NA MWANDISHI WETU
KAHAWA inayozalishwa Tanzania imeibuka na kupata nafasi ya kwanza kwenye maonyesho ya 22 ya Chama cha Kahawa Nzuri za Afrika (AFCA) 2026, na ya nne duniani kwa kuzalisha kahawa iliyothibitishwa ubora wa juu na endelevu kwa mazingira.
Kahawa inatajwa kuwa moja ya kichocheo cha watu kuishi muda mrefu zaidi duniani ikiwa watakuwa na utamaduni wa kuinywa ikiwemo pia husaidia punguza uzito na kuimarisha uwezo wa kufikiri.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali ya Awamu ta Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuimarisha na kuliongezea thamani zao la Kahawa kama moja ya mazao ya kimkakati ambapo wakulima wamekuwa wakipata pembejeo kwa wakati na kutatua matatizo yao ili waweze kuzalisha kwa ubora na viwango vya kimataifa.
Hata hivyo Umoja wa Afrika tayari umelifanya zao la Kahawa kuwa moja ya zao la kimkakati ambapo kwa Tanzania linalimwa katika mikoa 17 ikiwemo Kagera na Kilimanjaro.
Ubora huo umejulikana katika Ripoti ya Soko la Kahawa la Kimataifa (ICE), iliyowasilishwa na mtaalamu wa masoko duniani,Judith Garnes,aliyoiwasilisha katika Mkutano wa Kahawa uliofanyika kuanzia Februari 4 hadi 6, 2026. jijini Addis Ababa, Mji Mkuu wa Ethiopia.
Garnes amesema kuwa Kahawa inayozalishwa Tanzania inachukua nafasi ya kwanza barani Afrika na ya nne duniani kwa ubora ambao hauhusiani na uharibifu wa mazingira.
Mafanikio hayo yanaonyesha juhudi zilizowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa kila mkulima anazalisha kahawa bora kuanzia kupanda hadi kuvuna.
Hata hivyo Rais Dkt.Samia hakukosea kumteua Prof.Aurelia Kamuzora kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ambaye kiasili ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ambao moja ya utamaduni wao ni kumkarimu mgeni anayewatembelea nyumbani kwa kumpatia Kahawa iliyokaangwa ili aitafune wakati wa maongezi.
Vyombo vya habari vya kimataifa vimemnukuu pia Mkurugenzi wa Masoko na Ubora wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB),Frank Nyarusi, ambaye amethibitisha juu ya ubora huo.
Awali February 26,2025 katika Mkutano wa Kimataifa wa Kahawa uliofanyika jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Prof.Aurelia Kamuzora amesema wamekuwa pia wakiandaa soko ili kuwepo na wanywahi wengi wa Kahawa ndani ya nchi kutokana na faida ya kunywa Kahawa..
“Kunywa Kahawa ni utamaduni na inahitaji kubadilisha utamaduni wa mahali fulani ili wananchi wajue kwamba ukinywa Kahawa kuna faida ikiwemo kuishi muda mrefu.
“Mzungu akiingia ofisini lazima anywe kikombe cha Kahawa na ndio maana inauzwa huko, Je sisi mtu hajaingia ofisini anaanza kunywa Kahawa?Sisi kwa kutengeneza utamaduni tunaamini watu watakunywa Kahawa”amesema Prof.Kamuzora
Faida nyingine ya Kahawa ni kupunguza uzito,kuamsha ubongo ambayo inafanya binadamu kuendelea kufikiri vizuri zaidi.
Kwa Tanzania zao la Kahawa lilianzia mkoani Kilimanjaro baada ya kuletwa na wakoloni ambapo pia walipiga marufu watu kuinywa ili iweze kusafirishwa nchini kwao kutokana na umuhimu wake kwa afya ya binadamu.




Discussion about this post