NA GOODLUCK HONGO
CHAMA Cha ACT-Wazalendo kimesema kitadhibiti mzizi wa tatizo la biashara za dawa za kulevya kwa kuongeza biashara za halali na ajira kwa vijana.
Kauli ya ACT-Wazalendo imekuja wakati ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ikiimarisha mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ili kuimarisha afya za watanzania na amani kwa ujumla
Hata hivyo kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge na Uratibu) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeeleza kuwa kiasi cha tani 1965.34 za dawa za kulevya za aina mbalimbali zilikamatwa nchini kwa mwaka 2023 pekee
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ukamataji huo ni mkubwa kuwahi kutokea nchini katika historia ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya tangu nchi ipate uhuru wake.
Akizungumza na Bajeti Communication Septemba 23,2024 jijini Dar es Salaam juu ya mikakati ya chama hicho katika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya, Msemaji wa Sekta ya Afya wa chama hicho Dkt. Elizabeth Sanga amesema chama hicho kimejipanga kudhibiti biashara hiyo kikamilifu.
Amesema hali ngumu ya uchumi ni sababu kubwa ya watu kujiingiza kwenye tabia hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya na ulevi mwingine
‘’Kuthibiti mzizi wa tatizo , ACT-Wazalendo ina mikakati ya kuongeza ajira kwa vijana na kujenga mazingira bora ya kujiajiri na kuongeza biashara za halali mbadala wa biashara ya dawa za kulevya ambazo zitasaidia kupunguza matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayochochea matumizi ya dawa za kulevya.
‘’Kuimarisha sheria za kuthibiti biashara za madawa ya kulevya ikiwemo kutumia sera ya hifadhi ya jamii kumpa kinga mtanzania ”amebainisha Dkt.Sanga
Hata hivyo Dkt.Sanga ameongeza kuwa chama chao kitaimarisha huduma za afya ya akili kwa kutilia mkazo kuimarisha huduma katika ngazi za msingi yaani vituo vya afya na zahanati, kwa kuwa hali hiyo itawezesha walio katika changamoto za afya ya akili zinazoongeza uwezekano wa wao kuingia katika majanga ya matumizi ya dawa za kulevya kupata huduma za kinga na matibabu mapema.
Mbali na hilo lakini chama hicho pia kimejipanga kutoa elimu kwa vijana itayowasaidia kuepuka tabia za matumizi ya dawa ya kulevya.
Wanasiasa wamekuwa na nafasi chanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwa wanachama wao wengi ni vijana na hupata fursa ya kuhutubia maelfu ya watu katika mikutano yao ya hadhara hivyo kusaidia Serikali katika kukabiliana na biashara hiyo nchini.




Discussion about this post