NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma wamefanikiwa kuteketeza ekari 157 za bangi.
Operesheni hiyo iliyofanywa kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Haubi iliyopo wilayani humo, wamefanikisha hiyo operesheni maalum ya kutokomeza kilimo haramu cha bangi katika maeneo ya Hifadhi ya Milima ya Haubi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa mamlaka hiyo, Daniel Kasokola, amesema operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mei 14 hadi 19, imefanikisha uteketezaji wa ekari 157 za mashamba ya bangi yaliyokuwa katika vijiji vya Ntomoko, Kinyasi na Haubi

Amesema watuhumiwa saba wanashikiliwa kwa mahojiano huku pikipiki mbili zikikamatwa katika maeneo ya operesheni.
“Operesheni hii ni ya pili kufanyika mwaka huu katika Wilaya ya Kondoa,mwezi januari tulibaini na kuteketeza zaidi ya ekari 500 za bangi, kupungua kwa mashamba haya hadi ekari 157 ni ushahidi kuwa wananchi wameanza kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi na sisi tunawapongeza kwa ushirikiano huu.” amesema Kasokola.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatuma Nyangasa, amesisitiza kuwa Serikali ya wilayani humo itaendelea kushirikiana kwa karibu na DCEA katika kuhakikisha kilimo cha bangi kinatokomezwa kabisa na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa ili waachane na kilimo hicho haramu na badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao halali ya chakula na biashara kama vile tumbaku, ufuta na maharage.

“Tunawaomba wananchi waachane na kilimo haramu cha bangi na Serikali ipo tayari kuwaongoza katika kuelekea kilimo halali na chenye tija.
“Ushirikiano baina ya serikali na wananchi ndiyo silaha kubwa ya kuikomboa jamii yetu.” amesisitiza Nyangasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafai kilichopo wilayani humo, Shaibu Kalinga, amebainisha kuwa katika kijiji chao kumekuwa na historia ya kilimo cha bangi kwa muda ndefu, lakini kwa sasa viongozi wa kijiji wamejipanga kuongoza mapambano dhidi ya zao hilo haramu.
“Zamani bangi ilikuwa kama sehemu ya maisha kwa baadhi ya wakulima hapa kijijini, lakini sasa tunaelewa madhara yake,tumejipanga kutoa elimu na kuhamasisha kilimo halali tu.” ameongeza Kalinga
Naye Rajabu Hamis, mkazi wa Kijiji cha Mafai, amepongeza juhudi za Serikali kwa kutoa elimu kwa wananchi jambo ambalo limebadili fikra za wananchi kuhusu bangi.
“Tulilima bangi kwa sababu ya kukosa njia mbadala, lakini baada ya kupewa elimu na kuona jitihada za Serikali, tumeamua kuachana na bangi na kushirikiana na mamlaka kuitokomeza kabisa” amefafanua Rajabu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayejihusisha na kilimo, biashara au usambazaji wa bangi na dawa nyingine za kulevya




Discussion about this post