NA GOODLUCK HONGO
HAIJAWAHI kutokea katika historia ya zao la Kahawa Tanzania kwa kilo moja kufikisha Dola tano ya Kimarekani katika msimu wa 2024/2025 kutoka dola mbili katika miaka iliyopita huku ubora wa zao hilo ukishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani .
Hata hivyo mafanikio hayo si kazi ndogo kuyafikia hasa ukizingatia zao hilo halilimwi Tanzania pekee bali hata nje ya Tanzania hivyo kulikuwa na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia uongozi thabiti na wenye uzalendo wa kweli kwa Taifa lao wa Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB)
Bodi ya Kahawa yaTanzania (TCB) ni chombo cha Serikali kilichoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 3 Sheria ya Tasnia ya Kahawa Na. 23 ya mwaka 2001. Majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Sehemu ya 5 ya Sheria ya Tasnia ya Kahawa ya mwaka 2001 Na. 23, kama ilivyorekebishwa na Sheria yaMarekebisho ya Sheria za Mazao Na. 20 ya mwaka 2009, ni kutekeleza majukumu ya udhibiti na kutoa ushauri kwa Serikali katika masuala yote yanayohusiana na maendeleo ya sekta ya kahawa. Kama mdhibiti, jukumu kuu la TCB ni kuhakikisha kwamba Tasnia ya Kahawa inafanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya Tasnia yaKahawa na kanuni zake, na kulingana na sera na viwango vingine vya udhibiti vya kitaifa na kimataifa.
TCB ilipitia mageuzi makubwa matatu (3) tangu mwaka 1976 wakati ilipoanzishwa kwanza kama Mamlaka ya Kahawa ya Tanzania (CAT). CAT ilikuwa na jukumu la mafunzo, usimamizi wa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo za kahawa, na upanuzi wa eneo la uzalishaji wa kahawa.
CAT ilitekeleza majukumu yake kwa mafanikio chini ya miradi miwili kuu, Mpango wa Kuboresha Kahawa (CIP) na Mpango wa Maendeleo ya Kahawa (CDP), ambayo ilitiwa nguvu na Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya (EEC).
Mageuzi ya pili yalitokea mwaka 1984 wakati CAT ilipobadilishwa kuwa Bodi ya Masoko ya Kahawa ya Tanzania (TCMB). TCBM ilikuwa na jukumu la udhibiti kama ilivyofanywa na CAT na jukumu la kuchochea masoko ya kahawa.
Mabadiliko hayo yalikuwa muhimu kwani CAT hakuwa na uwezo wa kifedha kuendelea kufadhili miradi ya CIP na CDP, ambayo ilimalizika mwaka 1984 ambapo lengo lilikuwa kurejesha tena vyama vya ushirika nchini Tanzania.
Mageuzi ya tatu yalitokea mwaka 1993 wakati TCMB ilipobadilishwa kuwa Bodi ya Kahawa ya Tanzania (TCB) kujibu sera za uhuru wa biashara na kuanzishwa kwa uchumi huria katika miaka ya 1990.
Kama matokeo, TCMB iliondolewa kutoka kwa majukumu yote yanayohusiana na biashara ambapo kutungwa kwa Sheria ya Viwanda vya Kahawa Na. 23 ya mwaka 2001 ilizuia TCB kufanya majukumu ya kibiashara, ikiiwekea majukumu ya sera, udhibiti, na uratibu tu.
Mwaka 2009, marekebisho ya Sheria ya Viwanda vya Kahawa Na. 23 ya mwaka 2001 yalifuatia kutungwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mazao Na. 20 ya mwaka 2009, ambayo ilirekebisha muundo wa ufadhili na majukumu ya Bodi za Mazao.
Shughuli za TCB zimeainishwa kihalali kuwa ni pamoja na majukumu ya udhibiti na uratibu wa majukumu shirikishi, ambapo majukumu shirikishi ya TCB hutekelezwa kama majukumu ya pamoja na wadau wengine.
