• About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact
Thursday, May 21, 2026
  • Login
Bajeti
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
Bajeti
No Result
View All Result
Home Sayansi na Teknolojia

Prof.Lilian Kaale,Mbunifu wa teknolojia ya kuthibiti sumukuvu katika maghala ya kuhifadhia mahindi

Asema ni tatizo kubwa linalopaswa kushughulikiwa haraka,aishukuru COSTECH kufadhili bunifu yake

by bajeti
May 21, 2026
in Sayansi na Teknolojia
0
Prof.Lilian Kaale,Mbunifu wa teknolojia ya kuthibiti sumukuvu katika maghala ya kuhifadhia mahindi

Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Chakula,Sayansi na Teknolojia Profesa Mshiriki Lilian Kaale aliyebuni mdumo wa kudhibiti sumukuvu katika maghala yanayohifadhi mahindi

Share on FacebookShare on Twitter

NA GOODLUCK HONGO

SUMUKUVU (Mycotoxin) ni sumu  inayozalishwa na wadudu wanaojulikana kama Kuvu(Fungi) ambao wanapatikana kiasili katika mazingira na kisha kuathiri mazao yanayopelekea binadamu na mifugo kuathirika kiafya.

Sumukuvu huathiri nafaka kama mahindi,karanga,mtama,ngano,uwele na ulezi,korosho na hata viungo vilivyokaushwa,mbegu za  mafuta kama alizeti na pamba na mazao yatokanayo na mifugo kama  maziwa na mayai

Ukuaji au utokeaji wa Kuvu wanaotoa sumu ya sumukuvu unaweza kutokea kabla au baada ya kuvuna nafaka hasa wakati wa kuhifadhi kwenye mazingira ya joto,unyevu na machafu ambapo sumu hiyo haiwezi kuondolewa kwa kupikwa au kusindikwa.

Hata hivyo kuna aina mbalimbali za sumukuvu ambazo zimegunduliwa ambapo zinazoonekana kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mifugo ni Aflatoxin ,Ochratoxin  A,Patulin,Fumonisins,Zearalenone, na Nivaleno

Binadamu na mifugo wanaweza kuathirika kiafya kutokana na kula chakula chenye sumukuvu au chakula kitokanacho na mifugo iliyolishwa chakula chenye sumukuvu

Moja ya madhara makubwa yanayosabishwa na sumukuvu ni pamoja na saratani ya figo,ini,tataizo la watoto kuzaliwa na mgongo wazi,kuharisha,kutapika,maumivu ya tumbo na kuonesha dalili za manjano katika sehemu za mwili kama viganja vya mikono,ulimi,macho na nyayo

Wakati sumukuvu ikiendelea kuonekana kama janga na kusababisha vifo vya binadamu,tafiti na bunifu za teknolojia za kuithibiti sumu hiyo zinaendelea kufanyika ambapo Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Lilian Kaale amebuni mfumo wa kuthibiti sumukuvu.

Prof.Kaale ambaye anatokea Idara ya Chakula,Sayansi na Teknolojia katika chuo hicho amebuni na kufanikiwa kutengeneza mfumo unaoweza kuwadhibiti Kuvu ambao ndio wanaotoa sumukuvu baada ya kuwepo kwa mazingira yanayowawezesha kutoa sumu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam,Prof. Kaale anasema yeye alianza utafiti wa kupambana na sumukuvu baada ya kuona athari za sumu hiyo kwa binadamu na wakati mwingine kusababisha vifo.

Anasema sumukuvu ni janga kubwa kwa Taifa kutokana na kwamba watu zaidi ya milioni 50 wanakula chakula kitokanacho na zao la mahindi  ambapo huko ndiko sumukuvu inapopatikana kwa wingi sana ambapo alianza  utafiti wake  tangu 2018 baada ya kupata fedha kidogo kutoka Shirika la UNESCO.

Anasema yeye aliandika dodoso katika mashindano ya dunia ya wanawake baada ya kutokea kwa vifo vya watu waliokula chakula chenye sumukuvu mkoani Dodoma na alikuwa ni mmoja kati ya wanawake 20 waliochaguliwa na hapo ndipo UNESCO walipomuona na kumfadhili katika awamu ya kwanza ya utafiti wake katika Wilaya za Kondoa na Chemba.

