WASHINGTON DC,MAREKANI
WAKATI Dunia ikiadhimisha siku ya mazingira duniani leo,baiskeli imetajwa kuwa ni chombo kinachohifadhi mazingira kwa kupunguza utoaji wa hewa ukaa.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya uendeshaji wa baiskeli duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Juni 3, ya kila mwaka
Amesema uendeshaji baiskeli siyo tu unahifadhi mazingira kwa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi za kwenye magari bali pia unapunguza gharama kwa mtumiaji na kujenga afya.
“Baiskeli ni uhuru, baiskeli inafurahisha, ni nzuri kwa afya ya mtu,kimwili na kiakili na ni nzuri kwa sayari yetu pekee ya dunia.”amesema Guterres.
Amesema baiskeli ni maarufu kwa uwezo wake wa kumpatia mtu mazoezi na usafirishaji na siyo tu kwenda shuleni, madukani na kazini lakini pia kwa uendelevu wa mustakabali wa dunia.
Amefafanua kuwa siku ya uendeshaji baiskeli duniani inatoa fursa ya kuangazia umuhimu wa usafiri huo usiotumia nishati ya mafuta au umeme na nafasi yake katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na wakati huo huo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Guterres ameongeza kuwa matumizi ya baiskeli yanakwenda kizazi hadi kizazi na pindi mtu anapokuwa amejifunza katu hatosahau hivyo ni muhimu kuendelea kuitumia baiskeli.
“Hata kabla ya janga la ugonjwa wa corona(COVID-19), uendeshaji baiskeli ulikuwa moja ya njia muhimu za usafiri na mipango ya kupeana baiskeli ili kuendesha inazidi kuongezeka na hivyo kutoa fursa nafuu zaidi ya kutumia baiskeli wa safari fupi,” amesema Guterres.
Ameongeza kuwa janga la Corona limebadilisha mahitaji ya usafiri na tabia za binadamu na kuchochea miji kufikiria upya mifumo yao ya usafiri huku baiskeli zikiwa na dhima muhimu zaidi za usafiri nafuu na usiochafua mazingira.
“Ni kwa mantiki hiyo anasema mabadiliko hayo yanatoa fursa zaidi ya kutumia baiskeli sambamba na kuimarisha usalama barabarani kwa watumiao usafiri huo ikiwemo kuwepo kwa eneo maalum la waendesha baiskeli”.
“Tunapojiandaa kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa usafiri endelevu utakaofanyika Beijing China mwezi Oktoba, hebu na tuahidi kusaidia ili usafiri wa baiskeli uwe bora na salama.”amesema Guterres
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hadi sasa kuna takribani baiskeli bilioni moja duniani kote ,idadi ambayo ni kama ya abiria wanaotumia usafiri wa magari.
UN
Discussion about this post