NA MWANDISHI WETU
HALI inatisha,ndivyo unavyoweza kusema baada ya wanawake kutoka mikoa 12 nchini kati ya 26,kutajwa kuwazidi wanaume katika matumizi ya dawa za kulevya huku Njombe ikiwa eneo pekee lenye idadi sawa kati ya wanaume na wanawake.
Uchunguzi wa Bajeti Communication umegundua kuwa mikoa ya Dar es Salaam,Pwani na Kigoma ukiwemo Shinyanga inaongoza kwa wanawake wengi kutumia dawa za kulevya kuwazidi wanaume.
Hata hivyo Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2015 inatoa hukumu ya kifungo cha miaka mitatu au faini ya kuanzia Sh.500,000 na isiyopungua Sh.1,000,000 au vyote kwa pamoja kwa kutumia dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2023 iliyotolewa Mwezi Mei,2024 na kusainiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,(Sera,Bunge na Uratibu) Jenista Mahagama na Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) Aretas Lyimo imeeleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2023 pekee jumla ya waraibu 903,062,wanaume wakiwa 470,324 na wanawake 432,738 walipatiwa huduma ya tiba ya uraibu wa dawa za kulevya kama vile bangi,,mirungi,heroine,cocaine,vilevi na sigara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya watu wenye uraibu walibainika kutumia dawa za hospitali zenye asili ya kulevya kama vile Valium,Pethidine na Tramadol ,hali iliyosababishwa na kukosekana na kupanda kwa bei ya dawa za kulevya mitaa.
Taarifa hiyo imeonesha mikoa ambayo idadi ya wanawake wenye uraibu wa dawa za kulevya waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili nchini mwaka 2023 na kuwazidi wanaume kuwa ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wenye wanawake 121,813 huku wanaume wakiwa 112,504.
Mkoa wa pili wenye wanawake wengi wenye uraibu kuliko wanaume ambao walipata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili nchini Mwaka 2023 ni Pwani wenye wanawake 32,843 huku wanaume wakiwa 29,471
Kigoma inashika nafasi ya tatu kwa wanawake wenye uraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili ukiwa na wanawake 17,122 huku wanaume wakiwa 12,241.
Taarifa hiyo ya DCEA imeeleza kuwa Mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya nne kwa wanawake wenye uraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili mwaka 2023 ukiwa na wanawake14,885 na wanaume wakiwa 13,700
Mikoa mingine ni Kilimanjaro wenye wanawake 13,412 wanaume wakiwa 10,908 unaoshika nafasi ya sita huku nafasi ya saba ikishikwa na Mtwara wenye wanawake 13,153 na wanaume 10,215 ukifuatiwa na Mkoa wa Simiyu wenye wanawake 11,451 na wanaume 9,996 ukishika nafasi ya nane.
Mkoa wa Manyara umeshika nafasi ya nane ukiwa na wanawake 11,087 na wanaume wakiwa 9,239 huku nafasi ya tisa ikishikiliwa na Mkoa wa Songwe wenye wanawake 10,159 na wanaume 9,134.
Rukwa imeshika na nafasi ya 10 kwa kuwa na wanawake wenye uraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya Afya ya Akili mwaka 2023 kwa kuwa na wanawake 9,022 na wanaume 5,763 ambapo Mkoa wa Lindi ukishika nafasi ya 11 nchini kwa kuwa na wanawake 8,224 na wanaume 6,630
Mkoa wa Njombe ndio eneo pekee linalooneka wanaume na wanawake hakuna aliyemzi mwenzake baada ya wanawake 8,223 na wanaume 8,223 ikiwa ni idadi ya watu wenye uraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili nchini mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo mikoa mingine 14 iliyobaki wanaume wanaongoza kwa idadi ya watu wenye uraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili nchini kwa Mwaka 2023.
Hata hivyo Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya katika kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo kwa kutoa tiba kwenye vitengo vya afya ya akili vilivyopo katika hospitali za wilaya,mikoa na rufaa nchini.
Mbali na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupitia DCEA chini ya Kamishna Jenerali Lyimo,kila mtanzania anapaswa kusaidia mapambano hayo ambayo sasa yanawanyemelea kwa kasi mama na dada zetu hivyo kusambaratika kwa familia na kutishia kizazi cha sasa na kijacho.




Discussion about this post