KWAYA ya uinjilisti Yelusalemu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Msimbazi Jimbo la Kati inatarajia kuanzisha kiwanda kidogo cha kusindika nyama na utengenezaji wa mbolea.
Mbali na kuanzisha kiwanda hicho cha kusindika nyama lakini pia wataanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea inayotokana na kinyesi cha wanyama.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kwaya hiyo Sara Elia jijini Dar es Salaam juzi wakati wa uzinduzi mdogo wa nyimbo zao pamoja na uwekaji wakfu wa vyombo vya muziki iliyofanyika kwenye ibada maalum katika kanisa hilo.
Elia amesema wanatambua wajibu wa kutoa huduma ya uimbaji na kupeleka ujumbe wa kiroho wa kijamii hivyo wamedhamiria kuanzisha kiwanda hicho.

.
Amesema kuna machinjio ya kisasa Vingunguti hivyo wana ndoto ya kuanzisha kiwanda kidogo cha kusindika nyama na utengenezaji wa mbolea inayotokana na kinyesi cha wanyama Kwa kuwa mali ghafi zipo katika maeneo ya machinjio.
“Kwaya yetu ina wanakwaya wasiozidi 30 tumedhamiria kuwa na kwaya yenye kumiliki viwanda ndani ya kwaya hivyo tuendana na kasi ya Tanzania yenye uchumi wa kati na kutoa ajira ndani ya kanisa na wakihubiri Yesu Kristo,kutoa uinjilishaji kwa weledi mkubwa.
“Lakini pia kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hasani “amesema Elia.
Naye Mwalimu wa kwaya hiyo,Gabriel Mzirai amesema kwa upande wa nyimbo zao zimekuwa na baraka kwa waumini na wamekuwa sehemu kubwa ya mchango kanisani.
Mwinjilisti Kiongozi wa Kanisa hilo,Anna Mwigune amewataka wanakwaya hao wajitambue kuwa wao ni kioo cha jamii na ujumbe wao uwe wenye mafundisho ndani ya jamii.
Discussion about this post