NA BEATUS MAGANJA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na vyomvo vingine vya Ulinzi na Usalama wamefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa nyara za Serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere ( JNIA ) wakiwemo Kobe hai na vichwa vya Fisi.
Taarifa hiyo imetolewa Juni 13, 2024 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko kutembelea Hifadhi ya Pande iliyoko mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya hifadhi hiyo,Meja Jenerali Mstaafu Semfuko amesema bodi ya mamlaka hiyo imejipanga kuja na mipango madhubuti ya kuifanya Hifadhi ya Pande iliyopo jijini Dar es Salaam kuwa kivutio kwa watu waishio ndani na nje.
Aidha ameongeza kuwa Bodi yake imedhamiria kuwafanya watanzania waione Hifadhi ya Pande kuwa ni sehemu ya kipekee kwa ajili ya kustarehe na kupumzisha akili zao, na kwa kuanzia imeanzisha bustani ya wanyamapori hai ndani ya hifadhi hiyo ambao wako huru kutembea “free roaming” wakiwemo Nyumbu, Pundamilia, Swala.
Aidha amebainisha kuwa mikakati ya kuendelea kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo sambamba na kuongeza aina mbalimbali za vivutio vya utalii ikiwemo wanyamapori aina ya Twiga na Faru lakini pia kuongeza kasi ya kuitangaza hifadhi.
Meja Jenerali Mstaafu Semfuko ametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hifadhini humo kama vile ujenzi wa kumbi za mikutano, sehemu za kuchezea watoto na “eco lodge” na kusisitiza fursa bado zipo.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Kanda, Kamanda wa TAWA Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Sylvester Mushi amesema kutokana na umakini wa Kikosi cha Askari wa Mbwa na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wamefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa nyara za Serikali uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere ( JNIA ).
Amesema wamefanikiwa kuthibiti utoroshwaji wa nyara hizo wakiwemo wadudu aina ya N’nge 383, wadudu aina ya “Beatle” 261, Kobe hai saba, vichwa vya fisi 10, vichwa vya pimbi vitatu, vichwa vya ndege aina ya Korongo vitatu na bunduki mbili ambazo zilikamatwa katika Pori la Akiba Wami Mbiki.
Naye Mjumbe wa Bodi ya TAWA Prof. Suzanne Augustino ameleza kuwa kuhifadhi Pori la Akiba Pande,TAWA inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha utalii nchini.
Prof.Augustino amewataka watanzania wote wanaoshindwa kwenda kutalii katika hifadhi zingine kutokana na umbali watembelee hifadhi ya Pande ili kujionea vivutio vilivyopo.
Kwa upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Pande Dorothy Massawe ameishukuru TAWA kwa kuboresha miundombinu ya utalii katika hifadhi hiyo ambapo amekiri kuwa imekuwa chachu ya ongezeko la mapato na idadi ya watalii wanaoitembelea.




Discussion about this post