NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amemteua Mhandisi Ramadhani Lwamo kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa muda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 15, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Dkt. Moses Kusiluka imesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali na kumteuwa Mhandisi Ramadhani Lwamo kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Lwamo alikuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume akichukua nafasi ya Mhandisi Yahya Samamba ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Julai 2, 2024.
Uteuzi wa Mhandisi Lwamo umekuja wakati akihitimiza udhibiti wa matumizi ya baruti ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea kutokana na ongezeko la matumizi yake
Akizungumza Januari 13, 2025 jijini Dodoma siku moja kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,wakati akifungua kikao cha kuwajengea uwezo wakaguzi migodi na baruti,Mhandisi Lwamo amesema kutokana na ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini, utafiti wa mafuta na gesi asilia na ujenzi wa miundombinu mbalimbali, kuongezeka kwa matumizi hayo pia kumepelekea kupanuka kwa biashara ya baruti hapa nchini.
Amesema matumizi ya baruti nchini Tanzania yameongezeka kutoka tani 3,000 kwa mwaka katika miaka ya 1990 hadi kufikia wastani wa tani 26,516.07 kwa mwaka 2024.
“Matumizi makubwa ya baruti maana yake uchimbaji umeongezeka, hivyo bila udhibiti italeta madhara, kikao hiki ni kujengeana uwezo na lengo ni kuhakikisha wachimbaji hawapotezi maisha au kupoteza viungo kwa ajili ya matumizi ya baruti.
“Ongezeko la uhitaji wa matumizi ya baruti hapa nchini kumepelekea uwepo wa changamoto kadhaa katika usimamizi wake, udhibiti madhubuti ni muhimu, mkadhibiti katika maeneo yenu, itakuwa ni aibu mkaguzi mgodi na baruti eneo lake mtu akapata madhara,”amesema Mhandisi Lwamo .
Aidha Mhandisi Lwamo amebainisha kuwa,mpaka sasa kuna zaidi ya bohari (magazine) 231, stoo 493, masanduku ya kuhifadhia baruti zaidi ya 279 yaliyosajiliwa kwa ajili ya kutunzia baruti migodini na maeneo ya biashara ya baruti.




Discussion about this post