• About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact
Monday, May 25, 2026
  • Login
Bajeti
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
Bajeti
No Result
View All Result
Home Mazingira

Bodi ya Maji Bonde la Pangani(PBWB) na mikakati ya kulinda,kuhifadhi vyanzo vya maji,yaonya watumiaji wasiona na vibali

Yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapatia mabilioni ya fedha za miradi

by bajeti
April 10, 2026
in Mazingira
0
Bodi ya Maji Bonde la Pangani(PBWB) na mikakati ya kulinda,kuhifadhi vyanzo vya maji,yaonya watumiaji wasiona na  vibali

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB)Segule Segule

Share on FacebookShare on Twitter

NA GOODLUCK HONGO

KATIBU  Mkuu  wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amewahi kusema kuwa   Maji ni kama damu ya Maisha ya dunia, kwani hutumika kuanzia katika suala la afya na lishe, hadi elimu na miundombinu.

Maji yanatajwa kuwa ni  rasilimali  ya kwanza duniani kutumika ikifuatiwa na mchanga ambapo maji yanatajwa kuwa ni muhimu katika kila nyanja ya mwanadamu kuishi na ustawi wake lakini pia yanachangia pakubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kushamiri kwa kila taifa.

Hata hivyo UN inasema kuwa watu wanaoishi mijini wanatarajiwa kuwa kwenye mgogoro wa kukosa maji na utaongezeka mara mbili kutoka watu milioni 930 mwaka 2016 hadi kufikia watu kati ya bilioni 1.7 na bilioni 2.4 mwaka 2050.”

Kauli ya UN  kwa mataifa mbalimbali duniani imelenga kuhimiza kuchukuliwa kwa hatua madhubuti ili kuilinda dunia dhidi ya migogoro inayosababishwa na uhaba mkubwa wa maji ambao wakati mwingine husababishwa na Vita,Ukame wa muda mrefu,uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.

Katika miji na majiji mengi duniani bado upatikanaji wa maji safi na salama ni changamato kubwa ikiwemo upotevu wa rasilimali hiyo inayopotelea njiani kutokana na uchakavu wa mabomba ya kusafirishia.

Hata hivyo Tanzania inaelezwa  kuwa  na lita za ujazo wa maji unaofikia Bilioni 126 ambapo kati ya hizo Bilioni 105 ni Maji  yaliyo juu ya ardhi na Bilioni 21 ni Maji yaliyo chini ya ardhi

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 nchini Tanzania inalenga kuwa na Taifa lenye uhakika na usalama wa maji kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kudumisha na kuendeleza ekolojia pamoja na kuwa na taifa lenye mfumo imara na shirikishi wa usimamizi wa ardhi oevu na rasilimali nyinginezo.

Ilani  ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ikiwa na kauli mbiu “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”  ambapo katika ahadi na Maelekezo yake (2025 – 2030)  imefafanuwa kuwa  Serikali ya CCM  itaimarisha upatikanaji wa Maji kwa Wananchi wote.

Hata hivyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inayotembea inalindwa,kutunzwa,kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kutokana na rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu,Serikali iliamua kuweka mfumo maalum wa kulinda na kuhifadhi maji yaliyo chini ya ardhi na juu ya ardhi.

Moja ya mifumo iliyowekwa na Serikali katika kulinda na kuhifadhi maji ni pamoja na uanzishwaji wa Mabonde ambapo hadi sasa yameshafika tisa.

Moja ya mabonde hayo ni Bonde la Pangani linalosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la  Pangani (PBWB) ambayo makao makuu yake yako Moshi mkoani Kilimanjaro ilianzishwa rasmi Julai 1991 ikiwa inahusisha  eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 58,400 ambapo kilomita 54,600 sawa na asilimia 93 zikiwa Tanzania na kilomita 3,800 sawa na asilimia saba  zikiwa eneo la Kenya.

Bonde hili linahudumia watu zaidi ya miliomi 4.7 hasa katika majiji ya Arusha na Tanga  pamoja na Moshi mkoani Kilimanjaro na sehemu ya Mkoa wa Manyara.

