NA MWANDISHI WETU
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam ipo katika mchakato wa kutunga sheria ndogo ya kuwashughulikia ombaomba ikiwemo kuwashitaki watu wote wanaowapatia fedha.
Hata hivyo watoto wengi ndio waathirika na watu hao ambao huwatumia kuomba fedha huku wenyewe wakiwa wamekaa kivulini hali inayochangia ukatili dhidi yao ikiwemo kutokwenda shule.
Hayo yalizungumzwa jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Makatibu Tawala wote wa Mkoa wa Dar es Salaam Charangwa Makwiro wakati wa kuanza kwa uundaji wa mabaraza na madawati ya watoto shuleni kwa kuwahusisha maofisa Ustawi wa Jamii kutoka Mkoa wa Dar es Salaam wakishirikiana na Sos Children’s Villages
Makwiro alisema Manispaa ya Kinondoni na Ilala ndio waathirika wakubwa wa suala la ombaomba kwa kuwa kila wanapoondolewa basi hukimbilia Manispaa nyingine.
“Kwa niaba ya Makatibu Tawala wote wa Mkoa wa Dar es Salaam tumeyapokea maombi yaliyotolewa lakini tupate taarifa rasmi za maandishi.
“Ombaomba wapo kwa sababu watu wapo,wanahela kupita hata sisi,wakimaliza jioni wanaoga vizuri sasa sisi kama Jiji la Dar es Salaam tumeenda mbali zaidi na sasa tunaandaa sheria ndogondogo ili kuwakamata na wale wanaotoa fedha kuwapa ombaomba”amesema Makwiro
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Alex Mtaboneka amesema juhudi za kukomesha ukatili dhidi ya watoto lazima ziendane na kuwaangalia pia waganga wa tiba asili.
Amesema watu hao nao wanachangia katika suala hilo kwa kuwa hali ilivyo sasa wanaelekea kurasimishwa kwa kuitwa waganga wa tiba asili.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Familia kutoka SOS Children’s Villages Kennedy Mashema amesema wao wamekuwa na miradi mbalimbali ikiwemo kuwakutanisha wadau ili kuhakikisha kuwa ushiriki wa watoto katika kutambua haki zao pamoja na ulinzi ili kuondoa ukatili dhidi yao.
“Sisi SoS Children’s Villages kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mkoa wa Dar es Salaam tumeanza uundwaji wa mabaraza ya watoto na madawati ya watoto shuleni.
“Tumewezesha wanafunzi kushiriki kikamilifu siku ya Mtoto wa Afrika ikiwemo kuzishirikisha shule za Zingiziwa na Chakina kama shule za mfano katika juhudi za kupinga ukatili dhidi ya watoto”amesema Mashema.
Naye mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari Mikocheni Miraji Idrisa
Amesema amejifunza vitu vingi lakini muhimu zaidi ni kuwa watoto lazima wapate malezi ya baba na mama.
“Akipigwa basi huo ni ukatili maana lazima asikilizwe,sisi tuliopata elimu hii ndio tutakuwa mabalozi wa kuhakikisha kuwa ukatili dhidi ya watoto unafika mwisho na watoto lazima waishi na wazazi wao”amebainisha Idrisa




Discussion about this post