NA GOODLUCK HONGO
SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linafafanua kuwa upotevu wa taka zinazooza (ambazo hasa ni mabaki ya vyakula na matunda) ni changamoto kubwa inayosababisha tani bilioni 1.3 za chakula kupotea kila mwaka na kuchangia asilimia 10 ya gesijoto duniani.
Katika jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 60 ya taka zinazozalishwa kila siku ni zile zinazooza na huleta changamoto ya mazingira.
Hata hivyo, kwa mujibu wa FAO taka hizo zinaweza kutumika kama rasilimali muhimu.
Ripoti ya Dar es Salaa Urban Resillience Project (DURP) inaeleza kuwa asilimia 57 ya taka jijini Dar es Salaam huishia mitaani ambapo kati ya tani 5,300 zinazozalishwa kila siku ,tano 1500 pekee ndio zinazofikishwa dampo na kati ya hizo zaidi ya asilimia 60 ni taka zinazooza
Katika maeneo mengi yanakopatikana takaozo huwezi kukosa makundi ya Nzi wakirandaranda juu ya taka hizo na wengine wakiwa wametua wakiendelea na shughuli zao.
Hata hivyo kuna Nzi wa aina nyingi wakiwemo Muscadomestica ambao hawa hupatikana nyumbaji kama ndani lakini pia kuna Nzi aina ya Perryplaneta Americana ambao hawa hupatikana katika taka taka.
Licha ya kuwepo kwa wadudu hawa katika mazingira mbalimbali ya nyumbani na maeneo mengine yanayomzunguka binadamu bado faida zao hazionekani zaidi ya kujulikana kwa jamii kama wadudu wanaosambaza magonjwa na waharibifu wa mazao.
Licha ya wadudu hao kuonekana kwa wingi katika maeneo ya kutupia taka,lakini kumbe wanaweza kuwa na faida kubwa kwa jamii ikiwa watafanyiwa utafiti.
Hata hivyo Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa kwa kuzalisha wanasayansi wake ambapo wamekuwa wakitafiti na kubuni masuluhisho mbalimbali yanayotatua changamoto kubwa katika jamii bila kutegemea watafiti kutoka nje ya nchi.
Moja ya tafiti inayoweza kuleta mabadiliko makubwa na suluhilo la taka zinazooza na kutoka harufu mbaya ni Utafiti wa Mradi wa Ufugaji wa Nzi Chuma
Utafiti huo uliofanywa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar e salaam kupitia Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (UDSM-DUCE)Dkt.Lucas Luchemba umeonesha ni jinsi gani Tafiti na Bunifu za watanzania zinavyoweza kutatua changamoto inayozikabili jamii.

Mradi wa Ufugaji wa Nzi Chuma
Akizungumzia mradi huo mbele ya waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam,Dkt Luchemba anasema lengo kubwa la mradi huo lilikuja baada ya kuona changamoto kubwa ambayo ipo katika mazingira na jamii.
“Changamoto kubwa ambayo ilituchochea au kutushawishi kufanya mradi huu kikubwa zaidi tunaona ni changamoto ya chakula,chakula ambacho tunajaribu kutatua changamoto yake ni protini.
“Tunaona chanzo kikubwa cha protini ni samaki, maharagwe ya soya,na vinginevyo ambayo vitu hivi vina mchango mkubwa sana kwenye mchakato wa kutengeneza vyakula vya wanyama,lakini kwa upande mwingine vinahitajika kwenye vyakula vya binadamu”anasema Dkt.Luchemba
Anasema binadamu anahitaji soya, samaki lakini pia kwenye mchanganyiko wa chakula cha wanyama utaona soya inatumika kwa kiasi kikubwa hivyo waliangalia namna gani wanavyoweza kutoa suluhisho lakini pia wao kama watafiti wanapata manufaa.
Anasema katika utafiti wao waligundua kuwa wadudu wanaoitwa Nzi Chuma wanaweza kutoa funza wake wanaoitwa Black soldier fly lava.
Dkt.Luchemba anasema funza hao kupitia utafiti wanaonesha kwamba wana protini kuanzia asilimia 40 hadi zaidi ya 50 ambapo ni muhimu kwa ajili ya kulisha wanyama,samaki kuku na wengine.