Mbali na kupita katika mikoa minne lakini pia linapita katika wilaya zaidi ya 20 ikiwemo Arusha,Jiji la Arusha,Arumeru(Meru),Simanjiro,Siha,Hai,Moshi Mjini na Moshi Vijijini,Rombo,Mwanga,Same,Korogwe,Korogwe Mjini,Pangani,Jiji la Tanga,Mkinga,Muheza,Handeni,Handeni Mjini,Kilindi ikiwemo na Lushoto

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB)Segule Segule akizungumza katika moja ya mikutano ya kuhimiza utunzaji wa vyanzo vya maji

Akizungumza na Bajeti Communication mwishoni mwa wiki,Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maji  Bonde la Pangani (PBWB)Segule Segule anasema Maji ni rasilimali muhimu ya Taifa kama zilivyo rasilimali zingine ikiwemo Misitu,Ardhi na Madini ambapo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinasimamiwa na Mheshimiwa Rais na amekasimu madaraka yake kwenye taasisi mbalimbali ambazo amezipa kusimamia

Anasema kwa upande wa usimamizi wa rasilimali za Maji zinafanywa na Wizara ya Maji  chini ya taasisi zao za Bodi ya Maji na Mabonde.

Akizungumzia uanzishwaji wa mabonde,Segule anasema tamko la kisheria la kuanzishwa kwa Taasisi hizi za Mabonde ya Maji lilianzishwa mwaka 1981 hivyo sio Taasisi za leo ambapo wakati huo iliundwa kupitia Sheria ya Taasisi za Maji ya mwaka 1974.

Segule anaeleza kuwa Sheria hiyo ilifutwa rasmi mwaka 2009 na ndio  maana mabonde yanafanya kazi kupitia Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya Mwaka 2009 pamoja na Maboresho Na.8 ya Mwaka 2022 lakini uundwaji wake ilitokana na sheria ya zamani.

“Bonde la kwanza kuundwa kwa majaribio liliundwa mwaka 1991, na Pangani ndio Bonde la kwanza kuundwa  lakini baadaye tukapata Bonde la Mto Rufiji mwaka 1993 na mengine yote yaliundwa kati ya mwaka 2000 na 2004″anaongeza Segule

Maji yakitiririka katika moja ya vyanzo vya Bonde la Pangani

Kazi za mabonde

Kazi kubwa ya Mabonde ni kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali maji(Matumizi Endelevu) ambapo kupitia Wizara ya Maji inafanya maji hayo yaweze kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kazi ya pili ya Wizara ni kuyapeleka maji hayo  kuyatumia kutoa huduma kwa wananchi za Maji Safi na Salama ambapo jukumu hilo la kwanza la kuyafanya maji yawe endelevu ndio inafanywa na Mabonde na jukumu la pili la kusambaza Maji Safi na Salama inafanywa na Taasisi mbili za Mamlaka za Maji zinazohudumia maeneo ya mijini  na ya pili ni RUWASA iliyoundwa mwaka 2019 ambayo inahusika na utoaji wa huduma kama hiyo lakini Vijijini.

Mashine ikifukua mito iliyoziba na mchanga katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha ikiwa ni moja ya miradi ya PBWB

“Mabonde yako tisa na mifumo mikuu ya  maji iliyopo nchini iko 10 kwa kuwa unapozungumzia Bonde ni kubwa na ndani yake kuna vibonde vidogo vidogo vinavyounda Bonde moja.

“Dhana halisi ni kwamba Maji ni Rasilimali inayotembea tofauti na madini ambayo unaweza kuifanyia mpango hapo hapo na utaikuta hapo hapo kama ilivyo rasilimali ya ardhi ambayo imeiumbwa katika uso wa dunia na utaikuta hapo hapo.

“Lakini Rasilimali Maji inatabia ya kutembea na kukatisha katika maeneo ya Vijiji,Tarafa,Kata,Wilaya,mikoa,Kanda na hata Nchi na Nchi na haihusiki na mipaka ya kiutawala tunayoitengeneza.”anasema Segule

Segule anafafanuwa kuwa ukisimamia  maji kwa mipaka ya mikoa ,shida inayopatikana ni kuwa inahitajika kutoa maelekezo wakati vyanzo vile vya maji vipo katika mkoa mwingine na matumizi yako kwenye mkoa mwingine.

