NA MWANDISHI WETU,DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema chochote anachokifanya Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania ni kwaajili ya watanzania wote.
Senyamule ametoa kauli hiyo jijini Dodoma Desemba 24, 2022 wakati akikabidhi zawadi mbalimbali za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya katika kituo cha Safina kilichopo Ntyuka nje kidogo ya jiji hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametuma salamu za Upendo na kuwaomba watoto hao kukua katika maadili ya kumpendeza Mungu na wanadamu na kwamba chochote anachokifanya ni kwaajili ya watanzania wote ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa ili watoto wapate elimu bora na kuongeza kiwango cha utafulu.
“Lengo na dhumuni la Mheshimiwa Rais ni kuona watoto wanasheherekea sikukuu kwa furaha na amani, kumbukeni kuwa chochote anachokifanya ni kwaajili ya watanzania wote ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa ili watoto mpate elimu bora na kuongeza kiwango cha utafulu, hivyo mkiwa darasani msikilize mwalimu na mkirudi kituoni muda wa jioni jisomeeni” Amesisitiza Senyamule.
“Chochote unachokifanya fanya kwa bidii kwani kila mtoto ana ndoto na malengo yake ya baadae, Serikali inatambua mchango wenu ndio maana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa zawadi hizi za vyakula na kiasi cha fedha ili wote mfurahie sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya”ameongeza Senyamule.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amewashukuru waangalizi wa watoto hao kwa kujitoa kwao kuwalea katika maadili mema na kumuomba Mungu kuendelea kuwabariki Walezi na wahudumu wengine katika malezi ya watoto hao.
“Jukumu lenu ni pamoja na kuhakikisha watoto hawa wasoma ili kuyatumia madarasa yanayojengwa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili tuwe na kizazi chenye maadili mema ya kitanzania na ndoto za kutimiza malengo ya watoto wetu”amebainisha Senyamule.

Kwa upande wake Mlezi wa Kituo cha Safina Neckson William ameishukuru Serikali kwa kutoa zawadi za sikukuu kwa watoto.
“Tunaishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusaidia kituo cha Safina tumefurahi sana kwa kuwa tuna watoto ambao pia wapo nje ya Safina.
“Kituo kina watoto kuanzia miaka miwili na mwaka huu tumefanikwa kupeleka Chuo Kikuu watoto wawili” amebainisha William
Zawadi zilizokabidhiwa ni pamoja na Mchele, Unga wa Ngano, Sabuni, Sukari, Mafuta, vinywaji pamoja na mbuzi wawili ambazo ni kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watoto katika kipindi hiki cha sikukuu.
Kituo cha Safina kilianzishwa mwaka 2004 na kina jumla ya watoto 40, wavulana 35 na wasichana 5 pia kitua hicho kinawasaidia watoto ambao wanatoka katika mazingira magumu.




Discussion about this post