Aidha anaongeza kuwa mazingira yao ya kuwafuga na kuwazalisha,waligundua kuwa ili uweze kuwafuga chakula chao kikubwa ni mabaki ya taka au ya vyakula yaani ni taka zote ambazo zinaweza kuoza (Organic waste),na upande mwingine waliona kwamba wakiweza kupata hizo taka watakuwa na uwezo wa kusuluhisha au kutoa suluhu ya chakula na kwa upande mwingine suluhisho kwenye mazingira.
“Tunaona sehemu za kupeleka kutupia taka (Dampo) kunajaa na yanajaa kwa sababu taka nyingi zinatupwa na ukienda dampo utakuta harufu kali inatoka pale ni kwa sababu ya taka ozo lakini ukikuta kuna taka za kawaida kama majani,makaratasi zote zinaweza kuchomwa moto na zikateketezwa kiurahisi sana.
“Taka ambazo zinaleta shida katika mazingira yetu ni taka ozo , zinazalisha gesi ya ukaa carbondioxide,carbonmonoxide na Methane ambazo gesi hizi zinazungumzwa sana kwenye ulimwengu wa mazingira au zinapigwa vita sana.” anasema Dkt.Luchemba
Anaongeza kuwa asili ya Nzi Chuma wanapatikana kwenye mazingira ya kila siku ya kawaida na tafiti zinaonesha kuwa wadudu hawa ambao wanaruka, kwanza hawali bali wanamirija midogo inayotumika kwa ajili ya kunyonya maji.
Anaeleza kuwa wao wanakunywa maji na wanaweza kuishi siku moja hadi 10 na baada ya hapo wanakufa.
“Hawatagi hovyo haya mayai, haya majike baada ya kujamiina,wao hawana macho wala midomo bali wanahisi kupitia harufu na kisha kutaga kwenye maeneo yenye kificho ambapo baadaye yanageuka na kuwa funza.
“Wakianza kutoka kama funza tunawapa chakula kulingana na ukubwa wao na baada ya siku tatu wanakuwa wakubwa kidogo na ndipo tunawapa chakula kingine ili waendele kukuwa”anabainisha Dkt.Luchemba
Hata hivyo Dkt.Luchemba anafafanuwa kuwa wakiwa funza wanatabia ya kukimbia mwanga na kujificha chini kwa kuwa wanajua wanawindwa na maadui zao kama ndege ambapo kuku pia hufukua chini kwa kuwa wanajua kuna wadudu wanaojificha chini.
“Ukiacha taka nyuma ya nyumba utawakuta funza na wale funza usishangae,ni hao Nzi Chuma wanakuja kutaga mayai na mungu amewaweka kwa ajili ya kutusaidia kusafisha mazingira yetu.
“Kwa mradi wetu huu sisi tunawafuga kwa kutumia net na baadaye wanatusaidia kuchakata taka zetu na moja ya faida tunayopata katika mradi wetu,tunapata moja kwa moja funza wabichi ambao wanaweza kutumika moja kwa moja,lakini tunawakausha ili tuweze kuwahifadhi kwa muda mrefu kulingana na mahitaji ya soko.”aanafafanuwa Dkt.Luchemba
Dkt.Luchemba anabainisha kuwa kuna kuku wa nyama na wa mayai ambapo kuku wa nyama anahitaji protini lakini pia mafuta na kuku wa mayai anahitaji protini nyingi lakini haitaji mafuta.
Anaeleza kuwa wao wanawarahisishia wateja kwa kuwakausha funza hao na kiasi wanawakamamua na kupata mafuta kama yale ya alizeti.
“Tafiti zimefanyika na zimeonesha kuwa mafuta ya funza hao yanamatumizi kwenye biodiesel na kingine watengeneza vipodozi kama sabuni wanayatumia kwa ajili ya kungeneza bidhaa hizo za ngozi.
“Lakini kuna dawa za kusaidia matatizo ya ngozi,lakini pia watafiti wanaendelea na tafiti mbalimbali kuhusu haya mafuta ikiwemo Muhimbili ambao wameshaonesha nia ya kuhitaji haya mafuta kwa ajili ya kuangalia vitu vilivyomo kwenye ndani yake ili kufanya matibabu mbalimbali”anasema Dkt.Luchemba

LENGO LA UTAFITI
Akizungumzia kuhusu lengo la utafiti wao,Dkt Luchemba anasema wao kama watafiti lengo lao kubwa ni kuangalia changamoto kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikiwa kama watafiti kuwa tafiti zinaishia kwenye makabati na hazionekani kwenye mazingira ya kawaida.