“Mfano maji yanayolisha Jiji la Dar es Salaam yanatoka Ruvu na Mto Ruvu unatokea Mkoa wa Morogoro na unakatisha Mkoa wa Pwani lakini wanufaika wakuu ni Dar es Salaam lakini huu mto wote upo kwenye Bonde moja la Wami-Ruvu.”anasema Segule

Segule anabainisha sababu za  mabonde kuwa tisa lakini mifumo iko 10 kutokana na Bonde moja la Wami-Ruvu kusimamia mifumo miwili kwa pamoja ambao ni mfumo wa Mto Wami na mfumo wa Mto Ruvu na hiyo ndio sababu ya kuitwa Bonde la Wami-Ruvu.

Akizungumzia kuhusu mipaka ya Mabonde,Segule anabainisha kuwa mipaka ya mabonde imetengenezwa kwa kufuata mipaka ya maji  na sio ya kiutawala.

Anaongeza kuwa mabonde yote ya maji yanapewa majina yanayotokana na chanzo kikuu cha maji katika eneo husika ambapo hapo inaweza kuwa Mto au Ziwa na ndio maana kuna Bonde la Mto Pangani,Bonde la Mto Rufiji,Bonde la Wami-Ruvu ,Bonde la Ruvuma linalotokana na Mto Ruvuma,Bonde la Ziwa Victoria linalotokana na Ziwa Victoria.

“Bonde la Ziwa Nyasa linatokana na Ziwa Nyasa na Bonde la Ziwa Tanganyika linalotokana na Ziwa Tanganyika.

“Mipaka ya mabonde ni lile eneo lote ambalo maji yake ya mvua yanapeleka kwenye hicho chanzo husika hata kama eneo hilo lipo kilomita 500 kutoka katika chanzo hicho cha maji.

“Mvua ikinyesha basi maji hayo hutembea taratibu na kuingia katika eneo hilo na hapo ndipo linaitwa Bonde hivyo ni kama kidakio cha maji.”anasema Segule

Akitolea mfano wa Bonde la Pangani,Segule anabainisha kuwa linalichukua sehemu ya Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Manyara na  Tanga,hivyo mkoa mmoja  unaweza kuwa umegawanywa katika mabonde tofauti.

“Mfano Bonde la Rufiji linapita katika mikoa karibu saba hivyo baadhi ya mikoa imekata eneo kwa ajili ya Bonde na sababu ya mfumo huo ni kutokana na tabia ya maji kutembea na kuwa katika mfumo mkubwa mmoja, hivyo mkoa ni sehemu tu ya huo mfumo na tungesimamia kwa kufuata mikoa,wilaya usimamizi wake usingekuwa sahihi.

“Maji yanayotoka katika eneo moja yanawanufaisha watu walio mbali zaidi na eneo lingine”anasema Segule

Anasema Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Pangani hufanyika kwa kuzingatia mfumo shirikishi unaotoa fursa kwa jamii katika kupanga na kusimamia matumizi ya maji kama ulivyoainishwa katika mageuzi makubwa ya Sekta ya Maji yaliyofanyika kupitia Sera ya Maji ya Mwaka 2002.

 

Mashine ikitekeleza kazi za miradi ya PBWB ya ufukuaji mito

UGAWAJI WA MAJI

Akizungumzia kuhusu ugawaji wa maji wa Bonde la Pangani,Segule anasema maji yanatoka katika vyanzo kama Mto,Bwawa,Chemchem na Ziwa ambayo wakati mwingine hutengeneza mito ambayo hutokea katika maeneo mbalimbali.

Anasema kwa kuwa maji ni rasilimali inayotembea basi huko yanakopita kuna watu wanaona ni fursa kuyatumia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Sasa kila mtu akiona  anajifikiria mwenyewe au yule ambaye chemchem imetokea kwake au katika kijiji chake na akajimilikisha haitakuwa rahisi kuyasimmamia.