“Niliona ni tatizo kubwa Tanzania sio tu kwa uharibifu wa mazao lakini pia mazao ambayo tayari yameingiliwa na hii sumu yanasababisha matatizo makubwa sana kwa binadamu.

“Nilianza utafiti kidogo kwa ile hela niliyopewa na UNESCO kama Sh.Milioni 100 na baada ya hapo niliona ni kwa nini nisiendelee na awamu ya pili”anasema Prof.Kaale

Anasema alipokuwa anaendelea na awamu ya pili ndipo alipoandika barua kwenda kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo walikubali kumfadhili zaidi.

Anasema ubunifu huo ambao aliuita Online Ditaction of Alphatoxion in  Food   amejaribu kubuni mfumo wa kitaalam ili kuona namna gani inavyowezekana kuzuia au kugundua uharibifu wa mazao au uzalishaji wa sumu hiyo

Anasema Sumu hiyo inazalishwa na vimelea vinavyoitwa aflatoxin ambapo vyenyewe vinatoa sumu endapo ile hali inayowawezesha ya kutoa sumu inakuwepo ambayo ni hali ya jotoridi,unyevunyevu na humidity.

“Teknolojia yangu inafanya kazi baada ya kuvuna chakula na sio shambani lakini utafiti umeonesha kuwa upotevu mkubwa wa mazao unatokea pale baada ya kuvunwa na kuhifadhiwa na sio mazao hayo yakiwa shambani.

“Kama kiwango kinachotakiwa hakijafikiwa,hivi vijijdudu haviwezi kutoa sumu,na wanapenda sana kutoa sumu hii kwenye mahindi,Mtama na hata Karanga na ikiwa mazao haya yataathirika basi utaona ni kwa jinsi gani watanzania wanavyoathirika na hii sumu.

“Pia hivi vijidudu vinatoa sumu kwenye Karanga ambavyo ni vyakula muhimu sana kwenye nchi yetu,kwa mimi ndio maana nilijikita katika kufanya utafiti ambao utazuia uzalishaji wa sumukuvu basi nitaweza kusaidia kupunguza kabisa tatizo la wagonjwa kwa watanzania”anaeleza Prof.Kaale

Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Chakula,Sayansi na Teknolojia Profesa Mshiriki Lilian Kaale (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam jinsi teknolojia yake ya kudhibiti sumukuvu inavyofanya kazi

Aidha Prof.Kaale anasema sumu hiyo kwa kiasi kikubwa inaathiri sana Ini ambapo utafiti wake ulijikita huko ambapo baada ya kutafiti nan a ndipo alipobuni teknolojia hiyo ambayo sasa ipo sokoni

“Lengo letu kubwa ilikuwa ni kuangazia jinsi ya kuweka vituo ambavyo vitatoa tahadhari kwenye maghala ya kuhifadhi nafaka hizo ambapo ndipo tulipoweka tenkolojia hiyo.

“Unapovuna mahindi au Karanga au zao lolote,tunasema bado linaendelea kuishi na kupumua au kufanya kitu kinaitwa ‘respiration’ambapo inasababisha ongezeko la joto lakini pia inasababisha ongezeko la unyevunyevu ambazo ni hali muhimu sana kwa hivi vijidudu kutoa hii sumu.

“Sasa tukiwa kule kwenye maghala na vitu hivi vikiwa vinaendelea kuna uwezekano mkubwa kabisa wa kuwepo kwa hii sumukuvu,sasa sisi tulichofanya ni kuangalia jinsi gani ya kutengeneza hii tenkolojia na kuiweka kwenye hayo maghala hasa ya Serikali kutokana na ughali wa teknolojia yenyewe”anaongeza Prof.Kaale

Anabainisha kuwa wamependekeza kuiweka huko kwenye maghala kwa sababu mkulima mmoja mmoja hawezi kumudu gharama zake hivyo waliona ni jinsi gani wanavyoweza kuingia ubia na Serikali ili iweze kuwekwa katika maghala ya Serikali.

“Inapofikia hali ya mazingira yanaweza kuruhusu wadudu hao kuanza kuzalisha sumukuvu basi teknolojia yetu inaanza kutoa tahadhari kwa aina mbili ambapo moja itatolewa pale pale kwenye ghala lakini ya pili itatolewa tahadhari kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa yule ambayo anasimamia maghala hayo.

