NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
MFUMO unaotumiwa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu hali ya maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu umesaidia kuondokana na maafa kwa wanaofanya shughuli zao karibu na mito pamoja na maeneo yaliyo bondeni.
Bonde la Pangani ambalo mipaka yake inajumuisha mikoa minne ikiwemo Kilimanjaro,Arusha,Manyara na Tanga lakini pia hushughulika na maji yaliyopo katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo kutumika na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuzalisha umeme.
Hata hivyo PBWB imetengeneza mfumo wa utoaji taarifa za hali ya maji katika bwawa hilo kila siku ili kuwasaidia wananchi kuchukua tahadhari kabla ya maafa kutokea jambo linalowafanya wananchi kuwa makini pindi tu wanapopata taarifa.
Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Pangani hufanyika kwa kuzingatia mfumo shirikishi unaotoa fursa kwa jamii katika kupanga na kusimamia matumizi ya maji kama ulivyoainishwa katika mageuzi makubwa ya Sekta ya Maji yaliyofanyika kupitia Sera ya Maji ya Mwaka 2002
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 25,2026 kwa umma kuhusu hali ya maji kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB)Segule Segule amesema kina cha maji hadi kufikia Aprili 25,2026 cha bwawa ni mita 689.25 juu ya usawa wa bahari ambapo kina cha juu kabisa cha ujazo wa bwawa ni mita 688.91 juu y usawa wa bahari
“Kina hicho ni juu ya kina kilichonakiliwa Aprili 24,2026 kwa sentimita 5(Mita 0.05) ambapo kwa tarehe hiyo kilikuwa mita 689.20.
“Kina hicho ni sawa na sentimita 34(Mita 0.34) juu ya usawa wa juu wa bwawa hivyo tabaka hilo la maji linapita kwenye njia ya utoro (spillway) kwenda upande wa chini kwa kupitia Mto Pangani.
“Kufuatia hali hiyo ,mwenendo wa ongezeko la maji ndani ya bwawa kwa siku zilizopita ni wastani wa sentimita 11 kwa siku”amesema Segule

Aidha Segule amebainisha kuwa maji yanayotoka katika bwawa yataungana na maji yatolewayo na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kiasi cha mita za ujazo 33 kwa sekunde (sawa na lita 330,000/sekunde) ambayo yanatokana na shughuli za uzalishaji umeme na hivyo kiasi cha maji yatakayokapita Mto Pangani(wengine huita Mto Ruvu) kwenda upande wa chini wa mto huo unaopita maeneo ya Wilaya za Same(Vijiji vya Marwa na Ruvu),Mwanga(Kijiji cha Kirya),Simanjiro(Vijiji vya Ngage na Lemkuna),Korogwe(Vijiji vya Buiko,Korogwe Mjini,Makayo na Hale) pamoja na Wilaya ya Pangani yatarajie kupokea maji mengi kuliko hali ya kawaida.
“Tanatoa wito kwa wadau wote hususani wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao chini ya Bwawa la Nyumba ya Mungu pembezoni mwa Mto Pangani pamoja na maeneo yote yanayozunguka bwawa,kuanza kuchukua tahadhari mapema ikiwezekana kuondoka katika maeneo hatarishi kwa ajili ya usalama wao na mali zao.
“Taarifa itaendelee kutolewa ili kuwashirikisha wananchi kuhusu hali ya Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa kadiri itakavyoonekana inafaa mpaka pale ambapo hali itakaporejea kuwa ya kawaida”ameeleza Segule
Segule amewaomba wananchi wote wanaopata na kufikiwa na taarifa hizo za hali ya bwawa zinazotelewa mara kwa mara kuwafikishia wenzao ambao pengine kwa namna moja au nyingine hawapati taarifa kwa wakati ili kuepusha madhara yanaweza kutokea.
Bonde la Pangani linahudumia watu zaidi ya Milioni 4.7 hasa katika majiji ya Arusha na Tanga pamoja na Moshi mkoani Kilimanjaro na sehemu ya Mkoa wa Manyara.
Mbali na kupita katika mikoa minne lakini pia linapita katika wilaya zaidi ya 20 ikiwemo Arusha, Jiji la Arusha,Arumeru(Meru),Simanjiro,Siha,Hai,Moshi Mjini na Moshi Vijijini,Rombo,Mwanga,Same,Korogwe,Korogwe Mjini,Pangani,Jiji la Tanga,Mkinga,Muheza,Handeni,Handeni Mjini,Kilindi ikiwemo na ,Lushoto

Discussion about this post