NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari,Mawasilino na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuwapelekea kile wanacholalamikia katika Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016 ili kutengeneza mazingira bora zaidi kuliko yaliyopo.
Nape ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa wanahabari wamepeleka maoni yao na wao kama serikali wametoa ya kwao na kisha kujadiliana ili kuona namna ya kuboresha.
Amesema Sheria ya Habari ilipotungwa ,ililenga kutatua matatizo ya habari ikiwemo ajira zao,maslahi yao,mazingira yao ya kazi,wajibu wao na haki zao.
Amesema inawezekana masuluhisho yaliyopo kwenye sheria ndio yanayogombaniwa kuwa ni sahihi au si sahihi.
“Katika mazingira hayo,serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa ,tukae mezani tuzungumze na huo mchakato hauwezi kuwa mfupi.
“Ni mchakato wa mazungumzo mie nimeukuta na tutaendelea nao,tuna malengo ya kuukamilisha mapema kadri inavyowezekana”amesema Nape
Nape ameongeza kuwa lengo nin kutunga sheria itakayokaa muda mrefu lakini sheria itakayokubaliwa na pande zote mbili ambayo itatengeneza mazingira kuwa bore zaidi kuliko yaliyokuwepo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema suala la Bodi ya Ithibati ni miongoni mwa mambo yanayokwenda kujadiliwa katika mchakato mzima wa kupitia upya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 iliyounda Bodi ya Ithibati.
“Ninachotaka kusema ni kwamba,serikali imeonesha dhamira kwamba tunataka kwenda kupitia upya sheria na taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria na Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016”amesema Msigwa




Discussion about this post