NA MWANDISHI WETU,MANYARA
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezitaka Kamati za Pembejeo za Wilaya kwa kushirikiana na wenyeviti wa wilaya kuhakikisha kuwa wakulima wanajisajili kwenye daftari la mkulima ili wasipitwe na fursa ya mbolea ya ruzuku.
Hata hivyo Sendiga amewataka wakulima waliojiandikisha msimu uliopita kuhuisha taarifa zao ili nao wasipitwe na fursa hiyo
Sendiga ametoa wito huo Oktoba 10, 2024 alipokuwa akifungua maonesho ya siku nne yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA) kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba 13, duniani kote.
Sendiga amesema, awali wakulima walikuwa wakihofia kuwa watakapojiandikisha watatozwa kodi na watanyang’anywa mashamba yao lakini baada ya elimu kutolewa na viongozi wa mikoa wakiongozwa na wakuu wa mikoa sasa wananchi wameelewa na wanajitokeza kujisajili.
Amesema, ili kuhakikisha mbolea zinafika vijijini wafanyabiashara wanawajibu wa kuhakikisha wanafikisha bidhaa hizo vijijini ili kufikisha huduma hiyo karibu na wakulima.
“Uwekaji wa mbolea mijini, makao makuu ya wilaya, makao makuu ya mikoa, hapo hakuna wakulima wakulima wako vijijini, kwa hiyo wafungue maduka ya pembejeo za kilimo vijijini ili kuwapunguzia wananchi mzigo mzito wa kuja kuchukua mbolea mjini na baadaye wanapata shida ya kusafirisha kwa mabasi inayopelekea gharama kuongezeka na kuondoa umuhimu wa ruzuku iliyowekwa na serikali” amesisitiza Sendiga.
Hata hivyo Sendiga ameiomba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhakikisha kuwa bei elekezi zinazotolewa zinaakisi uhalisia wa jiografia na miundombinu ya mikoa kutokana na umbali ambapo jiografia yake ni ngumu na hivyo kupelekea baadhi ya wananchi kushindwa kunufaika na ruzuku iliyowekwa kwenye pembejeo hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema, kupitia maonesho haya wakulima na wananchi watapata fursa ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na maeneo mengine yatakayowasaidia kuongeza uzalishaji.
Ameeleza kuwa, mbolea ni moja kati ya pembejeo muhimu zinazohitajika katika uzalishaji wa mazao, wakati mbegu bora zikichangia takribani asilimia 50 ya uzalishaji wa mazao na mbolea huchangia kati ya asilimia 20 hadi 40 na asilimia zinazobaki hutokana na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kwa jumla.
Amebainisha kuwa,Mamlaka inaamini kupitia maonesho hayo wakulima na wadau wengine watapata wasaa wa kujifunza na kubadilishana tekinolojia katika kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea nchini.
Amesema, maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanaambatana na matukio mbalimbali ikiwemo kongamano la kwanza la mbolea litakalofanyika kwa siku mbili yaani Oktoba 11 na 12 mkoani Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema licha ya Mamlaka kudhibiti biashara ya mbolea nchini Mamlaka imekuwa ikijikita katika kutoa elimu ya mbolea kwa wakulima.
Ameongeza kuwa kwa kipindi kirefu kumekuwa na mkazo wa kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini lakini Mamlaka ilinahakikisha elimu ya mbolea inaelekea maeneo mengine ya nchi ili kuwezesha wakulima kuongeza uzalishaji.
Amewasihi wananchi wa Babati na maeneo jirani kutumia maonesho hayo kujifunza kutoka kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa mbolea waliopo katika viwanja hivyo vya maonesho.

Kwa upande wa Manyara Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya wadau katika mnyororo wa thamani ambapo siku yan kilele ya Oktoba 13, 2024 itaambatana na matukio ya mbio za ridhaa (fun run), upandaji wa miti na halfa ya kufunga maadhimisho hayo itakayofanywa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe




Discussion about this post