“Hii ndio kitu muhimu kabisa ambacho kinamfanya huyu mdudu anatoa sumu katika hali ya Temperature,Hummidity  na Moisture Content na ukiweza kuvidhibiti hivi sumukuvu haizalishwi kabisa”anabainisha Prof.Kaale

Prof.Kaale anafafanuwa kuwa teknolojia yake wameanzia kuifunga Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma chini ya uangalizi wa Wizara ya Kilimo mwaka 2025 na wanaendelea kufuatilia kwani bado Serikali haijaweza  kuupokea kabisa kabisa ambapo pia  Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (FAO) limeonesha nia kubwa katika suala hilo na hadi sasa tayari tumeshafanya utaratibu wote na FAO na tunaendelea kusubiria majibu lakini pia bado tunaendelea na Utafiti

Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Chakula,Sayansi na Teknolojia Profesa Mshiriki Lilian Kaale (wa tano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari pamoja na maofisa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia walipomtembelea ofisini kwake mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam

COSTECH yampatia mamilioni ya fedha

Akizungumzia uwezeshwaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,Prof.Kaale anabainisha kuwa COSTECH wamempatia kiasi cha Sh.Milioni 120 ili aendeleze ubunifu wake na hela ambayo ameipata kutoka COSTECH imemsaidia sana na kumpanua mawazo ambapo sasa hivi wanaandika mradi mkubwa kabisa na watu kutoka nchini Norway kuhusu sumukuvu na ni hiyo ni kwa sababu ya maarifa aliyopata kutoka COSTECH.

“Niliona tusiishie tu kutafiti hali inayozalisha sumukuvu lakini pia tuangalie tatizo limekuwa kubwa kiasi gani hasa katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Njombe na Iringa

“Nilikuwa nataka kuona ni kwa nini hawa watu wanazalisha vyakula sana lakini bado kuna utapiamlo katika mikoa hiyo.

“Kwa hiyo mradi huu ambao tunakwenda kuundika sasa hivi tunakwenda kuangalia kama kuna ushirikiano kati ya wadudu wanaozalisha sumukuvu na ukuaji wa watoto kwenye eneo hilo”anaeleza Prof.Kaale

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022. (DHS-MIS 2022)

Kauli ya Prof.Kaale inaenda sambamba na  Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (DHS-MIS 2022) uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa upande wa Hali ya Lishe kwa Watoto ambao umeleeza kuwa utafiti wa mwaka 2022 ulipima hali ya lishe miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Utafiti huo umeeleza kuwa hali ya lishe kwa watoto hupimwa kwa kulinganishwa na viwango rejea vya ukuaji wa watoto kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) vya mwaka (2006).

“Kwa ujumla, asilimia 30 ya watoto chini ya miaka mitano  wana udumavu,Udumavu huashiria hali ya lishe pungufu kwa muda mrefu.

 “Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa hali ya udumavu hupungua endapo elimu ya mama na hali ya uchumi wa kaya itaongezeka. Kiwango cha udumavu maeneo ya vijijini ni kikubwa (asilimia 33) ukilinganisha na maeneo ya mijini (asilimia 21).

“Mkoa wa Mjini Magharibi una kiwango cha chini cha udumavu (asilimia 13) na mkoa wa Iringa una kiwango cha juu (asilimia 57) ikilinganishwa na mikoa mingine.”umeeleza utafiti huo

Aidha utafiti huo umeonesha kuwa asilimia tatu ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano  wana ukondefu (kulingana na kigezo cha uzito na urefu wao).

Aidha umebainisha  kuwa, asilimia 12 ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano  wana uzito pungufu ambapo viwango vya hali ya lishe na ukuaji wa watoto chini ya miaka mitano vimeendelea kuboreka ukilinganisha na miaka iliyopita.

“Viwango vya udumavu vimepungua kutoka asilimia 50 mwaka 1991-92 hadi kufikia asilimia 30 mwaka 2022.