Majukumu haya yanajumuisha utafiti, ugani, usambazaji wa pembejeo, maendeleo ya kahawa na kuhamasisha vyama au taasisii nyingine zinazohusiana na au kushughulika na tasnia ya kahawa, kuhamasisha biashara na ushindani wa haki, kutoa huduma za ushauri wa kiufundi kwa wakulima wa kahawa, wazalishaji, watengenezaji wa vinywaji vya kahawa, wafanyabiashara, na wafanyabiashara wa nje.
Kufuatana na Sehemu ya 5 (1) hadi (6) ya Sheria ya Tasnia ya Kahawa Na. 23 ya mwaka 2001 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mazao Na. 20 ya mwaka 2009, TCB ina majukumu na nguvu zifuatazo za kutoa ushauri kwa Serikali juu ya sera na mikakati ya maendeleo ya tasnia ya kahawa.
Mbali na hilo lakini pia TCB inajukumu la
kudhibiti na kusimamia ubora wa kahawa na bidhaa zinazotokana na kahawa.
TCB pia ina jukumu la kukuza na kulinda maslahi ya wakulima dhidi ya vyama vya wanunuzi vinavyoweza kuundwa kupitia vyama ikiwemo kuwakilisha tasnia katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa kuhusu masuala yanayohusiana na tasnia ya kahawa.
Hata hivyo TCB hutoa leseni au vibali vya kuuza nje ya kahawa pamoja na kusajili wafanyabiashara mbalimbali wa kahawa.
Hata hivyo Dira ya TCB ni kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti wa Kahawa Barani Afrika.ikiwa na dhamira ya kutengeneza mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa ajili ya maendeleo ya tasnia ya kahawa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan mara kwa mara amekuwa akitoa sifa za ufanisi wa viongozi mbalimbali anaowateua hata katika Tume ,mbalimbali za kuchunguza matukio kwa kujivunia utendaji wao kazi badala ya kuwachukua wataalam wengine kutoka nje ya nchi ili hali watanzania wenyewe wanaweza.
TCB inayoongozwa na Mwenyekiti wake Prof.Aurelia Kamuzora ambaye kiasili ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ambao moja ya utamaduni wao ni kumkarimu mgeni anayewatembelea nyumbani kwa kumpatia Kahawa iliyokaangwa ili aitafune wakati wa maongezi.
Tangu kuteuliwa kwa Prof,Kamuzora kuiongoza taasisi hiyo,TCB imekuwa na mafanikio makubwa huku msimamo wake ukiwa ni Tanzania kwanza wengine ndio wafuate.
Katika msimu wa 2024/25 zao hilo la kimkakati liibuka ghafla na kuwa kusababisha miche yake kutafutwa kwa udi na uvumba baada ya kilo moja ya Kahawa kufikia dola tano za kimarekani ambayo ni sawa na zaidi ya Sh.10,000 ya Kitanzania ambayo inajukana kama bei ya Rais Samia.

Awali akizungumzia hali hiyo,Mkurugenzi wa Kampuni ya Karagwe Estate Limted iliyopo wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera Respicius Kamanzi ambaye Kampuni yake inajihusisha na ununuzi wa Kahawa anasema wao hununua Kahawa katika vyama mbalimbali vya wakulima wa Kahawa kwa njia ya mnada
Anasema wanapofika huwakuta wakulima wakiwa wamepeleka Kahawa yao mnadani kupitia katika vyama vyao na anayeshinda ndio huchukua mzigo.
