiano usiotegemea misaada, bali unaojengwa juu ya ustawi wa pamoja,” amesema Balozi Lentz.
Balozi Lentz pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na mipango madhubuti ya muda mrefu kupitia Vision 2050, na kusisitiza kuwa Serikali ya Marekani iko tayari kuunga mkono utekelezaji wake pamoja na kuimarisha falsafa ya 4R ya Rais ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya imani katika utawala.
Pande zote zimekubaliana kuwa mawasiliano ya karibu, ushirikiano wa mara kwa mara, na hatua za haraka katika kukamilisha makubaliano yaliyosalia ni muhimu katika kufungua uwezo kamili wa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.
Mkutano huo umewakilisha hatua muhimu katika kufafanua upya na kuhuisha mahusiano kati ya Tanzania na Marekani ambapo dhamira ya pamoja iliyothibitishwa na serikali zote mbili inaashiria mwanzo wa ushirikiano wa kisasa, uwazi, unaoongozwa na sekta binafsi ukijengwa juu ya ustawi wa pamoja wa kuheshimiana na ushirikiano wa muda mrefu wa kimkakati.
Miradi hiyo mikuu ya kimkakati ni pamoja na Mradi wa LNG wenye thamani inayokadiriwa kuwa Dola za kimarekani Bilioni 42 ambapo ni mradi mkubwa wa kugundua na kuchakata gesi asilia unaohusisha kampuni kubwa za kimataifa za nishati.
Mradi huo unalenga kufungua hazina kubwa ya gesi iliyopo baharini, kuongeza mapato ya taifa, kuunda maelfu ya ajira na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama mchezaji muhimu wa LNG.
Mradi wa pili ni wa Tembo Nickel wenye thamani ya Dola za kimarekani Milioni 942 ambapo uwekezaji mkubwa wa madini muhimu katika eneo la Ngara unaolenga nikeli ni kiungo muhimu katika utengenezaji wa betri za magari yanayotumia umeme.
Mradi huo utaimarisha minyororo ya kimataifa ya nishati safi, kuchochea viwanda na kuongeza pato la mauzo ya nje.
Mradi wa tatu ambao ni Mahenge Graphite wenye thamani ya Dola za kimarekani Milioni 300 ni chanzo kikubwa duniani cha madini ya graphite yenye ubora wa juu ambayo yana umuhimu katika uzalishaji wa betri na teknolojia za nishati jadidifu.
Mradi huu utaimarisha nafasi ya Tanzania kama mtoa huduma mkuu wa malighafi muhimu za viwanda vya kisasa vya betri.




Discussion about this post