NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Nchi za NORDIC Anne Veathe Tvinnereim.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 8,2022 jijini Dodoma,Waziri Jafo alishukuru Norway kwa ushirikiano wake kwa Tanzania hatua iliyochangia maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu na kusema ushirikiano huo uliodumu kwa takriban miaka 55 uendelee.
Amesema uhifadhi wa mazingira unaoonekana ni kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inakuwa salama katika sekta ya mazingira.
Dkt. Jafo amesema Serikali ya Tanzania inatarajia kushirikiana na Serikali ya Norway katika usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali zinazopatikana baharini bila kuathiri hifadhi ya mazingira.
Aidha ameongeza kuwa upo mpango kazi wa kuhakikisha mazingira ya bahari yanakuwa salama dhidi ya changamoto ya taka za plastiki ambazo ni hatari kwa maisha ya viumbe wa baharini.

Kwa upande wake Waziri Tvinnereim amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais katika kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira.
Amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwani imeweza kuandaa Sera ambazo zinachochea katika kulinda na kuhifadhi mazingira.
Pia waziri huyo aliahidi kuwa Serikali ya Norway iko tayari kuongeza nguvu katika jitihada zinazofanyika hapa nchini ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania inapata matokeo mazuri katika uhifadhi wa mazingira.
Naye Balozi wa Norway Elisabeth Jacobsen ameisifu Tanzania kwa jitihada za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikihatarisha usalama wa chakula.




Discussion about this post