MBUNGE wa Malinyi wilayani Malinyi Mkoa wa Morogoro Antipas Mgungusi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh.Bilioni 1.5 ili kusaidia kutatua kero za barabara katika eneo hilo.
Hayo ameyasema Agosti 21,2021 wilayani Malinyi Mkoa wa Morogoro wakati akizungumzia kuhusu kutatua kero za wananchi wa jimbo lake ambazo baadhi aliziahidi wakati wa kampeni katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amesema kwa sasa fedha zipo kwa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA)na kinachosubiriwa ni upembuzi yakinifu kuangalia maeneo korofi ambapo kazi hiyo wamepewa Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT).
Amesema kipindi cha masika kumekuwa na kero kubwa ya mafuriko hivyo fedha hizo zitakwenda kujenga madaraja na makaravati kwa kuwa eneo hilo linapitiwa na mto Furuwa ambao hauna kingo wala kina.
“Barabara hii ni muhimu sana watu wanatoka Mlimba kupitia Malinyi lakini pia inaungisha Malinyi Mjini na Kata za Biro na Igawa hivyo kukamilika kwakwe kutakuwa msaada mkubwa kwa wananchi.
“Tuliahidi kwa wananchi kushughulikia kero hii na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ametupa kisiasi cha Sh.Bilioni 1.5 ili tujenge madaraja na makaravati kwani barabara hii pia inakwenda katika hospitali yetu ya wilaya ambayo inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakati hospitali yetu ya serikali inaendelea kujengwa”amesema Mngungusi
Baadhi ya wananchi wa Malinyi waliishukuru serikali kwa kuweka maandalizi ya ujenzi wa barabara.
Tunamshukuru Mbunge na Serikali kwa ujumla kwa kuwa tulikuwa tunatumia mitumbwi kwenda kujifungua na wakati mwingine unajifungulia njiani na kupoteza mtoto lakini ikiwa watatekeleza hili basi utakuwa mkombozi kwetu”amesema Flaviana Chrisptopher.
Malinyi imekuwa ikikumbwa na mafuriko hasa nyakati za masika kutokana na kile kinachoelezwa kuwa eneo hilo kuwa tambarare na mto unaopita katika eneo hilo kutokuwa na kingo wala kina hivyo maji husambaa kote bila kudhibitiwa.
Discussion about this post