NA MWANDISHI WETU.ITILIMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ametoa ufafanuzi kwa wananchi wa Itilima jinsi serikali itakavyotatua changamoto ya bei ndogo ya pamba nchini na uvamizi wa tembo katika makazi ya wananchi.
Ufafanuzi huo umekuja baada ya kuwapa nafasi wananchi kueleza changamoto zao ikiwa ni pamoja na bei ndogo ya pamba, upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo na uvamizi wa tembo katika makazi na maeneo ya shughuli za binadamu.
Kinana ametoa kauli hiyo Julai 28, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Laini A wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu akiwa ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, uhai wa Chama na kusikiliza changamoto za wananchi.
Akiwa mkoani humo Kinana amepokea malalamiko ya wananchi hasa wakulima wa pamba kwamba wanatumia gharama kubwa kulima zao hilo, lakini changamoto inayowakabili ni bei ndogo, hivyo walimuomba awasaidie kufikisha kilio chao kwa Chama na Serikali upatikane ufumbuzi wa bei ya pamba.
Akijibu changamoto hizo Kinana amesisitiza kuwa amechukua changamoto hizo na atakwenda kuzungumza na viongozi wanaohusika.
Hata hivyo Kinana amesema baadhi ya hatua ambazo zitasaidia kukabiliana na changamoto katika zao la pamba ni pamoja na kujenga viwanda vya,nyuzi na kuchakata pamba na kutengeneza nguo ili kusiwe na ulazima wa kupeleka zao hilo nje ya nchi.
“Mkuu wa Mkoa wenu (Yahaya Nawanga), mwaka huu amelima pamba katika kila heka moja amepata kilo 500, wewe unayelima hapa (Itilima) kwa utaratibu wako, heka moja unapata kilo 150, hamuwezi kufanana kwa mapato.
“Sasa ni kazi ya serikali kuwaleta watalaamu wawafundishe wananchi walime kilimo cha kisasa, na kuhusu malipo ya pamba nitakwenda kukutana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,tutazungumza kwa nini watu wasilipwe fedha kila wanapouza.
“Sio wanauza halafu wanalipwa nusu, halafu wanalipwa tena robo na baadaye robo nyingine, fedha inakuwa haina thamani,”amesema Kinana

Akizungumzia kuhusu uvamizi wa Tembo,Kinana amebainisha kuwa amekaa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya, mkoa na maofisa wa uhifadhi wanyamapori kuzungumzia tatizo la wananchi kuvamiwa na kuuliwa na tembo.
“Tumezungumza kuhusu fidia kwa watu wanaokufa, tumezungumzia mipaka kati ya wananchi na hifadhi, nitakaporudi nitazungumza na Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Waziri wa Ardhi hili jambo hili lifanyiwe kazi.” ameongeza Kinana.




Discussion about this post