NEW YORK,MAREKANI
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema zinahitajika nguvu za pamoja kutoka kwa viongozi wote wa serikali duniani ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia.
Kauli ya Guterres imekuja baada ya ripoti mpya ya wanasayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC) iliyotolewa leo jijini New York,Marekani kubainisha kuwa shughuli za binadamu zinapeleka dunia katika madhara ya tabianchi yasiyorekebishika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini New York, Marekani kuhusu uchambuzi wa ripoti hiyo, Guterres amesema, ripoti imeonesha shughuli za kibinadamu zinazidi kuiathiri sayari dunia na joto limezidi kuongezeka ilihali kuna makubaliano yaliyofanyika Paris nchini Ufaransa ya nchi zote kupunguza gesi ya ukaa.
“Ripoti ya leo ya IPCC imeonesha alama ya hatari, shughuli za kibinadamu zinaendelea kuathiri dunia na haziwezi kukanushwa kwani kuna ongezeko la uzalishaji wa gesi ya ukaa.
“Ukataji wa miti na shughuli zote hizi zinawaweka mabilioni ya watu katika hatari. Joto limeathiri kila kona ya dunia na mabadiliko mengi hayatabiriki.”amesema Guterres
Akizungumzia mkataba wa kimataifa wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa mwaka 2015, Guterres amefafanua kuwa kwa sasa dunia kwenye nyuzi joto 1.2 katika kipimo cha Selsiyasi na joto lingali likiongezeka kwa haraka huku viwango vya gesi chafu navyo vikiongezeka,
Guterres amebainisha kuwa hali mbaya ya hewa na majanga mengine pia yamekuwa yakiongezeka.
“Kizingiti tulichokubaliana kimataifa cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kiko karibu sana kufikiwa na hii ni hatari na lazima tuchukue hatua sasa.”amesema Guterres
Discussion about this post