NA MWANDISHi WETU
KIKUNDI Cha Wamachinga kilichopo Kawe ,Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kampuni ya Camgas -Camel Oil Ltd,kimeamdaa kongamano la kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia na kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizI ya gesi safi
Kikundi hicho maarufu kama ‘Ngome ya Mama Samia’ kimebainisha kuwa Kongamano hilo litakalofanyika Agosti 26,2025 Msasani Beach Manispaa ya Kinondoni na litaihimiza pia jamii iweze kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa ambayo imekua ikiathiri afya za watumiaji pamoja Mazingira kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mratibu Mkuu wa Kongamano hilo Potipoti Ndanga aliyoitoa Agosti 21,2025,katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni kutokana na utafiti walioufanya kuanzia ngazi ya Serikali ya Mtaa,huku kaulimbiu yake ikiwa ni”Gesi safi ni habari ya Mjini”.
Tawaomba wakazi wa Wilaya ya Kinondoni kupitia majimbo yake ya Kawe,Kinondoni yenye jumla ya Kata 20 kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwa kuwa kutakuwa na fursa mbalimbali zitakazopatikana katika Kongamano hilo.
“Tumefanya utafiti kuanzia ngazi ya chini(grassroot)ambapo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa tumefanya utafiti tukapata mpishi bora mmoja kwenye Kata ambaye atawakilisha Kata katika Mashindano ya kumpata mpishi bora kwenye kongamano hilo.”amesema Ndanga .
“Tumewapata wakina mama kutoka Kata 20,ambao watakuja kwenye Mashindano ambayo Jimbo la Kawe lina Kata 10 na Kinondoni Kata 10.
Aidha Ndanga ameongeza kuwa lengo kuu ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara katika kutangaza Nishati Safi ya kupikia.
“Sasa kama Rais wa Nchi anatumia Gesi Safi ya kupikia,kwa nini wewe mwananchi usitumie gesi safi ya kupikia?ameongeza Ndanga .
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Afisa Mtendaji wa Kata ya Kawe Husna Nondo amefafanuwa kuwa kutumia Nishati Safi ya kupikia kunasaidia kuweka Mazingira Safi katika Manispaa hiyo.
“Tunataka kata zetu zote 20 za Manispaa ya Kinondoni,ikiwemo ya Kawe, Mitaa,na wafanyabiashara waweze kutumia Nishati Safi ya kupikia,na siku ya kongamano tutatoa Elimu mbalimbali juu ya matumizi bora ya Nishati Safi kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan”amesema Nondo.
Aidha ameongeza kuwa Nishati Safi imewafikia wananchi wa Kata ya Kawe,na hivyo wawe tayari kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Camgas-Camel Oil Ltd ambao ni wadhamini wa kongamano hilo Sadiq Abrt ameeleza kuwa yeye kama mwekezaji mzawa ameamua kudhamini Kongamano hilo ikiwa ni kuunga mkono Serikali ya kutangaza agenda ya kitaifa ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.
“Sisi CAMGAS tunatambua jitihada za Serikali,hivyo siku ya Kongamano tutatoa punguzo kwa wananchi watakaonunua mitungi ya gesi ya kupikia ili kuhakikisha jamii inatumia nishati hii muhimu ambayo haiathiri afya na mazingira ya wananchi” amesema Abrt
Naye Balozi Kampuni ya CAMGAS-CAMEL OIL LTD Dotto Magari amewataka wananchi wakiwemo wa Manispaa ya Kinondoni kuachana na matumizi ya Nishati Chafu ya kupikia na badala yake watumie nishati safi ikiwemo Gas itokanayo na kampuni ya Camgas.
Mlezi wa Ngome ya Mama Samia Kawe, Zainabu Janguo amebainisha kuwa ngome hiyo ina wanachama wapatao 459,na wataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.
“Tutalizindua kongamano hili kwa mara ya kwanza katika Wilaya ya Kinondoni lakini pia tuna mpango wa kufanya kongamano hili katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar Es Salaam,pia tutakua na mashindano ya kutafuta mpishi bora ambaye atapatiwa zawadi ya jiko la gas safi ya kupikia” ameongeza Janguo.




Discussion about this post