ALGIERS,ALGERIA
MOTO unaoendelea kuwaka katika baadhi ya nchi duniani kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ongezeko la joto linalosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa (tabianchi)umeua watu 42 nchini Algeria.
Moto huo unaowaka na kuteketeza maelfu ya hekta za misitu na nyumba umekuwa tishio kutokana na kusababisha vifo na kulazimisha maelfu kuhamishwa katika makazi yao.
Serikali ya Algeria imetangaza kuwa watu 42, kati ya hao 25 walikuwa wanajeshi, wamefariki katika moto wa unaoendelea kuwaka katika misitu nchini humo.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Aymen bin Abdurrahman katika taarifa kwenye kituo cha luninga cha serikali alitoa habari juu ya moto huo unaoendelea kuteketeza hekta za misitu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Amesema watu 42, 25 kati yao wakiwa wanajeshi, walifariki katika moto huo.
Ameongeza kuwa mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kukodisha ndege za kuzima moto kutoka nchi za Ulaya.
Kulingana na habari ya Shirika la Habari la nchi hiyo (APS),limetangaza kuwa moto wa misitu umewaka katika maeneo 103 ambao ulirekodiwa katika majimbo 17 nchini humo.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nchi hiyo Kamil Bilcud amesema kwamba kuna uwezekano wa kufanywa kwa hujuma katika suala hilo, na kwamba wale wanaohusika watatambuliwa katika uchunguzi.
Katika siku za hivi karibuni, Algeria imekuwa eneo la moto wa misitu ulioanza baada ya wimbi kali la joto na upepo mkali kutoka kusini.
Wakati huo huo nchini Marekani moto unaendela kuteketeza mamia ya hekta za misitu katika majimbo 15 ya nchi hiyo huku serikali ikipeleka wazima moto 26,000 kukabiliana na hali hiyo.
Wataalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa (tabianchi) wa Marekani wametabiri kuwa, moto huo utaendelea kuteketeza maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo na kuongezeka joto ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa (tabianchi) duniani.
Wataalamu hao na maafisa wa zima moto wametabiri kuwa, maeneo ya magharibi mwa Marekani yataendelea kuathiriwa na moto mkubwa kwa kuzingatia hali ya joto kali inayotawala sasa.
Kwa sasa maafisa wa Idara ya Zima Moto na wa majimbo ya Marekani wanajiandaa kukabiliana na moto mkubwa unaotazamiwa kuyaathiri maeneo ya kaskazini na kaskazini magharibi mwa jimbo la Califonia.
Luninga ya CNN imeripoti kuwa, hadi kufikia Agosti 10,mwaka huu wafanyakazi wa huduma ya zima moto zaidi ya 26,000 walikuwa wamefika katika majimbo 15 ya nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na moto huo ambao hadi sasa umeteketeza zaidi ya hekta 1000.
Moto wa sasa ulioiathiri Marekani uliopewa jina la “Dixie” unatajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya California.
Ugiriki na Uturuki ndizo nchi zilizoathirika zaidi na moto huo unaodaiwa kuwaka kutokana na ongezeko la joto kali huku baadhi ya nchi kama Canada ikiwemo Japan joto hilo limesababisha vifo vya watu wengi.
Agosti 10,2021,ripoti ya jopo la wanasayansi wa mabadiliko ya (hali ya hewa) tabia nchi (IPCC) kutoka Umoja wa Mataifa wameonya kuwa joto la dunia limeongezeka hadi kufikia 1.2 selsias na kwamba miaka 15 ijayo joto litaongezeka zaidi kutokana na shughuli za binadamu za uzalishaji wa gesi yan kaboni
IPCC imesema matukio ya moto, ukame na mvua kubwa katika sehemu mbalimbali duniani yametokana na athari za mabadiliko ya(hali ya hewa) tabia nchi.
Discussion about this post