MAMIA ya Wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam leo wamejitokeza kupata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa UVIKO-19 (COVID-19)hali iliyoifanya serikali kuongeza siku moja ya zoezi hilo.
Mbali na hilo lakini pia kila aliyepata chanjo hiyo amepatiwa cheti kinachotambulika kimataifa.
Akizungumza leo katika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam mara baada ya kukagua zoezi hilo la chanjo,Mkuu wa Mkoa huo Amos Makalla amesema hadi kufikia majira ya saa 4.00 asubuhi tayari wananchi zaidi ya 2,882 walikuwa wamejitokeza kuchanjwa.
Amesema zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa ambapo aliwataka wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam nao kuandaa zoezi kama hilo kwenye wilaya zao ili kila mwenye uhitaji apate huduma hiyo.
Amesema kila aliyepata chanjo hiyochati chake kitatambuliwa kimataifa hivyo ni muhimu kwa wanachi kujitokeza kupata chanjo hiyo wakati huu ambapo serikali inaendesha zoezi hilo bure.

“Kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi waliofurika Uwanja wa Uhuru kupata chanjo ya UVIKO-19(CORONA), tumeamua kuongeza tena siku moja ya utoaji wa chanjo ili kuhakikisha kila mwenye uhitaji anapata huduma”amesema Makalla.
Makalla amefafanua kuwa ameongeza muda huo kutokana na baadhi ya wananchi kutoka makundi mbalimbali walioomba muda uongezwe kutokana na baadhi yao kushindwa kuhudhuria siku ya leo kwa sababu mbalimbali.
Discussion about this post