NA MWANDISHI WETU,MWANZA
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewataka Wahifadhi nchini kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kuhifadhi rasilimali za Taifa.
Masanja ametoa kauli hiyo leo Agosti 27,2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Buhindu Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Amesema uwepo wa mahusiano mazuri utasaidia kupunguza changamoto za uchomaji wa mkaa, wizi wa miti, uingizaji mifugo ndani ya hifadhi na majanga ya moto kwenye misitu.
“Jengeni mahusiano mazuri na jamii na zinapokuwa na mahitaji ambayo yako ndani ya uwezo wenu msisite kuwasaidia” amesema Masanja.
Hata hivyo Masanja amewataka wahifadhi kuweka utaratibu mzuri wa uvunaji wa miti kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
“Tengenezeni mazingira rafiki ya utaratibu ulio wazi wa uvunaji miti, kila mtu aingie kwenye ushindani bila kumuonea mtu” amesema Masanja.

Naye, Meneja wa Shamba la Miti Buhindi Mussa Tinda ameeleza kuwa shamba limekuwa likisaidia jamii katika nyanja mbalimbali ambapo jumla ya Sh.Milioni 150 zimetumika.
“ Tumetoa mifuko ya saruji 300 kwa Kata ya Kafunzo,ujenzi wa mabweni na vyumba vya madarasa,uchimbaji wa kisima cha maji katika Shule ya Sekondari Ilenza, Ujenzi wa Kituo cha Polisi,kuchangia madawati na ujenzi wa vyumba vya madarasa” amebainisha Tinda
Tinda amefafanuwa kuwa shamba limeruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo cha muda mfupi katika maeneo ya wazi na yenye miche midogo na kutoa ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania, Fue Kandawala amemshukuru Rais Samia Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa kodi ya VAT kwenye miti iliyosimama pamoja na kupunguza tozo za halmashauri kutoka asilimia tano hadi tatu.





Discussion about this post