BAADHI ya nchi kusini mwa Bara la Ulaya zimekumbwa na joto kali ambalo limesababisha moto katika baadhi ya nchini kama Uturuki, Uhispania na Italia.
Mbali na nchi hizo lakini zingine zilizokumbwa na joto kali hadi sasa na kusababisha vifo vya makumi ya watu ni pamoja na Canada na Japan.
Wataalamu wamesema athari za mabadiliko ya tabia nchi ndiyo zinachochea hali hiyo.
Ugiriki nayo imekumbwa na wimbi kubwa la joto kali ambalo halijashuhudiwa kwa karibu miongo miwili wakati inazidisha juhudi za kuzima moto uliozuka maeneo kadhaa ya nchi hiyo kutokana na kupanda kwa kiwango cha joto.
Kwa mujibu wa taarifa ya DW imeeleza kuwa watabiri wa hali ya hewa wameonya kuwa kiwango cha joto kinaweza kupindukia nyuzi 47 za kipimo cha Celcius katika muda wa wiki moja inayokuja, na kuongeza uwezekano wa maeneo mengi zaidi kuwaka moto.
Mapema leo serikali ya nchi hiyo imetuma ndege na vifaa vingine kwenda maeneo mawili ya Peloponnese na kisiwa cha Rhodes kudhibiti moto ambao tayari umeunguza maelfu ya hekari za misonobari na mizaituni tangu ulipozuka mwisho mwa juma.
Wakati hali hiyo ikiendelea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyataka mataifa yote kuungana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
Guterres alitoa kauli hiyo baada kundi la nchi ishirini tajiri, G20 kushindwa kukubaliana kuhusu ahadi muhimu za mabadiliko ya tabianchi wakati wa Mkutano wao wa Mawaziri uliofanyika Julai 23-25 mwaka huu kuhusu Mazingira, Mabadiliko ya tabianchi na Nishati.
Discussion about this post