NA GOODLUCK HONGO
SHIRIKA lisilo la kiserikali la SOS Children’s Villages limesaidia zaidi ya vikundi 32 kujikwamua kiuchumi huku wakiendeleza kazi za kupinga ukatili dhidi ya mtoto katika Kata za Chanika na Zingiziwa jijini Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Development Concern (DECO) linalofanyakazi kwa kushirikiana na SOS Children’s Villages Robert Nyampiga wakati alipokutana na viongozi wa vikundi vya huduma ndogo za kifedha vilivyopo chini ya Mradi wa Kuimarisha Familia na Ustawi wa Mtoto kutoka SOS Children’s Village na kuunda Umoja wa Usimamizi wa Mfuko wa Mtoto (UWAMTO) katika Kata za Chanika na Zingiziwa.
Nyampiga amebainisha kuwa mradi huo ulianza baada ya SOS Children’s Villages kuona ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya watoto hivyo kuamua kuuanzisha ambapo umesaidia kupunguza vitendo hivyo kwa asilimia 80 katika Kata hizo.
Ameongeza kuwa wao wamekuwa na kazi kubwa ya kuhakisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili kama ubakaji na unyanyasi ili kuondoa wimbi la watoto walioko mtaani ambapo ikiwa juhudi zitafanyika kwa pamoja basi wimbi la watoto walioko mtaani litapungua na ikiwezekana kuondoka kabisa.
“SOS Children’s Villages ni mwezeshaji na mlezi wa vikundi 32 na wao kama DECO ni wawezeshaji ambapo vikundi hivyo licha ya kuwezeshwa kufanya masuala ya ujasiriamali ili kujiongezea kipato lakini pia kuendelea na shughuli za kupinga ukatili dhidi ya mtoto.”alisema Nyampiga
Naye Mwenyekiti wa UWAMTO Shirazi Sinde amesema changamoto waliyonayo kwa sasa ni uendelewa mdogo kwa wananchi juu ya UWAMTO kwa kuwa wao kama jamii wamekuwa wakisaidia watoto pindi wanapofanyiwa ukatili.
Mwakilishi wa Kikundi cha Tuwezeshane Maonesho Rashidi amesema SOS Children’s Villages wamefanya kazi kubwa ikiwemo kuchimba visima,kujenga madarasa na kusaidia watoto hasa katika kuibua ukatili dhidi ya watoto.
“Serikali inahuruma lakini tungeomba SOS Children’s Villages wasimamie wenyewe ikiwemo kusimama mahakamani kutoa ushahidi maana kazi waliyoifanya imesaidia sana kupungua kwa vitendo vya ukatili kwa watoto katika eneo hili tofauti na ziku za nyuma”amesema Maonesho

Awali Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Jiji la Dar es Salaam Daudi Mpoli amebainisha kuwa SOS Children’s Villages imefanya kazi kubwa katika ngazi mbalimbali za Wizara,Mkoa,Wilaya na Kata na kuwataka wale wote wanaowezeshwa kuendeleza miradi hiyo ili iwe endelevu.
“Nawapongeza sana juu ya kufanikiwa kuanzisha mfuko huu wa watoto katika Kata za Zingiziwa na Chanika lakini lazima mfanye kazi kisasa kwa kushirikiana na serikali kwani watu wanaopata mahitaji kutokana taasisi mbalimbali wapo wengi lakini Balozi na Afisa Maendeleo wa Kata wanajua taasisi na idadi ya watoto wanaosaidiwa katika eneo husika.
“Sisi kama serikali mikopo ipo katika vikundi kama hivi ili kutunisha mfuko huo kwani kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mfumo bora kwa vikundi kupata mikopo bila mlolongo”amesema Mpoli




Discussion about this post