NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 500,000 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 840,000 mwaka 2023/2024 .
Ongezeko hilo limetokana ya ruzuku ya Mbolea inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Laurent ametoa kauli hiyo Septemba 22,2024 Chinangali ll wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma, wakati akikabidhi vyeti vya mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa vijana 192 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT)
Amesema ongezeko la matumizi ya mbolea nchini ni kubwa hadi kufikia tani 840,00 na hiyo inaashiria kwamba jamii imeelimika kuhusu matumizi ya mbolea.
“Ongezeko la matumizi ya mbolea ni kubwa,na hii inaashiria namna jamii ilivyoelimika na kutambua umuhimu wa mbolea kwenye shughuli zao za kilimo,
‘’TFRA inaendelea kupanua wigo wa utoaji elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili waendelee kunufaika” amebainisha Laurent

Akizungumzia vijana 192 waliotunukiwa vyeti na Mamlaka hiyo,Laurent ameeleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, TFRA imeratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na Idara ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) ili kutoa mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa kuzingatia Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009.
Aidha amefafanuwa kuwa vyeti hivyo vitawasaidia vijana hao kujisajili kuwa mawakala wa pembejeo za mbolea.
‘’Ninawapongeza vijana wa BBT kutokana na mafunzo mliyopata,ambayo yatawajenga katika Kilimo mnachoendelea kufanya.
‘’Mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa kwenu yana maana kubwa katika maandalizi ya msimu wa kilimo unaoelekea kuanza hivi karibuni”ameongeza Laurent
Hata hivyo Laurent ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuwalea vizuri vijana wa BBT jambo linalochangia kuzidi kukua kwa Sekta ya Kilimo nchini.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) Mathed Kahaya ameishukuru TFRA kwa mafunzo waliyotoa na kuongeza kuwa mafunzo hayo yawe endelevu na yasiishie hapo kwani yatasaidia kuwakumbusha vijana hao mambo ya kuzingatia kwenye Kilimo chao mara kwa mara.




Discussion about this post