“Huku watu wanalalamika kuwa wanachangamoto nyingi ambazo zinawazunguka lakini wakirudi kwa watafiti hazionekani watu wanatulalamiki,sasa sisi tumejaribu kuona kwamba tafiti zipi ambazo zinakwenda kugusa jamii moja kwa moja kwa jamii ambayo inatuzunguka.
“Hii ni moja ya tafiti ambayo tunaona moja kwa moja inagusa jamii kwa sababu tukizalisha hawa wadudu tunawapeleka kwenye michakato kwani hawa wadudu ukiwavuna katika hatua wakiwa funza basi wana protini nyingi sana na unaweza kuwalisha kuku wako moja kwa moja au kama unahitaji kuwavuna na kuwahifadhi basi unawakausha na mwisho unaweza kuwasaga kwa ajili ya chakula cha kuku,samaki au wanyama wowote wanaohitaji protini kama nguruwe,mbuzi na wengine wakiwemo mbwa wa kufugwa”anasema Dkt.Luchemba
Aidha anabainisha kuwa funza hao ni chanzo kikubwa sana cha protini ambao kwa wao kama watafiti wameshafanya utafiti kuangalia kiwango cha protini.
Anaongeza kuwa wao kama watafiti pia wanaangalia ni bidhaa ipi sasa wanaipeleka sokoni ambapo kwa sasa wameshaanza kutengeneza bidhaa ya chakula cha samaki na kuku
“Tunachukua mahindi,pumba na ili mchanganyiko huo uweze kukamilika ni lazima uwe na protini,sasa sisi protini tunaitoa wapi,badala ya kutumia soya au samaki kama ambavyo wengine wanatumia,sisi tunatumia wadudu wetu ambao ni Nzi Chuma.
“Tunawazalisha kwa gharama ndogo kwa kutumia taka lakini ukilinganisha bei ya kilo moja ya hawa wadudu na bei ya soya utagundua kwamba kilo moja ya soya ni gharama sana kuliko kilo moja ya hawa wadudu.
“Ukilinganisha protini inayopatika kwa wadudu wetu na ile inayopatikana katika vyanzo vingine utaona kuwa protini ambayo inapatikana kwa wadudu wetu ni kiasi kikubwa sana”anabainisha Dkt.Luchemba

Dkt.Luchemba anaeleza kuwa wao kwa sasa wapo katika hatua ya kutengeneza chakula kinachotokana na hao wadudu ambapo jambo muhimu kwenye chakula ni protini.
Akizungumzia kuhusu malengo yao,Dkt.Luchemba anasema wakiweza kupata eneo na mipango yao yote ikaenda vizuri basi wanatarajia angalau kwa kile mwezi kuzalisha tani 10 za hao wadudu hao.
Mbali na hilo lakini pia wataweza kufikia masoko ya wafugaji na wafanyabishara mbalimbali wakiwemo wadau wa mazingira ambao wataunga mkono mradi huo na kutoa ahueni kwenye mazingira na kuwaomba wawashike mkono.

FAIDA YA MRADI
Akizungumzia faida za mradi huo muhimu kwa uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,Dkt.Luchemba anasema suluhisho lao lina faida mbili ambapo mosi wanatoa suluhisho la chakula na la pili wanatatua shida ya mazingira.
Anasema wanakusanya taka kutoka katika mgahawa wa chuo chao na mazingira yote yanayozunguka chuo wakiwemo wauza matunda,mamalishe na hata wauza chipsi ambao nao wanaweka maganda waliyomenya viazi ambapo huwapatia vyombo ili waweze kuweka mabaki ya vyakula hivyo.
Anaongeza kuwa taka zote hizo ni chakula cha wadudu wao na baada ya kuzikusanya na kuzichakata wanawapatia wadudu hao ambao wameshawakuza katika hatua ya funza baada ya kutoka katika hatua ya mayai.
Mbolea isiyo na kemikali na yenye virutubisho asilia
Aidha Dkt Luchemba anaongeza kuwa ule mchakato wa kuchakata zile taka kwa kuwa wanakula na kuzibadilisha kutokana na taka kuwa mbolea.
