KIGALI,RWANDA
TANZANIA imeweka utaratibu wa kisheria wa kugawa mapato yatokanayo na Biashara ya Kaboni kwa lengo la kuhakikisha jamii zinazoshiriki katika miradi hiyo zinanufaika na rasilimali zinazotokana na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika Mkutano wa Viongozi wa Ngazi ya Wizara na Wataalamu, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika 2026, uliohitimishwa Oktoba 15, 2026, jijini Kigali, Rwanda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema sehemu kubwa wa mgawanyo wa mapato unaenda kwa wamiliki wa rasilimali ikiwa ni mradi wa misitu asilimia 61, asilimia 31 inakwenda kwa mpendekezaji mradi na asilimia nane kwa Serikali.
Amesema utaratibu huo unaweka msingi wa uwazi katika usimamizi wa mapato ya Biashara ya Kaboni na kupunguza uwezekano wa migogoro ya mgao kati ya wawekezaji, Serikali na jamii zinazoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Meneja wa Uendelevu Afrika Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA),Dennis Kimani pembezoni mwa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika 2026, uliohitimishwa Oktoba 15, 2026, jijini Kigali, nchini Rwanda.
Mhandisi Masauni ameeleza kuwa Biashara ya kaboni ni sehemu ya juhudi za Tanzania kutekeleza malengo yake chini ya Mkataba wa Paris, ikiwemo kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa asilimia 30 hadi 35 ifikapo mwaka 2030.
Amesisitiza kuwa uzoefu wa Tanzania unaonesha umuhimu wa kuwa na sheria imara, taasisi yenye majukumu yaliyo wazi, mifumo ya kidijitali na utaratibu wa haki wa kugawa manufaa kwa jamii ili kuhakikisha miradi ya kaboni inaleta matokeo yanayoweza kuonekana kwa wananchi na kuchangia uhifadhi wa mazingira.
“Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji na nchi nyingine za Afrika na nje ya Afrika katika kuendeleza uwekezaji wa miradi ya kaboni yenye uadilifu na ubora wa hali ya juu, kwa lengo la kuhakikisha biashara hiyo inawanufaisha wananchi na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhandisi Masauni.
Ameongeza kuwa Tanzania inaunga mkono ushirikiano wa nchi za Afrika katika kujenga mfumo wa pamoja wa masoko ya kaboni unaozingatia maslahi ya Bara la Afrika na kuhakikisha manufaa ya biashara hiyo yanawafikia wananchi wote.
“Tunataka kuona masoko ya kaboni yakifanya kazi kwa manufaa ya wananchi wetu, huku tukishirikiana na ndugu zetu wa Afrika kujenga mfumo wa pamoja unaolinda maslahi ya bara letu,” amesisitiza Mhandisi Masauni

Katika hatua nyingine, Masauni amesema Tanzania imeanza kutekeleza miradi ya Biashara ya Kaboni kwa kuzingatia masharti ya Mkataba wa Paris.
Ameeleza kuwa Agosti mwaka huu (2026), Tanzania ilisaini barua nne za idhini kwa ajili za krediti za kaboni zinayoweza kutumika nje ya Tanzania, baada ya kufanyiwa tathmini na Kamati ya Kitaifa ya thathimini ya miradi ya kaboni.

Hatua hizo zinaonesha umuhimu wa kuunganisha uwekezaji wa kaboni, usimamizi wa mazingira na manufaa ya kiuchumi kwa jamii, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kujenga masoko ya kaboni yanayozingatia uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu.


Discussion about this post