NA MATILDA KASANGA, TFRA
MAADHIMISHO ya Siku ya Mbolea Duniani yatakayofanyika Oktoba 13,2024 kwenye Uwanja wa Stendi ya Zamani mjini Babati, mkoani Manyara,
Maoneshao hayo yanatazamiwa kuvuta hisia za wananchi wa mkoa huo watakapopata fursa ya kukutana na wataalam kuelezea mafanikio ya kampeni iliyoshika kasi nchini ya ‘Kilimo ni Mbolea.’
Kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na mikoa mingine nchini siku hiyo itakuwa ni jukwaa maalum ambalo litawapa fursa ya kujua mafanikio yaliyopatikana ya kampeni ya kitaifa ya Mbolea ni Kilimo.
Mbolea ni Kilimo ni kampeni mahsusi na ya makusudi ya kumkwamua mkulima kutoka kwenye umasikini na kumfanya atajirike kwa jasho lake katika Sekta ya Kilimo.
Tangu Tanzania Bara ijipatie uhuru wake kutoka kwa Waingereza zaidi ya miaka 60 iliyopita kumekuwepo na kampeni mbalimbali zilizolenga kuimarisha Sekta Kuu ya Kilimo
nchini.
Ni kampeni zilizobuniwa kwa makusudi ili kukuza sekta hiyo mama ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi kwa nchi nyingi za Bara la Afrika, ikiwemo Tanzania, tangu wakati wa utawala kikoloni.
Baadhi ya kampeni hizo ni pamoja na ‘Kilimo ni Uhai’, ‘Kilimo cha Kufa na Kupona’ na ‘Siasa ni Kilimo’’ ambazo zilibuniwa baada ya muongo mmoja wa uhuru ili kukifanya kilimo kuwa nguzo kuu ya uchumi.
Kwa sasa kampeni inayoendelea ya ‘Kilimo ni Mbolea ambayo inaweka mkazo katika matumizi ya mbolea ili kubadili kilimo cha asili cha miongo mingi na kiwe na tija kwa wakulima.
Kampeni hii inaongozwa na Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) chini ya utekelezaji wa Taasisi ya Black Codes Creativity (BCC) na ilizinduliwa rasmi katika Mkoa wa Ruvuma Julai 23, 2024.
Kwa mujibu wa Ripoti ya TFRA kuhusu kampeni hiyo, lengo lake kubwa ni kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbolea za kisasa na usajili wa wakulima kwenye mfumo wa portal ambao kwa sasa unawatambua wakulima zaidi ya 492,700 waliofikiwa kupitia matukio mbalimbali ya kikanda.
Taarifa ya TFRA inaeleza kuwa Kampeni hiyo imetumia mbinu nyingi za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na Redio, Television (TV), Magazeti, mitandao ya kijamii, mfumo wa PA, Balozi, SMS, Whatsapp na redio za kijamii ili kuongeza ushiriki.
Aidha imefafanuwa kuwa katika kampeni hiyo ya Kilimo ni Mbolea zimetumika mbinu mbalimbali za kuwaunganisha wakulima kwenye matukio na kidijitali.
Hii inajumuisha jumla ya wakulima waliosikia, kuona,au kusoma kuhusu kampeni kupitia matukio, SMS, mitandao ya kijamii, matangazo ya mtandaoni, vyombo vya habari, mahojiano ya redio, na vipeperushi.
‘’Katika mikoa mitano ambako shughuli za uandikishaji zimefanjyika, wakulima zaidi ya 1206 wamesajiliwa ambapo Mkoa wa Mara: 20, Kagera:76, Simiyu: 25, Tabora: 382, Katavi: 274, Morogoro: 183, Lindi 251) huku mitandao ya kijamii, zilichapishwa video na picha za kampeni ya Kilimo ni Mbolea ikiwemo kwenye akaunti za TFRA za Facebook, Instagram, na YouTube,”
“Tulitumia matangazo yanayolipiwa ili kuhakikisha maudhui yetu yanafikia watu wengi mtandaoni, pamoja na kumtumia balozi wa kampeni mkoani kuweka taarifa kwenye account yake ya mtandao wa instagram pamoja na Youtube na matangazo hayo yamewalenga wakulima sio tu kwenye mikoa tisa tunayofanya kazi bali pia nchi nzima kwa ujumla.”imebainisha taarifa hiyo
Hata hivyo faida kubwa ya matangazo ya mtandaoni ni kwamba ujumbe unaweza kufikia hadhira lengwa hata kama akaunti za TFRA hazina wafuasi wengi, lakini machapisho hayo ya mitandao ya kijamii yamefikia watu 2,240,564 wakiwemo wakulima 492,700.
Ripoti ya TFRA inataja mikoa tisa ya kipaumbele kuwa ni Ruvuma(Mbinga), Simiyu, Kagera, Mara, Tabora, Morogoro, Lindi, Manyara na Katavi na wadau muhimu wanaolengwa na kampeni hiyo ni pamoja na viongozi wa kisiasa (Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Wajumbe wa Halmashauri), Mameneja wa Kanda wa TFRA na Wataalamu wa Kilimo, Wakulima, Wananchi wengineo na taasisi mbalimbali
Shughuli maalum zilizokubaliwa kufanyika kila mkoa ni pamoja na ushirikiano na Serikali na wadau wengine,mikutano ya awali na Taasisi za Serikali na Mameneja wa Kanda wa TFRA ili kujadili hali ya eneo na mpango wa utekelezaji.
Shughuli nyingine ni ushiriki wa wakulima katika matukio makubwa ya elimu na burudani yatakayovutia na kuelimisha wakulima kwa kutumia maonesho na burudani yakiwemo mashamba ya mfano katika kila eneo lengwa, ushirikiano na redio za jamii, ushirikiana na vituo vya redio vya jamii na kufanya mahojiano na wataalamu na shughuli nyingine nyingi.
MAFANIKIO YA KAMPENI

