NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu Selemani Kakoso amesema wanahitaji uwekezaji ili kuifanya nchi isonge mbele lakini wawekezaji wanahitajika kufuata sheria.
Kakoso ameyasema hayo baada ya kusikiliza maoni ya Serikali kuhusu maombi ya Chama cha BOPOA – Lake Zone kufanya mapitio ya kifungu cha 57 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zake ili kuruhusu matumizi maalumu ya Ukanda wa Mita 60 kwa shughuli za kibandari kama ilivyoelekezwa na Tangazo la Serikali (GN) Namba 293 la Mwaka 2022.
Kakoso amesema ni muhimu kwa wadau kushiriki katika vikao vya kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali vinavyoitishwa na Bunge ili mchango wao uweze kufanyiwa kazi.
Kakoso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanganyika ameongeza kuwa ni kweli wanahitaji uwekezaji ili kuifanya nchi isonge mbele lakini wawekezaji wanahitajika kufuata sheria.
“Mazingira yameharibiwa hivyo wana wajibu wa kuyasimamia ili yarudi katika hali yake“amesema Kakoso
Kakoso ameelekeza wawekezaji BOPOA – Lake Zone kufanya shughuli zao kwa kufuata miongozo na sheria ya mazingira na kufanya kazi kwa ukaribu na NEMC kwakuwa wao ndio wanaosimamia mazingira kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akizungumza mbele ya Kamati hiyo,Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Reuben Kwagilwa amesema Serikali haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji wenye nia ya kufanya uwekezaji wa miradi ya maendeleo bali itaendelea kuwawekea mazingira wezeshi na kusimamia sheria ili mazingira yasiharibiwe.
Kwagilwa amesema Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa shughuli za kibandari nchini zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, huku ikiimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi.
Amesisitiza kuwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) halipo kwa ajili ya kuzuia miradi bali inafanya kazi yake kuhakikisha wadau wanatimiza wajibu wao kwa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria bila kuchafua mazingira.
Aidha,Kwagilwa amebainisha kuwa kwa kutambua umuhimu wa bandari katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza pato la taifa, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza miundombinu ya bandari na kuboresha uendeshaji wa shughuli za kibandari nchini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti lengo la kufanya haya yote ni kuongeza ufanisi, kuvutia uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta ya usafiri wa majini katika maendeleo ya nchi,“ amesema Kwagilwa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Jackson Kiswaga, Naibu Waziri wa Uchuzi David Kihenzile, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), NEMC na Chama cha BOPOA-Lake Zone.



Discussion about this post