Anasema wanapoinunua Kahawa hiyo iwe Arabica au Robusta na kisha huzisafirisha hadi kiwandani kwao
“Tukishaipeleka ile Kahawa kiwandani tunaikoboa na kisha kuiweka katika viwango vinavyotakiwa ikiwemo madaraja tofauti ambayo ni manne zikiwa na unene tofauti ikiwemo kubwa,kubwa zaidi hadi ya mwisho”
“Lakini hatuishii hapo ila kuna nyingine ambayo inashuka chini zaidi ambapo kabla ya kuiweka katika magunia tunaipitisha katika mashine ili kuisafisha zaidi ikiwemo kuondoa weusi pamoja na takataka”
“Baada ya kumaliza hapo tunaweka katika gunia kisha tunapima,tunashona tayari kwa kusafirisha”anasema Kamanzi

Akizungumzia suala la kuuza,Kamanzi anasema wateja wako wengi kutoka sehemu mbalimbali ambapo huingia nao mikataba kulingana na mahitaji wanayotaka wateja na muda wanaohitaji kupata
“Kwa mfano mwengine anaweza kukwambia anahitaji Kahawa mwezi wa saba,mwingine wa nane,mwingine wa 10 iwe tayari basi mnasaini mkataba kadiri ya mahitaji yake.
“Mwingine anakuja anahitaji tani 1,000, walio wengi hasa wanunuzi wakubwa na wengi ni wanunuzi wa nje na hasa huchukua grade one”anasema Kamanzi
Aidha Kamanzi anasema Kahawa ina faida nyingi ikiwemo kuondoa Kansa,kuchangamsha mwili na mengine
Akizungumzia kuhusu bei ya soko,Kamanzi anasema bei hupanda na kushuka hadi wakati mwingine hutia hasara ambapo hufikia hadi dola mbili za kimarekani kulingana na soko.
“Msimu huu tunaokwenda kumalizia Kahawa iko juu sana na haijawahi kuwepo na ni bei kubwa ya kutisha sana,Kahawa ilifika dola tano za kimarekani na point ina ilionekana kupanda zaidi hadi dola 5.7,na ilipanda sana msimu wa 2024/25 ambapo kila mtu alikuwa akishangaa kwanikipindi cha nyuma Kahawa ilikuwa inashuka kiasi kwamba hata mkulima anakata tamaa hadi alikuwa hawezi kupalilia na haoni sababu ya kupanda Kahawa,lakini msimu huu miche ilikuwa ya kugombania,bei ilifanya wakulima kwamba nilikuwa na hekari mbili kumbe nilitakiwa kuwa na hekari nne.
“Gunia mbili mkulima anapata milioni wakati zamani milioni ilikuwa ni shamba zima na katika eneo la Karagwe na Kyerwa ndio wakulima wakubwa wa Kahawa ambapo mtu kupata tani 40 au 50ni kitu cha kawaida,sasa niambie kwa bei hii mtu ana tani 50 sasa ukienda kijijni huo sasa hivi wanaita bei ya Rais Samia”
“Haijawahi kutokea imevunja rekodi kwa gunia mbili kupata Sh.Milioni moja sio kitu cha kawaida na kama nilivyosema wakulima wa kule kupata tani 50 ni kitu cha kawaida sasa kwa bei hiyo inakuwaje”amebainisha Kamanzi

Akizungumzia kuhusu mikutano inayoandaliwa na TCB,Kamanzi anabainisha kuwa mfumo huo ni mzuri kwa kuwa unasaidia kujua masoko na kukutana na wadau mbalimbali.
Wakati wakulima wakifurahia bei ya Samia,mafaniko mengine ya TCB ni kuifanya Kahawa inayozalishwa Tanzania kuibuka na kupata nafasi ya kwanza kwenye maonyesho ya 22 ya Chama cha Kahawa Nzuri za Afrika (AFCA) 2026, na ya nne duniani kwa kuzalisha kahawa iliyothibitishwa ubora wa juu na endelevu kwa mazingira.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali ya Awamu ta Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuimarisha na kuliongezea thamani zao la Kahawa kama moja ya mazao ya kimkakati ambapo wakulima wamekuwa wakipata pembejeo kwa wakati na kutatua matatizo yao ili waweze kuzalisha kwa ubora na viwango vya kimataifa.
