NA GOODLUCK HONGO
KITUO cha kuzalisha umeme wa maji katika bwawa la Kidatu mkoani Morogoro pamoja na Nyumba ya mungu mkoani Kilimanjaro vimefikisha zaidi ya umri wa miaka 50 tangu yalipojengwa kwa ajili ya uzalishaji wa nishati hiyo.
Hata hivyo baadhi ya mitambo yake imechakaa na kupelekea kushindwa kuzalisha umeme kwa kiwango cha asilimi 100 huku Kituo cha Kidatu kikizalisha asilimia 49 ya uwezo wake.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 iliyotolewa Machi 30,2026 imeeleza kuwa mfumo wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji katika Shirika la Umeme Tanzania (bila kujumuisha Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere) una jumla ya vituo vinane vyenye uwezo wa kuzalisha megawati (MW) 1,501.8, ambavyo vinahitaji ukarabati mkubwa au kubadilishwa.
Ripoti ya CAG Kichere imeeleza kuwa miongoni mwavyo, kipo kituo cha Kidatu kilichotakiwa kuzalisha (kilowati 204,000) kilichoanza kazi mwaka 1975, na Nyumba ya Mungu (kilowati 8,000) kilichoanza kazi mwaka 1968.
Aidha imeongeza kuwa kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2024/25, vituo vyote viwili vilikuwa vimefikia miaka 50 ya muda wake wa matumizi unaotarajiwa.
“Ufanisi wa vituo hivi umepungua; ambapo uzalishaji halisi wa mwaka umekuwa wa asilimia 49 kwa Kidatu na asilimia 82 kwa Nyumba ya Mungu.”amefafanuwa CAG Kichere
Katika ripoti hiyo CAG Kichere amefafanuwa kuwa hali hiyo inafanya kuwapo kwa uhitaji wa ukarabati mkubwa au ubadilishaji mitambo kwa mujibu wa Kanuni ya 9(2) ya Kanuni za Fedha za Umma (Usimamizi wa Mali za Umma) za mwaka 2024.
“Kidatu uwezo uliowekwa ni kilowati 204,000,uwezo uliowekwa kwa mwaka ni kilowati 1,787,040,000,umeme halisi uliozalishwa ni kilowati 874,377,000 sawa na asilimia 49 ya uzalishaji halisi ikilinganishwa na uwezo uliowekwa .
“Nyumba ya mungu uwezo uliowekwa ni kilowati 8,000,uwezo uliowekwa kwa mwaka ni kilowati 70,080,000 na umeme halisi uliozalishwa ni kilowati 57,618,930 sawa na asilimia 82 ya asilimia ya uzalishaji halisi ikilinganishwa na uwezo uliowekwa”ameeleza CAG Kichere
Hata hivyo CAG Kichere amebainisha kuwa hali hiyo iliyotokana na ukosefu wa mipango kamili ya ukarabati, ikiwamo mikakati ya kifedha, imesababisha vituo vya zamani vya kufua umeme kwa njia ya maji kukabiliwa na ongezeko la gharama za matengenezo.
Pia, imesababisha viwe vinaharibika mara kwa mara, hivyo kusababisha kukosekana kwa uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme.
“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania lifanye tathmini ya kina ya vituo vilivyochakaa ili kubaini kiwango cha ukarabati kinachohitajika ili kurejesha utendaji wake.
“Pia, tathmini hiyo iingizwe kwenye mpango kazi wa mwaka na bajeti.” ameongeza CAG Kichere


Discussion about this post