Mafanikio ya kampeni hii ni kwamba wakulima 492,700 wamefikiwa kwa kutumia mbinu mbalimbali kwa kutumia SMS, WhatsApp, na mitandao ya kijamii ambapo jumbe za SMS 221,900 na za WhatsApp 70,549 zimefika maeneo ya tukio.
Kupitia mitandao ya kijamii watu 2,240,564 wamefikiwa na kufanya machapisho 57, wakati wakulima zaidi ya 1,206 wamesajiliwa kwa ruzuku za mbolea.
UJUMBE WA SMS NA WhatsApp
Usambazaji wa ujumbe kwa wingi kupitia SMS 221,900 na WhatsApp 70,549, ikiwaruhusu wakulima wengi kupata taarifa muhimu za kampeni licha ya changamoto za kufika kwenye maeneo ya tukio.

MITANDAO YA KIJAMII
Kupitia mitandao ya kijamii, watu 2,240,564 wamefikiwa na kufanya machapisho 57.
USAJILI KWA WAKULIMA

Kwa upande wa usajili kwa wakulima,mafanikio yaliyopatikana ni Wakulima zaidi ya 1,206 wamefikiwa kwa ruzuku za mbolea.
MIKOA MINGI YAFIKIWA
Kampeni imefanikiwa kufanyika katika mikoa nane, ikihusisha vyombo vya habari 72 na kufanikisha uenezaji mkubwa wa taarifa kupitia vipindi vya redio, blogu, na magazeti, ili kufikia wakulima wengi zaidi.
Uzinduzi wa kampeni wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma ulifanyika Julai 24, 2024 wakati mkutano na vyombo vya habari ulioratibiwa na BCC ulifanyika Julai 23,2024 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TFRA, Joel Laurent, alitambulisha kampeni kwa waandishi wa habari 20.
Balozi wa Kampeni, Mkojani, alitambulishwa, na tukio hili lilipokea taarifa katika vyombo vya habari vikubwa, likifikia watu wapatao 143,000.
Uzinduzi wa kampeni ulifanywa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, aliyehutubia wakulima zaidi ya 1,600 na kuzindua rasmi Kampeni ya Kilimo ni Mbolea
Wimbo wa kampeni ulianzishwa wakati Mtaalamu wa Kilimo wa TFRA ametoa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, na Mkojani alifanya tamthilia ya vichekesho,pia vifaa vya kutangaza,ikiwa ni pamoja na vipeperushi, T-shirts, na vests za mwangaza kwa waendesha bodaboda, vilipatikana.
Matukio yote yalirekodiwa na baadaye kugawanywa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Baada ya tukio la uzinduzi, mkutano ulifanyika na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA na timu ya BCC walijadili maendeleo ya kampeni na mikakati kwa maeneo yajayo, ikiwa ni pamoja na uandaaji upya wa ratiba ya kanda.
Kampeni hii kwa mikoa husika ilishirikisha vyombo mbalimbali vya habari ili kuhakikisha ujumbe unafika kwa hadhira katika eneo kubwa.
Vyombo vya habari kama televisheni ikiwemo ITV, Channel 10, na Star TV vilitumika kueneza taarifa kwa watazamaji, huku redio kama Radio Free Africa, Key FM, na Salvation FM zikifanikisha kufikia watu wa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wa vyombo vya habari mtandaoni, blogu na majukwaa kama Michuzi, Global TV, na Matukio Daima Media zilitumika kusambaza habari kupitia intaneti.
Magazeti kama Habari Leo, Nipashe, na The Guardian yalitumiwa kueneza taarifa pamoja na majukwaa ya kidijitali kama Habari Leo Digital na Mfanyakazi Digital.
Wakati tukiadhimisha Siku ya Mbolea Duniani 2024 mafanikio ya Kampeni ya Kilimo ni Mbolea yatakuwa ni chachu ya kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na hivyo kuchochea ukuaji wa Uchumi wa Taifa.
MWSHO




Discussion about this post