NA GOODLUCK HONGO
KANISA la Ufufuo na Uzima limejipanga kuanza kuwasafirisha kwa kutumia helikopta waumini wake wanaofunga ndoa hadi katika mbuga ya wanyama ya Saadan kabla ya kuwarudisha tena katika viwanja vya kanisa hilo.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi Mkuu na mwanzilishi wa makanisa ya Ufufuo na Uzima duniani Askofu Josephat Gwajima Oktoba 18,2026 Ubungo mkoani Dar es Salaam wakati akiendesha ibada ya jumapili kanisani hapo.
Askofu Gwajima ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu yeye na maelfu ya waumini wake wazindue jengo jipya la Kanisa hilo aliloiita hekalu baada ya kukamilika kwa ujenzi wake uliochukua zaidi ya miaka mitatu.

Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo Askofu Gwajima amesema kama kuna mtu ndoa yake inalegalega basi aende kanisani hapo akiwa na njoo na mwenza wake na atakuwa pamoja nao katika mkesha mpaka asubuhi siku ya alhamisi ambapo pia atauliza maswali ambayo yatajibiwa ili arekebisha ndoa ambayo imeharibika.
“Kama unafikiri wewe ni kijana,sisi ujana hapa Ufufuo na Uzima ni mtu mwenyewe,ukiwaza kwamba wewe ni kijana hata kama una miaka 70 njoo,awazavyo mtu ndivyo alivyo”amesema Askofu Gwajima
Aidha amebainisha kuwa katika kipindi chao cha vijana na mahusiano kinachofanyika kila alhamisi kilipata usumbufu alhamisi iliyopita lakini alhamisi hii kitafanyika.
“Nilikuwa na watu zaidi ya 2000 alhamisi iliyopita na alhamisi hii usiku kitafanyikia ukumbi huu wa juu na kila kijana umeoa au umeolewa au hujaoa au hujaolewa ufike”
“Jambo lingine ambalo ninataka mjue,ukumbi wetu haujakamilika bado,tuliagiza viti kutoka nje ya nchi,viti zaidi ya 15,000 na tulitegemea viingie alhamisi na vifungwe ,vimechelewa kidogo,bila shaka jumatatu au jumanne vitaingia hapa,kwa hiyo tutakuwa na kazi ya kufunga viti”amesema Askofu Gwajima
Ameeleza kuwa kama mungu akipenda na kama ikienda kama alivyopanga basi jumapili ijayo watakuwa na viti vipya ambavyo vimefungwa na hawatakuwa na viti ambavyo watahamisha hamisha.
“Hapa kwa juu kuna mahali ambapo helikopta inatua,unatua na helikopta juu ya jengo na kuna njia hapo ya kushuka kuja Kanisani na ukimaliza ibada unapanda unaenda na helikopta tena.
“Unaepuka kabisa kuona na wambea,wale wanaotaka kufanya umbea na tumweka longe na ukitua na helikopta unapata bufee,na hata marubani wanaangalia ibada na ndege yao inakaa juu na ibada ikiisha huyo unaondoka
“Ninapanga maharusi ambao wanafunga ndoa vizuri,ukimaliza kufunga tunakupandisha kwenye helikopta na kisha unaruka kwenda Saadan kwenye mbuga ya wanyama,unazunguka kidogo halafu unarudishwa tena kwa ajili ya reception(mapokezi na hata yule aliyefunga ndoa zamani atatamani arudie tena mara ya pili na wakitamani hivyo itakuwa sawa sawa.”amesema Askofu Gwajima
Hata hivyo Askofu Gwajima hajabanisha kuwa helikopta hiyo itakuwa ni mali ya Kanisa la Ufufuo na Uzima au itakuwa inakodishwa kwa ajili ya matumizi ya maharusi wanaofunga ndoa kanisani hapo a kuongeza kuwa watu wamepona bila kuwa na vitambaa,mafuta wala chumvi.
Jengo jipya la Kanisa hilo linauwezo wa kuchukua zaidi ya watu 10,000 huku likiwa na majengo ya ofisi,mgahawa na kumbi za ibada pamoja na uwanja wa kutua ndege aina ya helikopta juu.

Discussion about this post