“Ndio maana sasa sisi ndio tunaitwa waratibu wa watumiaji maji wote na tunawaratibu kwa kuwapa vibali na kila anayetaka kuyatumia maji kutoka kwenye chanzo ni lazima aombe kibali.

“Kama unatumia maji juu ya ardhi au chini ya ardhi lazima upate kibali,kwani sisi maji yetu tumeyagawa katika makundi mawili yaani juu ya ardhi na chini ya ardhi.”anabainisha Segule

Anasema maji ya chini ya ardhi ndio wanayoyapata kwa kutumia visima na maji ya juu ya ardhi ndio hayo yanayopatikana moja kwa moja kutoka katika vyanzo vya maji hivyo maeneo yote hayo ni lazima upate kibali kutoka katika Bonde husika.

Anaeleza kuwa wanatoa vibali kwa watu wa Umwagiliaji,Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa ajili ya kuzalisha umeme kwani utaratibu unawataka kuomba kibali katika Bonde husika,mfano TANESCO wameomba kibali cha kutumia maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Moja ya miradi inayosimamiwa na PBWB ya ufukuaji mito mkoani Arusha ambayo ilipoteza njia yake ya asili na kusababisha mafuriko kwa wananchi

“TANESCO yake ni miundombinu lakini yale maji ni lazima aombe kibali lakini pia tuna mradi mkubwa wa Same-Mwanga-Korogwe ambao ni mradi wetu wa Wizara ya Maji na kabla ya mambo mengine walitutaka sisi tufanye tathmini ikiwemo mradi huo kuwa endelevu na tulitoa kibali pale cha kutumia maji lita 750 kwa sekunde.

“Kila anayechukua maji moja kwa moja kutoka kwenye chanzo anawajibu wa kuomba kibali kutoka katika Bonde husika.

“Ukiona mto unapita kwako na unataka kuweka mashine ya kuvuta maji ili utumie katika bustani,ilimradi tu unaweka  miundombinu ya kuvuta maji kutoka  kwenye hicho chanzo unatakiwa ujisalimishe kwanza kwenye Ofisi za Bonde husika ili upewe kibali.”anafafanuwa Segule

Segule anaongeza kuwa utaratibu wa kuomba vibali sio mgumu kwani siku hizi kuna njia nyingi ikiwemo mitandao ambapo hakuna haja ya kuonana uso kwa uso,hivyo unaweza kuomba kibali uko ulipo.

Aidha anafafanuwa kuwa kabla  ya kutoa kibali ni lazima wataalamu wao wafike eneo husika na wajiridhishe na kufanya vipimo juu ya uhai wa hayo maji ili unapopewa kibali kutumia maji hayo hautaathiri watumiaji wengine ambao wameshapewa vibali.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB)Segule Segule

“Tunapaswa kuwalinda,mfano mtu anayetaka kibali kutoka Mto Pangani ambao unapita Same,Mwanga,Korogwe,Muheza  na Pangani hadi kuingia Bahari ya Hindi,na hapo mtu anaweza kuwa yuko Muheza ana akaomba kibali cha miaka 10 na kuanzisha shamba lake sasa leo na wewe uko eneo la Same na unaomba kibali cha kutumia maji hayo  hayo ni lazima tuhakikishe maji utakayopatiwa wewe hayaweza kumuathiri yule wa Muheza.

“Sasa hii ni pamoja na miradi ya Serikali na wawekezaji kwani wako watu pia wenye viwanda ambao wanatumia maji moja kwa moja au kwenye vyanzo husika,hivyo tunafanya ugawaji wa maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa mfumo wa utoaji wa vibali.

“Sasa lazima tujiridhishe kwani unaweza kuathiri maji ya kunywa,hivyo kabla hatujampa kibali tunakuwa tumeshafanya tathmini ya kina hali ya maji na haki za wadau wengine walioomba vibali kabla ya mhusika”anabainisha Segule

Akizungumzia kuhusu watu wanaochimba visima,Segule anabainisha kuwa sehemu kubwa ya maji yao yanapatikana kutokana na mvua ambapo baada ya kunyesha maji yanatiririkia kwenda baharini moja kwa moja ambayo hayo wanakuwa wameshayapoteza kwani yakishaingia baharini hakuna njia ya kurudisha ili yatumike tena.