“Wakati sisi tunawavuna wale funza mabaki yote yanakuwa ni mbolea na ile mbolea faida yake moja kubwa sana inavirutubisho vingi lakini pia wanatoa kemikali kwani taka zingine zinazokuja huwa zinakuja na vitu mbalimbali ikiwemo sumu.
“Mungu aliwatengeneza hawa wadudu kwa kuwa wanatoa kemikali ambayo iko katika mfumo wao wa chakula inaitwa antimicrobial peptide jina la kisayansi na kemikali hiyo inachakata zile takataka zikiwa na vimelea vyovyote vibaya na inavunjavunja na hatimaye ile mbolea inakuwa haina chembechembe yoyote ya sumu au vitu mbalimbali.
“Ile mbolea pia inabaki na hiyo kemikali ambayo inasaidia kuongeza rutuba lakini pia inafukuza wadudu ukiitumia kwenye shamba lako”anafafanuwa Dkt.Luchemba

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mbolea hiyo kufukuza wadudu wabaya na kuongeza rutuba katika udongo ,Dkt.Luchemba anaeleza kuwa moja ya tafiti wanayotarajia kufanya ni namna bora ya kuitumia hiyo mbolea.
“Kwa tafiti tulizosoma kwenye machapisho zinaonesha kuwa kuna watu wanachukua kilo moja ya mbolea halafu wanachanganya na lita 20 za maji na kisha wanapulizia kwenye bustani kwa kuwa hawataki mboga za majini zitumie kemikali”anasema Dkt.Luchemba
Bei ya bidhaa
Akizungumzia gharama za manunuzi ya bidhaa wanazozalisha kwa kutumia Nzi Chuma,Dkt.Luchemba anabainisha kuwa kilo moja ya funza hao wanauza kwa Sh.2500 fedha ya Tanzania wakiwa wabichi na wakiwakausha na kuwasaga basi kilo moja huuzwa kwa Sh.5000.
“Kiwango chao cha protini ni maradufu ya kiwango cha protini unachokipata kwenye vyanzo vingine kwani kinafikia asilimia 55 hadi 60,kwenye kilo moja ya funza hawa na unaweza kutumia kilo mbili kwenye vyanzo vingine vya protini”anasema Dkt.Luchemba

Utunzaji wa Mazingira
Akizungumzia kuhusu mazingira na utafiti wao,Dkt.Luchemba anasema wanampango wa kuzalisha wadudu hao kwa kiasi kikubwa kwa lengo la kuwaweka pamoja watu wengi ambao wanazalisha taka ozo ili kuzipatia mbadala .
“Kama unavyoona sasa hivi watu wanaokota chupa za maji,na zinaokotwa kwa sababu zina mbadala wake yaani viwanda ambavyo vinachakata hizo chupa,kwa hiyo na sisi tunatamani sana tuwe na mbadala wa matumizi ya taka ozo yaani ifikie hatua watu wawe wanazileta wao wenyewe badala ya kuzipeleka dampo.
“Watu wawe wanazihifadhi vizuri katika nyumba zao na sisi tukienda na magari yetu na vifaa wakiwa tayari wameshaziandaa vizuri ili tuzalishe hao funza kwa wingi.
“Lengo kubwa ni kwamba tukienda dampo tusisikie harufu na tukute taka zingine ngumu kama makaratasi,na hii itasaidia kuyapatia ahueni dampo zetu kupumua”anaeleza Dkt Luchemba
Dkt.Luchemba anabainisha kuwa Serikali na dunia nzima inahangaika kwa sababu masuluhisho kama haya hayajatiliwa mkazo,hivyo wao wanaonesha mfano lakini zaidi pia wanalenga shamba darasa lao hilo litumike kama mfano.
“Hapa tunawanafunzi wa Shada ya Uzamili na Uzamivu, ambao wanafanya mafunzo yao kwa vitendo kwenye mradi wetu huu na tunaamini kwamba wakishatoka hapa na kwenda kuwa walimu sehemu mbalimbali mikoani wataenda kuendeleza elimu hii ya kutunza mazingira lakini pia namna ya kuzalisha chakula cha wanyama na kuku”anasema Dkt.Luchemba

UTAFITI NA DIRA YA MAENDELEO 2050
Akizungumzia kuhusu utafiti wake na Dira ya Maendeleo 2050,Dkt.Luchemba anabainisha wao kama watafiti wanajua kwamba Serikali imezindua Dira ya Maendeleo 2050 na wanaona kwamba mchango wao mkubwa kwenye mradi wao huo 2050 wanaona ni namna gani watakavyopunguza gharama za chakula cha wanyama kwa kutoa njia mbadala ya kutatua changamoto ya chakula.