Hata hivyo Umoja wa Afrika tayari umelifanya zao la Kahawa kuwa moja ya zao la kimkakati ambapo kwa Tanzania linalimwa katika mikoa 17 ikiwemo Kagera na Kilimanjaro.
Katika Ripoti ya Soko la Kahawa la Kimataifa (ICE), iliyowasilishwa na mtaalamu wa masoko duniani,Judith Garnes,aliyoiwasilisha katika Mkutano wa Kahawa uliofanyika kuanzia Februari 4 hadi 6, 2026. jijini Addis Ababa, Mji Mkuu wa Ethiopia anasema kuwa Kahawa inayozalishwa Tanzania inachukua nafasi ya kwanza barani Afrika na ya nne duniani kwa ubora ambao hauhusiani na uharibifu wa mazingira.
Hali hiyo inaonesha juhudi zilizowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa kila mkulima anazalisha Kahawa bora kuanzia kupanda hadi kuvuna.

Awali February 26,2025 TCB iliandaa Mkutano wa Kimataifa wa Kahawa uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Prof.Aurelia Kamuzora anasema yeye amekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwa miaka mitatu na wamefanya mabadiliko makubwa sana ikiwemo kuleta mkutano hupo Tanzania na wameweza kuufanikisha vizuri
Anasema anamshukuru sana Rais Dkt.Samia kwa kumpa uteuzi wa mara ya pili na naendelea kuifanya hii kazi kwa kuipenda kwani najua inainua wananchi hasa wale wakulima ambao ndio watanzania walio wengi
Anasema wanaendelea kuandaa soko ili kuwepo na wanywaji wengi wa Kahawa kwa kuwa kuinywa ni utamaduni na wanahitaji kubadilisha utamaduni wa aina Fulani.
“Lazima wananchi wajue ukinywa Kahawa kuna faida fulani na unaona wazungu wanaishi muda mrefu kwa kuwa Kahawa na ukianza kunywa Kahawa ndipo hapo sasa viwanda vyetu vitaanzishwa kwa kuwa soko tayari limeshatengenezwa na vingine vipo tayari na hilo ni kwa Tanzania lakini tukitaka kukamata soko la Afrika lazima tuhimize unywaji,tunatengeneza miundombinu ikiwemo mawasiliano mazuri ndani ya Afrika ndio soko la Kahawa litaendelea kukua.
“Tuhahitaji hatua za kutupeleka kuuza pamoja na kutengeneza viwanda na kuuza Kahawa yetu huku Afrika ambapo ni kitu ambacho hakiwezi kuota leo lakini tunashukuru Azimio la Dar es Salaam ambalo tunaanza hatua mbalimbali ambazo zitatupeleka huko”
“Mzungu akiingia ofisini lazima anywe kikombe cha Kahawa na ndio maana inauzwa huko, Je sisi mtu hajaingia ofisini anaanza kunywa Kahawa?Sisi kwa kutengeneza utamaduni tunaamini watu watakunywa Kahawa”amesema Prof.Kamuzora
Faida nyingine ya Kahawa inatajwa kuwa ni kupunguza uzito,kuamsha ubongo ambayo inafanya binadamu kuendelea kufikiri vizuri zaidi.
Kahawa pia inaelezwa kupambana na chembechembe hatarishi mwilini zinazoweza kusababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kulinda seli za mwili,kusaidaia pia kupunguza hatari ya magonjwa sugu.

Hata hivyo Kahawa inaelezwa kuwa pale inaponywewa kwa kiasi kinachofaa husaidia kuongeza umakini,kuboresha kazi za ubongo,kuboresha afya ya moyo na kulinda mwili dhidi ya uharibifu wa seli.
Kwa Tanzania zao la Kahawa lilianzia mkoani Kilimanjaro baada ya kuletwa na wakoloni ambapo pia walipiga marufu watu kuinywa ili iweze kusafirishwa nchini kwao kutokana na umuhimu wake kwa afya ya binadamu.

Discussion about this post