NA GOODLUCK HONGO
SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) limeomba kuwepo kwa lugha za alama katika taarifa mbalimbali zinazotolewa kwa jamii kupitia vyombo vya habari ili waweze kupata haki zao.
Mbali na haki zao lakini pia uwepo wa ukalimani wa lugha kwa ajili ya walemavu wakiwemo wa kusikia utasaidia kujikinga dhidi ya hatari inayoweza kuwakuta ikiwemo milipuko ya magonjwa kama UVIKO 19.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Septemba 13,2022 wakati wa maandalizi ya siku ya Watu wenye Ulemavu wa Kusikia (VIZIWI) inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba Mosi,Mwenyekiti wa shirikisho hilo Taifa Ernest Kimaya amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa haki za watu wenye ulamavu zinapatikana.
Amesema moja ya matukio makubwa ambayo yaliwaathiri sana walemavu ni taarifa za ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo taarifa nyingi zilizotolewa kwa vyombo vya habari hazikuwa na lugha ya alama kwa maana nyingine ukalimani kwa ajili ya walemavu.
“Sisi kama SHIVYAWATA tunawaunga mkono wenzetu wenye ulemavu wa kusikia(VIZIWI) kuelekea kwenye maadhimisho yao lakini pamona na serikali kutuunga mkono lakini ni muhimu suala la ukalimani wa lugha likapewa kipaumbele kwenye vyombo va habari”amebainisha Kimaya
Kwa upande wake Mratibu wa Idara ya Jinsia (Wanawake,Vijana,Wazee na Watoto) kutoka Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Lupi Mwaisaka amebainisha kuwa VIZIWI bado wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa habari hasa vinazohusu afya zao na familia.
“Kila mmoja anatambua kuwa ulimwengu ulikumbwa na tatizo la ugonjwa wa UVIKO 19,janga hili bado lipo na linachukuliwa kwa tahadhari kubwa na habari za tahadhari hizi jamii ya VIZIWI bado hazijawafikia ikiwemo elimu juu ya kinga na chanjo yake.
“CHAVITA imeandaa mkakati wa kuwafikishia VIZIWI taarifa sahihi ili wajiandae kwa kuwa janga hili hujitokeza mara kwa mara kwa njia ya mlipuko”amesema Mwaisaka
Mwaisaka amebainisha kuwa CHAVITA kwa kushirikiana na Wizara a Afya kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wanaendesha kampeni ya uhamasishaji wa elimu sahihi juu ya chanjo ya UVIKO 19 kwa jamii ya viziwi katika mikoa mitatu ya Arusha,Mwanza na Mbeya
Naye Mwanasheria wa CHAVITA Novath Rukwago amefafanuwa kuwa suala la watu wenye ulamavu wa kusikia kupata taarifa kwa kwa kutumia lugha zao lipo kisheria.




Discussion about this post