NA GOODLUCK HONGO
SERIKALI imeendelea kupambana na wahalifu wanaojihusisha na dawa za kulevya ili kulinda afya za watanzania kwa kuwashughulikia kila kona ili watafute shughuli zingine za kujipatia kipato.
Dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikiathiri zaidi nguvu kazi ya Taifa ambao ni vijana imesababisha mzigo mkubwa katika familia za kuwatunza waraibu wa dawa hizo huku wauzaji wakiishi maisha ya anasa kwa kumiliki magari,majumba na mali zingine nyingi za thamani.
Katika kupambana na wahalifu hao licha ya kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria lakini pia pale wanapopatikana na hatia,mali zao zote hutaifishwa.
Katika Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2025 iliyotolewa Mei 2026 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeleeza kuwa katika kuendeleza hatua za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya,mali zenye thamani ya Sh.Bilioni 3.3 zilitaifishwa.
Taarifa hiyo iliyowekwa saini na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge ,Uratibu na Wenye Ulemavu) Prof.Palamagamba Kabudi na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)Aretas Lyimo imebainisha kuwa moja ya mali zilizotaifishwa ni pamoja na jahazi.
“Katika kuendeleza hatua za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya,Mahakama Kuu Division ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa maamuzi ya kutaifishwa kwa mali za watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya zenye thamani ya Sh.Bilioni 3.3”
“Mali zilizotaifishwa ni magari 16,nyumba 12,viwanja 11,pikipiki mbili na jahazi moja”imebainisha taarifa hiyo


Discussion about this post