Dkt.Luchemba anabainisha kuwa wakishapunguza gharama za chakula basi wafugaji watafuga kwa unafuu lakini kikubwa zaidi namna ambavyo watakavyoweza kuondoa taka ozo kwenye mazingira yao.
“Sisi tunaamini kwamba kutekeleza mradi wetu huu unamchango mkubwa sana katika kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050 na sisi kama watafiti tunaomba tushirikiane na Sekta Binafsi kwani UDSM,COSTECH wameshaonesha juhudi zao.
“Tukipata nafasi kwa kuifanya kwa ukubwa zaidi katika maeneo kama ya dampo tunatarajia tuwe na vijana wasipungua 50 lakini pia tutakuwa na vikundi vya wajasiriamali ambao watakuwa wanakuja kwenye shamba darasa na baada ya miaka mitatu ijayo tuwe tumefikia vikundi zaidi ya 200.
“Na kila kikundi kimoja hakipungua watu 20 hadi 50 ,sasa tukiwa na vikundi vyote kutakuwa na matokeo makubwa sana”anaongeza Dkt.Luchemba
NGUVU YA COSTECH YAONGEZA MAFANIKIO
Akizungumzia wadau waliofanikisha utafiti hadi kutoa matokea hayo,Dkt.Luchemba anabainisha kuwa wao wameanza kwa kusaidiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo pia waliwaruhusu na kuwapa fedha za kujenga banda ndani ya eneo la chuo baada ya kuona manufaa ya mradi huo lakini pia COSTECH nao waliwaona na kuwapatia nafasi ya kujifunza zaidi ya wiki nne.
“Mimi mwenyewe nimehudhuria mafunzo COSTECH na wanaendelea kututembelea na kutusimamia na tunaweza kujivunia kutoka katika mafunzo ya COSTECH tuliweza kufundishwa namna na ya kupitia hatua mbalimbali kwenye miradi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“COSTECH pia walitupatia mafunzo ya namna ya kutunza au kuwa na hati miliki kwa sababu huu ni ujuzi na mtu akisikia anaweza kwenda kutengeneza sasa bahati nzuri siku ya tarehe 14/5/2026 zaidi ya mwezi mmoja uliopita tulianza kuandika Hati Miliki ya wazo letu na tumeshapata cheti kutoka BRELA.
“COSTECH wamekuwa na sisi bega kwa bega na wataendelea kutuunga mkono lakini pia tunaomba sana wadau mbalimbali waweze kutushika mkono ili tuweze kuifikia jamii,lakini pia shamba darasa letu hili tunatarajia kuwaalika wajasiriamali wanaojihusisha na mazingira waje kupata mafunzo haya”anaseleza Dkt.Luchemba.
Anasema wao ni taasisi ya elimu wanatamani kuweka kama mfano kwani kwa sasa kuna wanafunzi wanaotarajiwa kuingia mwaka wa kwanza hivyo wanataka kuhakikisha kuwa wanaanza kujishikiza katika mradi huo.
“Lakini pia kuna mpango wa kufungua shamba darasa la kulima mbogamboga na pia kufuga kuku,kutakuwa na shughuli mbalimbali zinakuwa zinaendelea hapa lakini lengo kubwa ni kuona namna gani matokeo ya tafiti ambazo tunazifanya kila siku zinavyokwenda kuwagusa wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wanaokuja kujifunza ualimu na pindi wanapoondoka basi wapeleke katika shule zao”anabainisha Dkt.Luchemba

UMUHIMU WA ELIMU YA AMALI
Akizungumzia Sera ya Elimu ya Amali,Dkt.Luchemba anabainisha kuwa sera hiyo wameshaanza kuitekeleza kutoka kujifunza kwa kusoma na kwenda kujifunza kwa vitendo.
