NA MWANDISHI WETU,MANYARA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Anthony Diallo amewataka wakulima nchini kutumia teknolojia bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea.
Dkt.Diallo ametoa kauli hiyo Oktoba 13,2024 mjini Babati mkoani Manyara wakati alipokamilisha mbio za mbolea katika kilele cha Siku ya Mbolea Duniani.
Dkt. Diallo amesema zipo teknolojia za ina mbalimbali za kilimo zinazosaidia tija ya mavuno ikiwemo matumizi ya mimea na kufukuza visumbufu vya mazao.
Aidha ameongeza kuwa mmea unahitaji kupata chakula sahihi ambacho kinatokana na matumizi sahihi ya mbolea na kuwataka wakulima kutumia kilele cha maadhimisho ya siku ya mbolea kujifunza mbinu za kilimo bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent amesema kuwa TFRA imeleta mbio za mbolea kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia michezo.
Ameongeza kuwa kilimo kinahusisha afya hivyo pamoja na mambo mengine wakulima waliopata fursa kushiriki mbio za mbolea wamenufaika kwa kujenga afya pamoja na kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Dunia huadhimisha siku ya Mbolea kila ifikapo Oktoba 13 ya kila mwaka ambayo kitaifa inafanyika mjini Babati mkoani Manyara ikitanguliwa na Mbolea day fun run iliyowakutanisha pamoja wakulima na wadau wengine wa tasnia ya mbolea kujenga afya ya mwili na kubadilishana uzoefu.




Discussion about this post