NA GOODLUCK HONGO
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Charles Kichere ameibua upya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited
Mnamo tarehe 27 Oktoba 2013, Serikali ya Tanzania na kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL) ziliingia makubaliano ya Hati ya Kujikinga na Hasara (Deed of Indemnity) ili kuilinda Serikali dhidi ya madai yoyote kutoka kwa upande wa tatu yatakayotokana na kutolewa kwa fedha katika akaunti ya escrow.
Hali hiyo ilifuatiwa na Hati ya Makubaliano kati ya IPTL na Serikali iliyotiwa saini mnamo tarehe 1 Machi 2021 ili IPTL aweze kulipa madai ya Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) ambayo ilikuwa na maslahi katika fedha za akaunti ya Escrow, ambazo zililindwa na Hati ya Kujikinga na Hasara, na kuiondolea Serikali wajibu wake kama mdhamini wa mkopo wa IPTL ambao haujalipwa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 iliyotolewa Machi 30,2026 imeeleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2024/25, Serikali pamoja na TANESCO waliingia katika Hati ya Makubaliano na Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) ili kulipa madeni ya Benki hiyo ya dola za Marekani milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 268), ambayo yalitokana na IPTL kutoa fedha za escrow bila kulipa deni la mkopo kwa Benki.
Kufuatia makubaliano, Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 268 kwa TANESCO kwa ajili ya fedha za maendeleo, na baadaye TANESCO ikalipa kiasi hicho kwa Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) ili kulinda maslahi ya Serikali.
Hata hivyo, wajibu wa kurejesha mkopo huo hapo awali ulikuwa wa IPTL, kama ilivyovibainishwa chini ya Hati ya kujikinga na Hasara (Deed of Indemnity) ya mwaka 2013 iliyotiwa saini wakati wa utoaji wa fedha kwenye akaunti ya escrow.
Katika kipindi cha ukaguzi, nilibaini juhudi zisizotosheleza za kurejesha kiasi cha shilingi bilioni 268 kutoka kwa IPTL, jambo linalothibitishwa na kukosekana kwa hatua za ufuatiliaji pamoja na nyaraka wezeshi.
“Ninarejea pendekezo langu kuwa Serikali kwa kushirikiana na TANESCO wasimamie utekelezaji wa wajibu wa IPTL wa kulipa dola za Marekani milioni 100 kwa mujibu wa matakwa ya Hati ya Makubaliano ya mwaka 2021 kama sehemu ya utekelezaji wa hatua madhubuti za kisheria na kifedha.”amesema CAG Kichere

Discussion about this post