NA MWANDISHI WETU
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Charles Kichere amebaini kuwepo wajumbe katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tukuyu wakiwa na elimu ya darasa la saba badala ya kidato cha nne.
CAG Kichere ameyabainisha hayo katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 iliyotolewa tarehe 30/3/2026 .
“Katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tukuyu, nilibaini ina wajumbe wawili wenye sifa ya elimu ya darasa la saba. Jambo hilo ni kinyume na Kanuni ya 6(4)(a) ya Kanuni za Huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira za mwaka 2019.
“Kanuni hiyo inataka, katika kupendekeza na kuteua wajumbe wa bodi wa mamlaka za majisafi, mamlaka inayohusika itazingatia mtu anayependekezwa au kuteuliwa awe na angalau kiwango cha elimu cha kidato cha nne, uzoefu wa usimamizi au amewahi kutumikia kama mjumbe wa bodi, mkazi wa kudumu ndani ya eneo la utendaji la mamlaka ya maji, na awe na rekodi nzuri ya ulipaji wa ankara za maji”amefafanuwa CAG Kichere
Katika hatua nyingine CAG Kichere amebaini katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Kamati ya Mipango na Fedha, Kamati ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu, na Kamati ya Ukaguzi zilikuwa na wajumbe chini ya watatu, jambo ambalo ni chini ya idadi ya chini inayohitajika kwa ajili ya utendaji mzuri wa kamati.
Amesema upungufu alioubainisha ulisababishwa na mamlaka za uteuzi kuchelewa kuteuwa wajumbe wapya mara baada ya muda wa wajumbe wa awali kumalizika ikiwemo mapitio yasiyotosheleza ya sifa za wajumbe ili kuhakikisha uzingatiaji wa kanuni na taratibu.
Ameongeza kuwa bila kuwa na Bodi ya Wakurugenzi inayofanya kazi, ufanisi wa taasisi unaweza kuathiriwa ambapo hali hiyo inasababisha udhaifu katika utawala, kuongezeka kwa hatari ya kutokuwa na udhibiti wa kifedha, na kupungua kwa imani ya wadau.
“Ninapendekeza: (a) Mashirika ya umma na taasisi zingine zilizobainishwa, kwa kushirikiana na Serikali, ziweke utaratibu madhubuti wa kuhakikisha teuzi za Bodizinafanyika kwa wakati mara tu wajumbe wanapomaliza muda wao;
“(b) Ofisi ya Msajili wa Hazina ifuatilie kwa ukaribu muda wa ukomo wa wajumbe wa bodi na kuanza mchakato wa uteuzi au kuhuisha wajumbe, angalau miezi sita kabla ya muda kwisha, ili kuzuia nafasi za wajumbe na mwenyekiti kuwa wazi.”ameeleza CAG Kichere




Discussion about this post