NA TBN, ARUSHA.
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Anda Filip amesema kupitia Dira ya Maendeleo 2050, Tanzania ina fursa ya kuimarisha ushiriki wa wanawake na vijana katika kujenga na kutekeleza ajenda za maendeleo ya muda mrefu.
Amesema kuimarisha ushiriki wa wanawake na vijana kutahakikisha vipaumbele vya taifa vinaendelea kutekelezwa na vizazi vijavyo bila kutegemea mabadiliko ya awamu za uongozi.
Mbali na hilo lakini pia uzoefu wa Tanzania unaweza kuwa somo kwa mataifa mengine katika kujenga mifumo jumuishi ya kufanya maamuzi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Oktoba 7, 2026 wakati wa Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika jijini Arusha, Filip ameipongeza Tanzania kwa hatua iliyopiga katika kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Amesema amevutiwa na namna Tanzania ilivyoongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 39.
Aidha amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa na maamuzi ya kitaifa.

Katika mkutano wa IPU unaendelea jijini Arusha, Tanzania inawakilishwa na Wabunge nane ambapo kati ya hao, Wabunge wanne ni wanawake ikiwa ni sawa na asilimia 62.5 ya uwakilishi wa wanawake wanaoiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Wabunge hao wanawake ni Dkt. Pindi Chana, Dkt. Zeyana Hamid,Kiza Myeye, Mhandisi Fatma Rembo na Asha Feruzi.
Wabunge wengine waliopo IPU ambao ni wanaume ni Dkt. Damas Ndumbaro,Elibariki Kingu na Rashid Shangazi, ambao idadi yao ni sawa na asilimia 37.2 ya uwakilishi wa wabunge wa Tanzania.

Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani ulianza tarehe 5 Oktoba, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) na unatarajia kuhitimishwa Ijumaa Oktoba 9, 2026.
Mkutano huu umeshirikisha wajumbe zaidi ya 2000 kutoka mataifa mbalimbali.



Discussion about this post