“Lakini kuna maji yanaingia chini ya ardhi ambayo hayo ndio yanaitwa hifadhi ya maji chini ya ardhi ambayo yanakaa katika miamba lakini sio miamba yote  inauwezo wa kuhifadhi maji.

“ Maji yote ya Tanzania ni lita za ujazo  Bilioni 126,ambapo Bilioni 105 ni maji juu ya Ardhi na Bilioni 21 ni maji chini ya ardhi na kati ya hizo Bilioni nane zipo katika Bonde la Pangani na kati ya hizo Bilioni 7.4 ndio maji juu ya ardhi  na Bilioni 0.6 ni maji chini ya ardhi.”anaongeza Segule

PBWB pia huhamasisha wananchi kupanda miti katika vyanzo vya maji ili kuvilinda na mabadiliko ya tabianchi

Hata hivyo Seguye ameongeza  kuwa maji hayo hayajasambaa kila mahali na kuna sehemu nyingine hayana maji na kuna maeneo mengine yana maji mengi kuliko maeneo mengine na takwimu hizo wanazipata kupitia kazi ya kwanza ya ukusanyaji takwimu.

Ujenzi wa bwawa la maji mkoani Manyara uliotekelezwa na PBWB

 

UTHIBITI UBORA WA MAJI

Akizungumzia watu wenye nia ya kuchimba visima ili kupata maji ya chini ya ardhi, Segule anabainisha kuwa ukishawataarifu nia yako ya kuchimba kisima basi kitu cha kwamba utatakiwa kutafuta mtafiti aliyesajiliwa na Serikali ili akushauri uchimbe cha urefu wa kiasi gani, na watafiti hao wanapatikana pia katika kila Ofisi ya Bonde ambapo kuna wataalamu wa miamba ambao wanaweza kukusaidia kwa gharama za kiserikali

PBWB wakiendelea na upimaji wa mtiririko na kiasi cha  maji

Aidha Segule anaongeza kuwa Serikali imetoa ruhusa kwa watafiti binafsi ambapo kabla ya kupewa kibali,Bonde husika linakuwa limeshawakagua na kujua utaalamu wao  na mitambo wanayotumia.

“Kwa mfano,Bonde la Mto Pangani gharama za utafiti ni Sh.Milioni 1.5 kwa maana ya Moshi Arusha na Tanga lakini ukienda nje ya majiji itaongezekana kidogo kulingana na umbali wa eneo husika.

“Hadi sasa tumeshatoa vibali zaidi ya 1200 vya uchimbaji maji chini ya ardhi na mwaka huu wa 2026 hadi sasa tumeshatoa vibali zaidi ya 70.

“Si kila anayeomba anapaswa kupewa kibali kwani tunajiridhisha pia na vigezo vingine ikiwemo kujua anayekuchimbia kama vifaa vyake vinakidhi vigezo katika eneo husika na sio kwamba mashine inachimba kila mahali”anabainisha Segule

Hata hivyo amefafakuwa kuwa ikiwa watamkama mtu anayeshimba kisima bila kibali,sheria imewapa mambo mawili,moja ni kumlipisha faini ya papo kwa papo ambapo hapo tunahesabu idadi ya makosa lakini hilo akiona haridhiki nalo basi tunamfungulia mashitaka na tunampeleka mahakamani.

PBWB wakipima maji yaliyo chini ya ardhi kabla ya kutoa vibali kwa waombaji

“Maji chini ya ardhi yakichafuka huwezi kuyaona na sisi tumeshakuwa na imani kwamba maji ya chini ya ardhi ndio masafi na unaweza kuyachukua moja kwa moja ukayatumia.

“Sasa kuna uwezekano mkubwa ikiwa mtu atayaathiri tutaathirika watu wengi kwa muda mrefu kabla ya kubainika”anasema Segule

Akizungumzia kuhusu watu wanaojichimbia visima mitaani bila kutumia mashine,Segule anabainisha kuwa hao ni wahalifu kama wahalifu wengine na watawashughulikia  kama wahalifu.