“Asilimia ya watoto chini ya miaka mitano  wenye udumavu kimkoa, Iringa inaongoza kwa hali hiyo ikiwa na asilimia 57 ikifiatiwa na Njombe na Rukwa ambayo yote ina asilimia 50 ya hali hiyo”umeongeza utafiti huo

Prof.Kaale ambaye pia ni Mkurugenzi wa  Kampuni ya Innovation and Entrepreneurship Centre ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDIEC) anabainisha “Hatujafanya utafiti ni namna gani sumukuvu inavyoweza kuhusishwa na ukuaji wa binadamu hasa kwa watoto lakini mimi ninauhakika kabisa kwamba sumukuvu inaweza kuwa na madhara kwa ukuaji wa watoto na ni muhimu pia kwa Serikali kuona ni jinsi gani inaweza kuwekeza  kwenye eneo hili ili kuweza kuokoa matatizo ya sumukuvu.

 “Nimefanikiwa kuwasimamia wanafunzi mmoja wapo akiwa ametoka COSTECH  ambaye yeye anaendelea na utafiti wa jinsi gani ya kuondoa sumukuvu ambayo tayari imeshakuwa katika mahindi.

“Utafiti huo bado unaendelea na umeanza kuonesha mafanikio lakini pia ninachoweza kusema,Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeweza kufungua milango kwenye maeneo yangu ya utafiti hasa katika eneo hili la sumukuvu kwa sababu ni eneo ambalo ni muhimu na linaathiri watu wengi sana”anasema Prof.Kaale

Prof.Kaale anaongeza kuwa sumukuvu ni tatizo kubwa sana tena linatakiwa liwe la kiserikali na kisera kwa sababu ni tatizo ambalo limeingilia vyakula ambayo tukisema tuna watanzania milioni 62,watu milioni 50 kwa siku wanakula chakula kinachotokana na mahindi mtama au karanga

“Naishukuru sana COSTECH kwa kuweza kuniunga mkono kwenye huu ubunifu wangu ,lakini pia wasichoke kuendelea kufadhili watu wengine hasa kwenye maeneo nyeti kama hili la sumukuvu ambalo atahari zake ni kubwa zinazoweza kuwaathiri watanzania”anabainisha Prof.Kaale

Ubunifu na Dira ya Maendeleo ya 2050

Akizungumzia kuhusu ubunifu wake na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Prof.Kaale      anasema Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050 inaongelea uchumi wa nchi kwa mapana yake na ubunifu wake sio tu kwamba unakwenda kuzalisha ajira lakini pia ukipitishwa rasmi na kuanza kutumia basi hautatumika Tanzania pekee bali pia kwenye Bara la Afrika kwa mapana yake.

“Ukiweza kupunguza upotevu wa vyakula, basi unaongeza pato kubwa kabisa serikalini, ukiangalia mahindi ni zao ambalo kwa  Serikali sio zao la chakula bali pia ni zao la biashara.

“Ukifika Dodoma pale Kibaigwa utaona ni jinsi gani raia wa Kenya na wa nchi zingine zinazotuzunguka wanafanya biashara,lakini sasa tusifanye biashara kwenye kitu ambacho hakipo salama,na kama tunaweza kuuhakikishia umma na mataifa ambayo yametuzunguka kwamba chakula chetu ni bora kabisa kwa sababu ya teknolojia tuliyoiweka ya kuondoa kabisa tatizo la sumukuvu basi mapato ya wakulima na Serikali yataongezeka zaidi na kuinua uchumi wa Taifa letu

“Lazima sasa ubunifu huu unatakiwa kuwa endelevu kwani unaenda kuleta mabadiliko na hivyo kuendana kabisa na uchumi unaoongelewa katika Dira yetu ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kupunguza upotevu wa chakula.

“Ubunifu huu sio tu unamsaidia mkulima mmoja mmoja lakini pia inasaidia Serikali  na Taifa kwa ujumla kuanzia mambo ya afya,kwani yale mahindi yatakuwa hayana sumukuvu na hakutakuwa na upotevu na wakulima watapata faida kwani hawatamwaga tena mahindi yao kwa sababu yana sumukuvu na kupata hasara hali itakayopelekea kushindwa kulima tena kwa kukosa mtaji.

Mbali na hilo lakini pia ubunifu huo umezalisha ajira kwa watu wa ICT kutumia mfumo huo ikiwemo kufanyia  ukaguzi na marekebisho unaotakiwa kufanyika mara mbili kila mwaka.

