NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Cha African Democratic Alliance(ADA-TADEA) kimesema changamoto kubwa inayoikabili Tanzania kwa sasa ni Upendeleo,Rushwa na Ufisadi hali inayowakwaza sana wananchi hivyo Serikali yao ikichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 watafulia mbali suala hilio.
Hayo yamebainika ndani ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025-2030 ya chama hicho iliyozinduliwa Septemba 14,2025 Mbagala mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuzindua kampeni za urais,ubunge na udiwani ili kuwanadai wagombea wao nchi nzima.
Ilani hiyo imeeleza kuwa nchi hii ya wote hivyo Serikali ya Wananchi itakayoongozwa na Kiongozi kutoka ADA-TADEA itakuwa ni ya Watanzania wote na itazingatia Upendo, Uzalendo, Weledi na Uwezo wa mtu.
“Katika nchi yetu Tanzania changamoto kubwa kwa sasa ni Upendeleo, Rushwa, na Ufisadi,hali hiyo inawakwaza sana wananchi, hivyo, sisi tunakuja na mkakati maalum wa kuifutilia mbali hali hiyo.
“Waziri atatoka chama chochote ili mradi ana sifa stahiki, hali kadhalika kwa wakuu wa mikoa na wilaya nao watakuwa katika utaratibu ule ule.
“Nchi hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo Watanzania wote wana haki sawa, na nchi haitajengwa na Makada wa Chama Tawala bali itazingatia haki na usawa wa watu wote, kama kuna Mkuu wa Wilaya au Mkoa Tanzania Bara ambaye ni Mzanzibari, ni haki kuwa na Mkuu wa Mkoa au Wilaya Mtanzania Bara, Zanzibar, vivyo hivyo kama kuna Afisa Ardhi Mzanzibari katika Manispaa ya Tanzania Bara, ni haki kuwa na Mtanzania Bara kwenye Manispaa au mji wa Zanzibar.”imeongeza Ilani hiyo
Hata hivyo Ilani hiyo imefafanuwa kuwa kama Mtanzania Bara anaweza kumiliki ardhi Zanzibar vile vile Mzanzibari ana haki ya kumiliki ardhi Tanzania Bara.
“Hii inaitwa usawa kwa jamii yote ya Watanzania, kwa kuwa Serikali ni ya Watanzania, kwa ajili ya Watanzania ambayo imewekwa na Watanzania wenyewe.
“Hii inatokana na ukweli kwamba kura hazipigwi na wananchi wa chama kimoja bali Watanzania wote, hivyo Serikali haiwezi kuwa ya chama kimoja (Tawala)! Bali kilichoshinda ni Ilani ya Uchaguzi wa Chama husika na Kiongozi aliyeinadi, hivyo Sera za Chama kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ndiyo zitakazotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano”imefafanuwa Ilani hiyo
Ilani hiyo imebainisha kuwa kwa mantiki hiyo Chama Tawala hawana hati miliki ya nchi kwa kujimilikisha Serikali na kuifanya ni yao peke yao, na kuwaacha Watanzania wengine wote nje ya Serikali yao eti kwa kuwa si Makada wa Chama Tawala.
“Hali hiyo ndiyo iliyokifanya Chama cha ADA-TADEA kuandaa Ilani hii ya Uchaguzi ya mwaka 2025 kwa kuleta Mapinduzi ya Njano ambayo maana yake ni Mabadiliko ya Mtazamo, Mabadiliko ya Teknolojia na Mabadiliko ya Uchumi. “Kwa upande wa “Watumishi wa Umma tutazingatia kuwapa ajira Vijana wapate uzoefu na uwezo kwenye majukumu husika, Vijana watapewa fursa ya kwanza ili wapate uzoefu kutoka kwa wakongwe katika masuala mtambuka.”imeeleza Ilani hiyo
Kwa upande wake Mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Georges Busungu amesema Ilani hiyo inachagiza ujenzi wa Taifa la Kijamaa analolitegemea kama ilivyokuwa azima ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Aman Abeid Karume Kiongozi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar
“Lengo kuu ni kuimairisha Uchumi,Uzalendo na Utaifa kwa kuiweka Tanzania kwanza kwenye fikra zetu,hali hiyo itaifanya Tanzania kuwa mpya ,kiasi ambacho watanzania wote bila ubaguzi watashiriki maendeleo yao ya Taifa .
“Ninataka Tanzania ambayo itakuwa na utajiri,haki na amaniwa kufanya mambo yake kwa kujiamini na uzingatifu wa Uhuru na Uwajibikaji wa kila mtu”amesema Bussungu
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Salehe Msumari ameelezea ilani yao kuwa ni bora kuliko za vyama vingine na kwamba ADA-TADEA kimekuwa na kuendeela kupanuka kutokana na hamu ya wananchi kujikomboa kutoka kwenye uchumi hodhi,utumwa wa fikra za ukoloni mambo leo na nguvu ya ubeberu
“Chama hiki kiliundwa kwa lengo la kuleta mabadiliko kawa amani ya kisiasa nchini Tanzania yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tanzania African National Union (TANU) na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa awamu ya kwanza Hayati Oscar Salathiel Kambona(1925-1997)”amesema Msumari


Discussion about this post