Bwawa likiwa limejaa maji baada ya kukamilika ikiwa ni9 moja ya miradi iliyotekelezwa na PBWB mkoani Manyara

UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Akizungumzia kuhusu utunzani wa vyanzo vya maji,Segule anasema  licha ya  kugawa maji na kutoa vibali lakini pia ni wana jukumu la kutunza vyazo vya maji yanapotoka ambapo hilo ni jukumu lao la msingi sana ambapo kwa sehemu kubwa wao ni kama waratibu tu lakini jukumu la utunzaji ni la kila mwananchi.

Aidha Segule anaongeza kuwa hata kauli mbiu yetu inasema “Utunzaji wa Vyanzo vya Maji,Ni jukumu letu sote”kila mwananchi pale alipo akiona eneo ambalo linaitwa chanzo cha maji aidha ikiwa ni Bwawa,Mto,Ziwa,Chemchem au Mwamba unaowapatia maji kupitia uchimbaji wa visima basi wanapaswa kuzingatia taratibu ili kutunza hayo maeneo yaweze kutuhudumia vizazi vya sasa na vijavyo.

PBWB pia huweka mipaka uzuia wananchi kuingilia maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji

“Wananchi wasilime au kufanya shughuli zozote ndani ya mita 60,moja ya shughuli tunazozifanya katika vyanzo vya maji ni pamoja na kuainisha alama au kuweka alama kwenye maeneo ambayo sheria imetaja mita 60 na hizo mita zinaishia wapi basi ni wajibu wetu tunaotekeleza.

Lengo ni kuwaelemisha wananchi wajue mwisho wa eneo ambalo wao wanaweza kufanya shughuli zao za kibinadamu ,lakini walinzi wa haya yote ni mwananchi mwenyewe kwani chanzo cha maji popote kilipo mnufaika wa kwanza ni yeye mwananchi kwenye eneo husika.

“Ni wajibu wa wananchi wote sisi kushirikiana kuhakikisha hivyo vyanzo vya maji vilivyopo kwenye maeneo yetu tunavitunza “Wenzetu wa Maliasili wana kauli mbiu yao wanasema “Tumerithi ,Tuwarithishe”ukiona letu sisi tumevikuta vyanzo vya maji ni kwa sababu walikuwepo watu ambao hawakuviharibu na wapo walioishi kabla yetu katika hii dunia basi na sisi tuvitunze ili manufaa yake yaweze kuwafikia wale ambao watakuja baadaye.”anaeleza Segule

Kazi ya utafiti wa  maji chini ya ardhi  ni moja ya majukumu ya PBWB

UENDELEZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Kwa upande wa Uendelezaji wa Vyanzo vya Maji,Segule anasema hapo hujikita zaidi katika kazi za ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa Mabwawa.

“Hii pia ni sehemu tunayoifanyia kazi na hivi tunavyoongea tumekamilisha ujenzi wa bwawa kwenye katika Kijiji cha Langai wilayani Simanjiro mkoani Manyara

“Bwawa hilo kwa sasa limeshajaa maji na linawanufaisha wananchi wengi ikiwemo wafugaji”anabainisha Segule

Wafanyakazi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani wakiwa katika picha ya pamoja na wandarasi waliokuwa wakitekeleza mradi wa uchimbaji bwawa katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara

Mbali na mradi huo lakini pia tuna mradi wetu wa ukusanyaji wa Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Maji wa kuziboresha mfumo wetu wa ukusanyaji Takwimu ili tuweze kurekodi Takwimu tukiwa hata nyumbani au ofisini

“Tunaishukuru Sana Serikali katika eneo hili imetupa fedha nyingi na hii mifumo itatuwezesha sisi kupata taarifa kwa wakati na kuzichakata ikiwemo kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kwa wakati”anaongeza Segule

Hata hiyo Seguye anabainisha kuwa mbali na miradi hiyo lakini pia mradi mwingine ni wa kufukua mito iliyofukiwa na mchanga ili kuwaepusha watu na madhara ya mafuriko.

