BRAZAVILLE,JAMHURI YA CONGO
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) limesema umri wa kuishi barani Afrika umeongezeka kwa wastani wa miaka 10 kwa mtu mmoja kati ya mwaka 2000 na 2019.
Hilo ni ongezeko kubwa kuliko ukanda mwingine kwa takwimu za shirika hilo duniani katika kipindi hicho ambapo sababu ya kuongezeka kwa umri wa kuishi ni kutokana na kuimarika kwa huduma za mama na mtoto.
Taarifa ya WHO Kanda ya Afrika iliyotolewa Agosti 4,2022 huko Brazaville, Jamhuri ya Congo, imenukuu taarifa ya mwaka 2022 ya kufuatilia huduma ya afya kwa wote Kanda ya Afrika lakini imeonya kuwa ugonjwa wa COVID-19 inaweza kutibua mafanikio hayo.
“Ripoti imebaini kuwa idadi ya miaka ambayo mtu anaishi akiwa na afya njema imeongezeka hadi umri wa miaka 56 mwaka 2019 kutoka umri wa miaka 46 mwaka 2000,” imesema taarifa hiyo ikifafanua kuwa, “ingawa bado tuko nyuma ya wastani wa Dunia wa umri wa kuishi wa miaka 64, bado katika kipindi hicho hicho, wastani wa kuishi duniani uliongezeka kwa miaka mitano pekee.”
Kuimarika kwa huduma za msingi za afya, mafanikio katika afya ya uzazi hasa kwa wajawazito, watoto wachanga na afya ya mtoto yamechangia kuongezeka kwa umri wa kuishi.
Maendeleo mazuri katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama vile Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), Kifua Kikuu (TB) na Malaria.
“Kwa wastani, utoaji wa huduma ya afya kwa wote, imeongezeka kutoka asilimia 24 mwaka 2000 hadi asilimia 46 mwaka 2019,” imesema taarifa hiyo.
Akizungumzia ongezeko la umri wa kuishi Afrika, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema ni ushahidi ya harakati za bara hilo kuboresha afya na ustawi wa wakazi wake.
“Ina maana watu wengi wanaishi maisha yenye afya, wanaishi muda mrefu na wachache wanatishiwa na magonjwa ya kuambukiza na wana huduma bora za kujikinga na magonjwa,” amesema Dkt. Moeti.
Hata hivyo ameonya kuwa maendeleo hayo yasifikie mwisho kwa kuwa bila hatua za kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani au kansa, mafanikio yaliyopatikana yatatokomea.




Discussion about this post