PARIS,UFARANSA
WAKATI Umoja wa Mataifa ukitaka hatua za haraka kuchukuliwa na serikali zote duniani juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi,Ufaransa imehamisha maelfu ya raia wake kutokana na moto wa msitu unaowaka katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Ufaransa inajiunga na baadhi ya nchi kama Marekani,Canada,Uturuki,Algeria na zingine ambazo zinapambana na moto wa msitu unaeondelea kuwaka na kuharibu maelfu ya hekta za misitu na makazi ya watu kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ongezeko la viwango vya joto kutokana na mabadiliko ya tabia nchi .
Agosti 9,2021,Ripoti mpya ya wanasayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC) kutoka Umoja wa Mataifa imeonesha kuwa joto la dunia limeongezeka hadi kufikia 1.2 katika vipimo vya selsias na kusababisha kutokea kwa moto, mafuriko,na vimbunga.
Kwa mujibu wa taarifa ya DW leo imeeleza kuwa maelfu ya watu wakiwemo watalii wameokolewa baada ya moto wa nyika kuwaka karibu na kituo cha watalii eneo la Saint-Tropez kusini mwa Ufaransa.
Idara ya zima moto imesema wazima moto wapatao 750 na ndege za kupambana na moto zilitumwa katika eneo hilo ili kusaidia katika shughuli za uokoaji.
Moto huo ambao ulianza jana Jumatatu karibu kilomita 100 kutoka wa mji wa Toulon, umesambaa kwa kasi na kuchoma hekta 3,500 za msitu na sehemu kavu kufikia leo asubuhi.
Msemaji wa idara ya zima moto ya nchi hiyo amesema maelfu ya watu wamehamishwa kama hatua ya tahadhari lakini hakuna wahanga, na kuongeza kuwa moto huo bado unandelea kuwaka.
Ufaransa ni ya hivi karibuni kati ya nchi za ukanda wa Mediterania zinazoshuhudia wimbi kali la joto ambalo limesababisha moto mkubwa wa nyika.
Wanasayansi wanatahadarisha kuwa matukio ya moto kuwaka yataendelea kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi(mabadiliko ya hali ya hewa)
Baadhi ya nchi ambazo zinapambana na moto wa nyika uliosabishwa na mabadiliko ya tabia nchi duniani ni pamoja na Canada,Uturuki,Marekani,Algeria ikiwemo Japan ambayo watu wamefariki kutokana na joto kali.
Discussion about this post