NA MWANDISHI WETU,MANYARA
MAZAO ya misitu ni vitu vyote vinavyopatikana kutoka msituni, vikiwa vimegawanyika katika mazao makuu kama mbao, magogo, nguzo na mazao yasiyo ya mbao kama kuni, mkaa, matunda, dawa, asali,pamoja na nyasi ambavyo vyote huchangia zaidi ya asilimia 90 ya nishati ya kaya nchini Tanzania.
Mazao ya Misitu yanatajwa kama chanzo cha chakula, kipato, na malighafi za viwandani katika maeneo mengi nchini na hata nje ya nchi
Hata hivyo kutokana na umuhimu wa mazao ya misitu,Serikali ya Tanzania iliweka Sheria ya Mazao ya Misitu ili kudhibiti matumizi yasiyofaa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Sheria ya Mazao ya Misitu nchini Tanzania inasimamiwa na Sheria ya Misitu Na.14 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake, zikiwemo Kanuni za Usafirishaji za 2023.
Sheria hizi hudhibiti uvunaji, usafirishaji, na uuzaji wa mazao kama mbao, mkaa, na miti ili kuhakikisha uhifadhi, uvunaji endelevu, na ulipaji ushuru wa serikali.
Hata hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaojihusisha na uvunaji wa mazao ya misitu hasa ya asili hali inayosababisha mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa mimea ya asili wakiwemo wanyamapori,wadudu pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Wakati ongezeko hilo likiendelea,Serikali peke yake haiwezi kuzuia kwa asilimia 100 kuvunwa kwa mazao ya misitu hivyo ushirikishwaji wa wadau ni jambo linalosaidia sana kupunguza migogoro kati ya wananchi na Serikali hasa pale nguvu ya dola inapotumika kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wameanza kujipanga kwa kutoa elimu kwa wadau wote wanaojihusisha na mazao ya misitu.
TFS Wilaya ya Kiteto imelenga kutoa mwongozo wa kina kuhusu taratibu sahihi za uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao hayo ili kuimarisha uendelevu na nidhamu ya sekta hiyo.
Mfumo wa kuwakutanisha wadau wa mazao ya misitu ni jambo muhimu katika mustakabali wa kupunguza migogoro katika jamii hivyo kujenga ushirikiano bora utakaowezesha kila mwananchi wa eneo husika kushiriki kulinda urithi huo.
Kikao hicho,kimewakutanisha wafanyabiashara, wakusanyaji na wadau mbalimbali wa mazao ya misitu, ambapo wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia shughuli za mazao ya misitu nchini.

Akizungumza Machi 27,2026 wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara wakati wa kikao kati ya TFS na wadau wa mazao ya misitu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mufandii Msaghaa, amewataka wadau hao kutumia elimu waliyoipata kuendesha biashara zao kwa kuzingatia sheria na kulinda rasilimali za misitu.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu zinafanyika kwa kufuata taratibu zilizowekwa, ili kulinda mazingira na kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha kizazi cha sasa na kijacho,” amebainisha Msaghaa.
Aidha,ameishauri TFS kuendeleza mfumo huo wa kutoa elimu hiyo mara kwa mara kwa wadau ili kuongeza uelewa wa pamoja na kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza katika utekelezaji wa shughuli za misitu.
Kwa upande wake Kamanda wa TFS ambaye ni Mhifadhi Mkuu wa Misitu Wilaya ya Kiteto, PCO John Olomi, amesema TFS itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria na kutoa elimu kwa wadau ili kuhakikisha biashara ya mazao ya misitu inakuwa endelevu na yenye tija.
Olomi amebainisha kuwa ushirikiano kati ya TFS na wadau ni nguzo muhimu katika kulinda misitu na kukuza uchumi wa wananchi kupitia matumizi sahihi ya rasilimali hizo.
“Ni wajibu wetu TFS kutoa elimu kwa wadau na wananchi katika eneo letu kuhusu masuala yote yanayohusu mazao ya misitu kama biashara,usafirishaji,uvunaji na ushirikiano kama huu utatuleta pamoja katika utekelezaji wa kazi zetu kwa amani na kwa upande mwingine tukilinda rasilimali hizi za misitu kwa manufaa ya Tanzania yetu. amesema PCO Olomi

Hata hivyo waadau hao wa mazao ya misitu wameishukuru TFS kwa kuandaa kikao hicho wakisema kimewasaidia kuelewa kwa undani zaidi sheria na taratibu za biashara hiyo, hali itakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa uhalali na ufanisi zaidi.
Wameongeza kuwa elimu hiyo itasaidia kupunguza changamoto walizokuwa wakikutana nazo hususan katika usafirishaji na uuzaji wa mazao ya misitu, huku wakiahidi kushirikiana na serikali katika kulinda rasilimali za misitu na kuendesha biashara endelevu.
Kikao hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Misitu katika Wilaya ya Kiteto, huku kikitarajiwa kuongeza ufanisi, uwazi na uendelevu katika biashara ya mazao ya misitu.
Wilaya ya Kiteto ina Hifadhi ya Msitu wa Emborley-Murtangos wenye ukubwa wa hekta 133,330 ilianzishwa na Vijiji vya Namelok,Kimana,Lengatei,Lotepes,Emart,Ndirgish,Nhati,Engusero,Sidai mwaka 2004 na kusajiliwa rasmi mwaka 2007.




Discussion about this post