“Miradi hii tunaifanya katika Mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro,Arusha pamoja Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru ambapo hapo tulitekeleza mradi kama huo wa kilomita 18 ambao ulisaidia kuwaepusha wananchi wengi na adha ya mafuriko ambao walikuwa wanapata kwa muda wote”anaongeza Segule

Ufukuaji wa mito iliyojaa mchanga ni moja kati ya miradi iliyotekelezwa na PBWB

Hata hivyo kwa sasa kunanyesha mvua nyingi kwa wakati mmoja ambapo zinaleta athari ikiwemo baadhi ya miundombinu yetu ya vipimo vya maji NA vile vya kubebea maji kuelekea katika mito mikuu

Segule anabainisha kuwa Serikali imeendelea kuwekeza fedha ambapo kwa sasa wanafanya kazi ya ukusanyaji wa taarifa lakini pia wamejipanga pindi mvua hizi za sasa  zitakapoisha wanakwenda kukarabati maeneo mbalimbali yaliyoharibiwa na mvua.

Bango la katazo la shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya mita 60 ya chanzo cha maji

“Tunamshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,yeye ni Jemedari wetu ambapo katika kipindi chake ndipo dhana ya mabonde na utunzaji wa vyanzo vya maji ilipong’ara(shine) na kueleweka vizuri kwa wananchi.

“Yaani yeye Mheshimiwa Rais mwenyewe amekuwa akihimiza suala hili la usimamizi endelevu na amekuwa akilisemea mwenyewe  na viongozi wakuu akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais,Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini pia imepata jemedari wetu anayeweza kulisimamia vema Mheshimiwa wetu Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambaye pamoja na maelekezo ya Viongozi basi tusingeweza kupata matokeo ambayo Viongozi wetu wanataka

“Pamoja na yote lakini tunawashukuru wananchi ambao wanashiriki kwenye kampeni zetu za kutunza vyanzo vya maji wako pamoja nasi,wakiona uharibifu wanatoa taarifa,sasa hao wote kwetu sisi ni wadau muhimu sana lakini pia na waandishi wa habari kwa kuwa mstari wa mbele kupeleka elimu ikiwemo usimamizi wa rasilimali maji,lakini pia mnatusaidia kuwafanya wananchi waelewe na kushiriki vema kuhakikisha uendelevu wa vyanzo vya maji”anaeleza Seguye

PBWB pia hufanya kazi ya kusafisha vyanzo vya maji na mito ili mfumo wa maji uendelee katika njia zake bila kuathiriwa na uchafu

 

Next Post
Bodi ya Maji Bonde la Pangani(PBWB) na mikakati ya kulinda,kuhifadhi vyanzo vya maji,yaonya watumiaji wasiona na  vibali

Maji yaongezeka Bwawa la Nyumba ya Mungu,PBWB yahimiza wananchi kuchukua hatua

MSD yaanza kuzalisha bidhaa za afya kupunguza gharama za uagiza nje

MSD yaanza kuzalisha bidhaa za afya kupunguza gharama za uagiza nje

ESAP yaanza utengenezaji vilipuzi kwa ajili ya uchimbaji madini

ESAP yaanza utengenezaji vilipuzi kwa ajili ya uchimbaji madini

Discussion about this post

Contact us:

BAJETI COMMUNICATION

info@bajeti.co.tz
bajetinews@gmail.com
+255718699828
P.o.BOX 18133,
DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Category

  • Habari
  • Magazeti
  • Makala
  • Mazingira
  • Michezo
  • Picha
  • Sayansi na Teknolojia
  • Siasa

Our Visitors

  • Today's visitors:16
  • Today's page views 16
  • Total visitors 16,470
  • Total page views 18,681

Kuhusu Tovuti Hii

Hii ni tovuti ya habari iliyojikita katika kuandika  habari za kina   zikiwemo za mazingira kwa lengo la kuelimisha na kuuhabarisha umma.

Subscribe

  • About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact

© 2025 Bajeti

No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo

© 2025 Bajeti

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In