PORT-AU-PRINCE,HAITI
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Shirika la Ulinzi wa Raia nchini Haiti limesema idadi ya vifo kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Agosti 14,2021 imeongezeka na kufikia 2000 na wengine 10,000 kujeruhiwa.
Hata hivyo mbali na tetemeko hilo kuuwa na kujeruhi, familia zaidi ya 30,000 hazina makazi baada ya nyumba 115,000 kuharibiwa kutokana na tetemeko hilo.
Agosti 16,2012, ndani ya saa 48 baada ya tetemeko hilo, kikaja kimbunga Grace, ambacho pamoja na uharibifu mwingine, Shule 94 zimesambaratishwa kabisa ikiwa ni wiki tatu tuu kabla wanafunzi kurejea shuleni hapo (Septemba 7, 2021).
Katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa jiji la Les Cayes, Kiongozi eneo hilo Aldorf Hilaire amesema manusura wanategemea msaada kutoka kwa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka pekee kwa sababu msaada wa serikali haujafika kwenye eneo hilo hadi sasa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephaane Dujarric amesema umoja huo umetenga dola milioni nane kutoka Mfuko wa dharura ili kutoa huduma muhimu za afya, maji safi, makao ya dharura na usafi wa mazingira kwa watu wote walioathiriwa
Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF),limesema mvua kubwa pia zimeharibu upatikanaji wa huduma za maji, makazi , na huduma nyingine za msingi.
Hospitali katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa nchi hiyo ambako tetemeko lilitokea zimeelemewa na idadi ya watu waliojeruhiwa na zinahitaji wafanyakazi zaidi wa afya na vifaa ikiwemo dawa za kupunguza maumivu.
Mexico na Jamhuri ya Dominican ni miongoni mwa nchi zilizotuma msaada wa chakula na dawa ambapo Cuba imepeleka wafanyakazi 235 wa huduma za afya.
Haiti ni kisiwa kidogo kilichoko Ukanda wa Caribbea ambapo matukio hayo yote yanatokea ikiwa ni mwezi mmoja tuu tangu rais wa nchi hiyo Jovenel Mois kuuawa Ikulu Julai 07, 2021
Discussion about this post