NA MWANDISHI WETU
MABADILIKO ya tabianchi yametajwa kuwa ni kikwazo kikubwa katika Sekta ya Kilimo Tanzania Bara huku Tanzania Zanzibar ikikabiliwa na wizi wa mazao.
Hayo ni kwa mujibu wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20 katika Ripoti ya Matokeo Muhimu kwa Sekta za mazao,mifugo na ufugaji wa samaki iliyotolewa Agosti mwaka huu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Sensa hiyo imeonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaonekana kuwa ni changamoto kubwa inayoikabili sekta ya kilimo kwa Tanzania Bara ikifuatiwa na gharama za pembejeo ikilinganishwa na Zanzibar ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa za wizi wa mazao na uhaba wa ardhi.
“Matokeo ya Sensa yanaonesha kuwa, kaya nyingi zilikutana na vikwazo mbalimbali katika Mwaka wa Kilimo 2019/20.
“Baadhi ya vikwazo vikubwa muhimu vilivyoripotiwa na kaya katika shughuli za kilimo ni mabadiliko ya tabianchi (ukame, mafuriko; asilimia 17.8), gharama za pembejeo (asilimia 15.6), upatikanaji wa ardhi (asilimia 13.5), bei ndogo za mazao (asilimia 7.2), magonjwa na wadudu waharibifu (asilimia 6.7), upatikanaji wa pembejeo (asilimia 5.6) na rutuba ya udongo (asilimia 5.6).imeeleza taarifa hiyo.
Katika ujumbe muhimu wa Sensa hiyo umeongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yataendelea kuathiri sekta za mazao na mifugo na hivyo kupungua kwa tija katika uzalishaji.
Hata hivyo imependezwa kuwa kuendeleza kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, kilimo cha umwagiliaji na utafiti na matumizi wa mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi ni muhimu.
Aidha katika ujumbe muhimu wa taarifa hiyo imebainisha kuwa kutokana na uhaba wa ardhi uliopo Zanzibar, ni muhimu kutoa kipaumbele kutumia eneo dogo kwa kuongeza uzalishaji.
“Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, matokeo ya Sensa yanaonesha kuwa, wizi wa mazao (asilimia 20.8) ni kikwazo kikubwa kilichoathiri shughuli za kilimo kwa mwaka wa kilimo 2019/20, ikifuatiwa na upatikanaji wa ardhi (asilimia 12.0), uharibifu wa wanyama/ndege (asilimia 11.0),
“Magonjwa na wadudu waharibifu (asilimia 11.0), gharama za pembejeo (asilimia 6.8), upatikanaji wa pembejeo (asilimia 5.1) na wizi wa mifugo (asilimia 5.1)”imefafanua taarifa hiyo
Discussion about this post