“Sasa hivi tumeshatembelewa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mazoezi lakini pia tumewaalika Shule ya Sekondari Cha’ngombe na zingine zinazotuzunguka hapa waje wajifunze hii Elimu ya Amali.
“Hii ni moja ya kitu kikubwa sana kwenye Elimu ya Amali kwani wanafunzi wanapomaliza elimu zao ni ngumu kujua wafanye nini baada ya kupata vitu kama hivi kwani takataka akiiona ataona kama thamani ,ataona hela na ni rahisi kumshawishi mama nyumbani kwamba hizi takataka usizitupe kwenye pipa la uchafu kwa ajili ya kwenda dampo na tutazifanyia uchakataji.
“Hapa tutakuwa tumeelimisha jamii na matokeo yetu ya elimu itakuwa imeonekana moja kwa mja kwenye jamii”anasema Dkt.Luchemba

Wanafunzi walivyonufaika na Elimu ya Amali
Baadhi ya wanafunzi wanaofika kujifunza kwa vitendo juu ya mradi huo wameoneha kurahia kutokana na kwamba mfumo wa uzaloshaji wake unagusa mazingira yao ya kila siku hasa uzalishaji wa taka na ufugaji wa wanyama na ndege katika familia zao.
Mmoja wa wanafunzi wa darasa la tano kutoka Shule ya Msingi Mazoezi Cha’ngombe Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-DUCE) waliofika kujifunza kuhusu mradi huo wa Inzi Chuma Sophia Mohamed anaeleza kuwa mwanzo aliogopa kuwaona wadudu hao.
“Nilichojifunza mimi,hizi taka tunazozitupa zitatusaidia katika maendeleo yetu ya mazingira na ndio usalama wetu, tusitupe taka hizi kwenye mazingira yetu,tunatakiwa tuziweka vizuri.
“Nimewapenda baada ya kusikia hawana madhara wala kuleta magonjwa,tunatengeza mafuta kwa ajili ya wagonjwa wa ngozi,tunatengeneza mbolea lakini mimi nilitamani mafuta”anasema Mohamed
Kwa upande wake Mwanafunzi Fahad Juma wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mazoezi Cha’ngombe iliyopo ndani ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-DUCE) anasema katika mradi huo amejifunza namna ya kutunza chakula,uchafu na mazingira.
“Mabaki ya chakula yatatusaidia katika uzalishaji wa kitu kingine na gari la taka likija nitawapa taka ngumu na wakiniuliza kuhusu taka laini nitawapa elimu ya namna nilivyojifunza.
“Hawa wadudu mara ya kwanza kufika hapa niliwaogopa ila kadri muda ulivyozidi kwenda nikatambua hawana madhara yoyote na wanafaa kufugwa sehemu yoyote lakini kuna masharti yao unatakiwa kufuata na watakupatia fedha na kusafisha mazingira”anasema Juma
Juma anasema elimu aliyoipata ni kuwa wadudu hao wakikaushwa wanazalisha mbolea na funza wake wanaasili ya mafuta na mafuta yake wanatibu magonjwa ya ngozi ambapo wanasayansi waligundua.
WADAU WANAPASWA KUCHANGIA
Akizungumzia gharama za uendelezaji wa miradi hiyo,Dkt.Luchemba anasema kufanya mradi kama huo wanaoufanya wao inahitaji kuwa na eneo kubwa zaidi kwani kwa sasa eneo wanalofanyia ni dogo.
“Tunahitaji kwenda pembeni ya dampo kwa sababu ukikusanya taka nyingi eneo hili la chuo zitatoa harufu hivyo tukipata sehemu ya dampo hakuna mtu atapiga kelele kwamba una mletea harufu kwa kuwa sehemu ya dampo ina harufu pia.
“Tunahitaji pia kuwa na magari ya usafiri kwa ajili ya kuchukua taka ozo na kupeleka eneo lao,pia tunahitaji mashine za kufanyia uchakataji ili taka zinapokuja zichakatwe/zivunjwevunjwe ili hawa wadudu waweze kula kiurahisi zaidi,kwa kuwa tutakuwa tunazalisha kwa wingi tunahitaji mashine za kukausha wale wadudu
“Tunahitaji pia rasilimali fedha kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya majengo kwa ajili ya kutunzia taka lakini pia kwa ajili ya kuzalisha wale wadudu”anafafanuwa Dkt.Luchemba




Discussion about this post