“Ubunifu huu unachangia kwa kiasi kikubwa kabisa uchumi wetu lakini pia unaendana na Dira yetu ya Maendeleo ya 2050

Upatikanaji wa Teknolojia ya kudhibiti sumukuvu

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa teknolojia ya kudhibiti sumukuvu  Prof.Kaale anasema kwa wafanyabiashara wa kiwango cha kati na juu wanaweza kupata teknolojia hiyo kwa kuwa gharama zake zinafikia kiasi cha TSh.Milioni 30 kwa mfanyabishara kuweza kuweka mifumo ya teknolojia hiyo katika ghala lake.

“Pia teknolojia hii unaweza kuitumia mahali popote,mfano sisi hapa tulipo UDSM tunaudhibiti wa ule mfumo uliofungwa kule wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma tunaona kila kitu hadi hali ya joto kama limeshuka au limepanda.

“Hata kama sisi tukiona tofauti hapa katika mfumo basi tunamtaarifu yule aliyekuwa katika eneo la ghala kwenda kuangalia tofauti hiyo na kwa kuwa mfumo huu tayari umeshafungwa tunaendelea pia kurekebisha vitu vinavyojitokeza ili uweze kuwa katika hali ya kisasa zaidi.

“Tuna software na hadware na ikileta shida basi mtu wa ghala anapatiwa taarifa na kumpa maelekezo ya jinsi ya kufanya kwani hata hao wanaosimamia maghala wameshapewa mafunzo maalum ya kutumia teknolojia ambayo simu yake inamuonesha kila kitu”anasema Prof.Kaale

“Sasa hivi tupo kwenye hii awamu ya uangalizi ,tungependa kabisa hii teknolojia iwekwe kwenye maghala tofauti ya Serikali hata pia ya wafanyabiashara  na wale wakulima ambao hawawezi kupata teknolojia hii wanaweza kusaidiwa na Serikali kwani kuna maghala yapo huko vijijini ambapo wakulima wanaenda kuhifadhi mahindi yao pale na wanalipia.

“Sasa ikiwa maghala yapo na Serikali ikaweza kuweka hii teknolojia inaweza kusaidia wakulima wengi zaidi katika eneo hilo kuweza  kuondoa tatizo la sumukuvu kupitia teknolojia yake.

“Mchele kwa kiasi kidogo sana lakini mahindi kwa kiasi kikubwa zaidi,mfano pumba za mahindi ukimlisha kuku au mnyama na wewe ukanywa yale maziwa tayari ule mzunguko wa sumukuvu uko pale pale.

“Huu mfumo ukishaweka ndani ya ghala hasa ukutani,kuna kuwa na vitu kama feni na vingine na baada ya hali ikishaanza kutaka kufikia hali ya wadudu hao kuzalisha sumu basi feni zitaanza kufanya kazi  mara moja na kuanza kufyoza ule unyevunyevu au milango kufunguliwa ili kutoruhusu wadudu hao kutoa hiyo sumu.

Prof.Kaale anaeleza wameanza na Mkoa wa Dodoma ambapo hiyo ndio sehemu ya kwanza kugundua huyo mdudu baada ya watu kadhaa kufariki 2015 baada kupimwa na kugundulika chakula walichokula kilikuwa na sumukuvu na ndio sababu ya kuona umuhimu wa kufanya utafiti katika Wilaya za Kondoa na Chemba.

“Kwa sasa kazi nyingine inayoendelea ya utafiti ni kuondoa sumukuvu katika mahindi au nafaka zenye sumu ili yaweze kuendelea kutumika tena na sio kumwagwa hivyo tukifanikiwa kudhibiti sumu hii katika maghala basi tutaondoa tatizo hili”

Discussion about this post

Contact us:

BAJETI COMMUNICATION

info@bajeti.co.tz
bajetinews@gmail.com
+255718699828
P.o.BOX 18133,
DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Category

  • Habari
  • Magazeti
  • Makala
  • Mazingira
  • Michezo
  • Picha
  • Sayansi na Teknolojia
  • Siasa

Our Visitors

  • Today's visitors:2
  • Today's page views 3
  • Total visitors 16,316
  • Total page views 18,502

Kuhusu Tovuti Hii

Hii ni tovuti ya habari iliyojikita katika kuandika  habari za kina   zikiwemo za mazingira kwa lengo la kuelimisha na kuuhabarisha umma.

Subscribe

  • About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact

© 2025 Bajeti

No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo

© 2025 Bajeti

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In